loader
Dstv Habarileo  Mobile
Makamu wa Rais China kutembelea Tanzania

Makamu wa Rais China kutembelea Tanzania

Alisema lengo la ziara hiyo ni kuimarisha mahusiano ya karibu na ya kindugu kati ya nchi hizi mbili, ambayo mwaka huu yamefikisha Miaka 50 tangu kuasisiswa rasmi mwaka 1964.

Aliongeza kuwa Li Yuanchao atawasili nchini kupitia Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), ambapo atatembelea vivutio vya utalii vilivyopo Mkoa wa Arusha, hususani Bonde la Ngorongoro Juni 22 na jioni atawasili jijini Dar es Salaam kuendelea na ziara hiyo.

“Kama mnavyojua ziara hii inakuja wakati muafaka ambapo tunaelekea katika kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Tanzania” alisema Shimbo.

Aidha, akiwa Dar es Salaam atakutana na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa kitaifa kati ya Juni 23 na 26 mwaka huu na kufungua jukwaa la kiuchumi kati ya Tanzania na China.

Miongoni mwa viongozi atakaokutana nao ni Rais Jakaya Kikwete, mwenyeji wake Dk Mohamed Gharib Bilal na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Pia, atatembelea Zanzibar Juni 25 ambapo atakutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Idi na kurejea Dar es Salaam Juni 26 tayari kwa safari ya kuelekea China.

Aliongeza kuwa Tanzania na China, zimekuwa zikishirikiana katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kisiasa na hili linadhihirishwa na mikataba takribani 17 ambazo nchi hizi zilikubaliana Machi 2013 wakati wa ziara ya Rais wa China, Xi Jinping.

Mazungumzo kati ya Makamu huyo na viongozi wakuu wa kitaifa yatajikita zaidi katika kuimarisha zaidi ushirikiano uliopo wa kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Balozi wa China nchini, Lu Youqing alisema lengo kubwa la ziara ni kuongeza uhusiano baina ya China na Tanzania, ambao umedumu kwa miaka mingi.

Alisema na hii itakuwa ni muhimu wakati China na Tanzania wanasherehekea miaka 50 ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili. Pia, alisema ziara hiyo sio tu kwa ajili ya kubadilishana mawazo katika maendeleo na kupunguza umasikini, bali wataweza kuhamasisha wawekezaji wa China na kampuni, kuungana na Tanzania na kusaidia kuleta maendeleo.

foto
Mwandishi: Sophia Mwambe

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi