loader
Dstv Habarileo  Mobile
Mashehe, mapadri waionya NEC

Mashehe, mapadri waionya NEC

Aidha, wameshauri siku itakayochaguliwa kwa ajili ya kupiga kura, itangazwe kuwa ni siku ya mapumziko ili kutoa fursa kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi katika mchakato wa kupata viongozi wa ngazi mbalimbali nchini kwa njia ya kidemokrasia.

Ushauri huo ulitolewa jana katika mkutano wa viongozi wa dini na NEC kwa ajili ya kuwashirikisha viongozi hao kuhamasisha waumini wao kushiriki katika uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura unaotarajiwa kufanyika Septemba mwaka huu.

Walisema kwa kufanya uchaguzi siku isiyo ya ibada, itawezesha waumini wengi kujitokeza kupiga kura.

Mchungaji Benard Kingo wa Kanisa la EAGT alisema ni vema kuangalia siku hiyo ya kupiga kura, isiingiliane na siku ya ibada. Alisema ni vema kuiweka katikati ya wiki, hivyo kusaidia kuongeza idadi ya wapigakura.

Mwenyekiti wa Tume, Jaji mstaafu Damian Lubuva alikubali kupokea ushauri huo na kueleza bayana kuwa kufanya uchaguzi siku za ibada imekuwa ni mazoea.

Lakini, alisema katika baadhi ya nchi walizotembelea, wamekuwa wakifanya uchaguzi katikati ya wiki na kufanya siku ya mapumziko.

Aidha, baadhi ya viongozi hao wameishauri Tume kutotumia walimu katika kuboresha Daftari hilo au kusimamia upigaji kura, bali wawatumie wasomi katika maeneo husika, ambao hawana ajira.

Ushauri huo ulitolewa na Mchungaji Aguttu Oballa wa Kanisa la Mennonite Sinza, aliyeeleza kuwa walimu hao tayari wako kwenye ajira, lakini wapo wasomi wengi katika maeneo husika wa kidato cha sita hata chuo kikuu, ambao wangesaidia kufanya kazi hiyo kwa ufanisi.

“Kutokana na ukubwa wa suala hili na kuhamasisha watu wengi kujitokeza ni vema mkawaangalia wasomi waliopo mitaani, kusaidia kwa kuwapa ajira hiyo ya muda ili kuongeza kipato na siyo kuwatumia walimu mara zote ambao tayari wako kwenye ajira,” alisema.

Shekhe kutoka Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Mohammed Said aliishauri Tume kutumia wasomi ambao watakuwa makini, kwa kutowasumbua Waislamu kutoa kofia na hijabu wakati wa upigaji kura, kama ilivyoagizwa na tume hiyo.

Alisema katika miaka ya hivi karibuni waumini wengi wa dini hiyo, wameshindwa kujitokeza kujiandikisha kupiga kura, kutokana na kutakiwa kutoa kofia au hijabu, jambo wanaloamini linakwenda kinyume na imani ya dini yao.

Akizungumzia suala hilo, Kamishna wa Tume hiyo Zanzibar, Mchanga Hassan Mjaka alisema kinachotakiwa katika picha ni sura ya mtu, hivyo haitakiwa waumini kutolewa mavazi hayo, isipokuwa wale wanaovaa mavazi ya kufunika uso na kuacha macho ndiyo watatakiwa kuvua. Alibainisha kuwa kwa mwaka huu, hatarajii suala hilo kutokea, kwani watawaelimisha watendaji.

Mratibu wa Baraza la Maaskofu wa Kikatoliki (TEC), Paulo Chilewa akiitaka NEC kuangalia namna ya kuhakikisha wanafunzi katika vyuo, wanaweza kupiga kura kwa kuandikishwa maeneo watakayokuwepo wakati wa kupiga kura.

Alisema katika uchaguzi uliopita, walibaini wanafunzi wa vyuo zaidi ya 100,000 walishindwa kupiga kura, kutokana na kujiandikisha vyuoni na wakati wa kupiga kura walikuwa katika majimbo yao.

Akizungumzia suala hilo, Lubuva aliwashauri wanafunzi hao kuhakikisha wanakumbushana kufanya utaratibu wa kubadilisha maeneo watakayokuwepo ili waweze kupiga kura.

Chilewa pia aliishauri NEC, kuongeza muda wa kujiandikisha katika daftari la wapigakura kuishia saa 12 jioni na sio saa tisa kama ilivyokuwa kwa vitambulisho vya taifa kuwawezesha wafanyakazi kushiriki baada ya kutoka kazini.

Awali, akifungua mkutano huo, Lubuva alisema viongozi hao wa dini watasaidia kuhamasisha waumini wao ambao ndio wapigakura, kujiandikisha katika daftari hilo la wapigakura ili kuongeza idadi ya wapigakura wenye sifa.

Mkurugenzi wa Uchaguzi, Julius Malaba alisema kwa kutumia viongozi hao walio karibu na wananchi kutasaidia kupeleka taarifa kwa urahisi na imani kubwa kwa wananchi wengi kwa wakati mmoja.

Uboreshaji wa daftari hilo la kupiga kura unatarajia kufanyika Septemba kwa Watanzania wote kujiandikisha upya na kupata vitambulisho vipya.

Hatua hiyo itasaidia kuondoa manung’uniko ya baadhi ya wanasiasa, wanaochukulia kushuka kwa idadi ya wapigakura nchini, kuwa kunatokana na wengi kunyimwa fursa ya kuandikishwa, wanayostahili kuipata.

HALMASHAURI ya Manispaa ya Morogoro imepata nmkopo ...

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi