loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Masimulizi ya Thabiti Kombo kuhusu kuchafuka kwa hali ya hewa kisiasa

Masimulizi hayo yanahusu mambo tofauti muhimu yaliyotokea na yeye akishuhudia au akiwa sehemu yake wakati wa ukoloni, harakati za ukombozi na hata baada ya uhuru, Mapinduzi ya Zanzibar, Uhuru wa Tanganyika na Muungano wa Tanzania hadi mauti yalipomfika Agosti 28, mwaka 1986.

Masimulizi yake ni marefu na yanahusu mambo mengi lakini leo tunaangalia mchafuko wa hali ya hewa ya kisiasa kwa mara ya kwanza na ya pili Tanzania, mabapo Shekhe Thabiti Kombo anasimulia kuwa wafitini hata baada ya kuuawa kwa Abeid Amaan Karume, bado hawakutosheka, walitaka tena kuangusha uongozi wa chama cha Afro Shirazi (ASP), kwa madai kuwa shida za wananchi zimezidi.

“Lakini wote tunajua mbinu hizi za kuzua maneno zinapangwa nje ya Zanzibar, na utekelezaji wake siku zote una lengo la kurudisha umwinyi visiwani humu (kwa kisingizio kuwa eti shida zimezidi),” anasimulia Shekhe Kombo.

Anaendelea kusimulia wakati akiwa hospitali kuuguza majeraha ya risasi ambayo aliyapata wakati Rais Abeid Amaan Karume akiuawa kwamba baada ya maziko ya Abeid Amaan Karume mkutano ulifanywa kufikiria ni nani atashika nafasi ya Karume japo kwa muda.

Anasema katika majadiliano hayo walikubaliana kwamba Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi ndiye ashike nafasi hiyo na baadaye akathibitishwa na kuteuliwa kuwa Rais wa Zanzibar, Rais wa ASP na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na pia Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Anasimulia kuwa njama za kuua Mapinduzi na kuvuruga Muungano hazikuishia hapo, bali njama nyingine na fitina za ndani kwa ndani nazo ziliingia ndani ya chama na kuondoa imani juu ya viongozi wa ASP na wakati mwingine hata kwa baadhi ya viongozi wa TANU.

“Ilifika mahali amani, masikilizano kwa vipindi virefu, mpaka watu wakaamini kuwa wananchi wa Zanzibar wanalaani Mapinduzi ya ASP, na wala hawautaki Muungano. Fitina kama hizo nilishawahi kusema hazikuanza leo wala jana, zilianza zamani sana na wakati huo siasa zilitikisa hata umoja wa ASP,” anasema na kuongeza kwamba siku hizi mivutano hiyo inayozaliwa na fitina huitwa “kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa”.

Kombo katika masimulizi yake ndani ya kitabu hicho anasema siku moja viongozi wa Zanzibar wasiopenda Muungano walimwambia kijana mmoja Mtanganyika, mwandishi wa habari magazetini na vijana wenzake wengine, wachache, waondoke visiwani humo kwa sababu hawatakiwi.

“Vijana hao wakafunga virago, wakaondoka kurudi Dar es Salaam na kutoa taarifa kwa Oscar Kambona ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na pia Katibu Mkuu wa TANU. Kwa upande wa Zanzibar taarifa hiyo nayo ikamfikia Abdalah Kassim Hanga aliyekuwa Waziri, hata hivyo wote hao walikuwa hawaupendi sana Muungano,” anasema Kombo katika masimulizi yake.

Kombo anaendelea kusimulia kwamba Mwalimu Nyerere alipozipata taarifa hizo aliziamini, kwa sababu aliwaamini viongozi hao (Kambona na Hanga), kwa kuwa walikuwa wanasikilizwa sana na kuaminiwa. “Mwalimu, aliudhika sana, akaitisha Baraza lake la Mawaziri ili wafanye shauri kama hapana budi wavunje Muungano kwa sababu Karume hataki Muungano, amewafukuza watu waliopelekwa kufanya kazi Zanzibar,” anasema Kombo.

Aliendelea kusema hali hiyo ikawa mshindo mkubwa, mawaziri wametaharuki, wakati huo yeye (Kombo) alikuwa Dar es Salaam, kwenye kikao cha Bunge na Lucy Lameck akapata wazo. “Kuna yule mzee, Katibu Mkuu wa ASP anaishi Dar es Salaam Club, pengine ingefaa tumwite tumuulize vizuri,” ilikuwa ni kauli ya Lucy kama anavyosimulia Kombo kwenye masimulizi yake.

Hivyo Kombo anasema aliitwa Ikulu, wakati huo ni saa tatu usiku, akawakuta mawaziri wamo katika mshangao, Hanga na Kambona wakawa wanazozana. “Nilikuambia tangu zamani mambo haya hayawi,” Kombo anawakariri akina Kambona na Hanga wakizozana. Anaendelea kusimulia: “Nyerere akaniambia, nimekuita hapa kukuambia Karume hataki Muungano.

Nikashangaa, nikamuuliza kwa nini? Nikamjibu pale pale kwamba Karume hawezi kufanya hivyo. Mwalimu akaniuliza. Nitajuaje? Nikamwabia nipe mtu niende naye Zanzibar, huyo mtu akamuulize Karume mwenyewe.” “Ndipo akainuka Michael Kamaliza, lakini hali yake ilikuwa mbaya, ikaonekana hawezi kwenda.

Nikapewa Mheshimiwa Rashid Kawawa, ndege ikatayarishwa tukaondoka kwenda Zanzibar. Tukafika tukamkuta Karume amelala, tukamgongea, akaamka. “Kawawa hakuchelewa, akautoa ujumbe wake. ‘Nimetumwa na Mwalimu Nyerere nije kukuuliza kama unautaka Muungano au huutaki, kwa sababu vijana walioletwa hapa kufanya kazi hizo za Muungano wewe umewafukuza kuwa inasemekana wewe huutaki Muungano.

“Karume akashangaa sana. Akasema ‘Astaghafirullah’ huku akielekea kibla. Akainua mkono wake juu, akasema, ‘Naapa kama hayo mambo unayoyasema mimi nayajua, ndiyo kwanza nasikia habari hii kutoka kwenu kwamba nimefukuza watu, wala sijui watu gani na sijasema siutaki Muungano. Kamwambieni Mwalimu Nyerere ni uongo mtupu, mimi nataka sana Muungano uwepo na uendelee,’” anasema Kombo katika masimulizi hayo akimkariri Karume.

Anasimulia kwamba hatua hiyo ikawafanya akina Kombo na Kawawa warejee Dar es Salaam usiku huo huo kurudisha majibu na waliporudi waliwakuta mawaziri bado wapo Ikulu wanawasubiri na ilikuwa saa tano usiku! Kawawa akatoa ripoti kwa Mwalimu kuwa maneno hayo ni uongo mtupu na hayajui mambo hayo.

“Nikamwambia Mwalimu, ‘Je, umesadiki maneno yangu kwamba hao ni watu wabaya wanaomsingizia?’ Mwalimu akafurahi sana, akanikumbatia, akanishukuru akasema ‘asante sana, umetusaidia msaada mkubwa’. Basi mawaziri wakaruhusiwa kurudi nyumbani kwao, ikawa kutokea hapo hali ya hewa ikatulia,” anasimulia.

Kuchafuka kwa mara ya pili Katika masimulizi yake Kombo anasema, kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa kulikuwa mwaka 1983, wakati ule fitina zilimzunguka Rais wa Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi tangu baada ya kuwepo kwa wimbi kubwa la kuukataa Muungano.

“Wimbi hili lilikuja na hoja kwamba eti, Muungano huo haukuja kwa utaratibu halali, na maneno mengine mazito ambayo hata mtu hujui yanatokea wapi. “Ukawapo mfarakano mkubwa kati ya kikundi likichomzunguka Jumbe na viongozi wengine wa Zanzibar na katika hali hiyo mashabiki wa nje na ndani wakain gilia kati vilevile na hali ya hewa kisiasa ikachafuka kweli,” anasimulia Kombo.

Mambo hayo yakajadiliwa kwa urefu na kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa mjini Dodoma mwishoni mwa mwaka 1983. “Mimi sikuwemo katika mkutano huo, nilikuwa Moshi KCMC nikifanyiwa upasuaji wa jicho. “Na kwamba yalikuwa yakiendelea mazungumzo makali ya siku nne, hatimaye Rais Jumbe akajiuzulu.

Ndipo Halmashauri Kuu ya Taifa ikaanza kujadili nani anayefaa kuongoza Zanzibar kwa muda wa miezi mitatu, kabla ya rais kuchaguliwa.

“Wakati wa majadiliano hayo nikakumbukwa tena, na mchango wangu wa fikira ukatakiwa, lakini wakati huo mimi niko Moshi naumwa, basi wakatumwa Daudi Mwakawago, Moses Nnauye na Lucy Lameck wakaja na ndege kunichukua,” anasema Kombo na kuendelea… Vijana wakanieleza kwamba Mwalimu ananitaka haraka Dodoma, ingawa anajua niko hospitali naumwa.

Tukaondoka tukafika Dodoma, nikaanza majadiliano na Mwalimu nyumbani kwa Mkuu wa Mkoa, Mama Anna Abdallah,” anasema Kombo kwenye masimulizi yake.

Anasema katika majadiliano yake na Mwalimu, alimueleza mawazo yake kwamba mtu anayefaa kuongoza Zanzibar wakati huo kwa utulivu ni Ali Hassan Mwinyi na Nyerere akamuuliza kutokana na hali yake ya ugonjwa kama anaweza kwenda kwenye mkutano akawaambie wajumbe jambo hilo.

“Nikajibu, ndiyo naweza. Basi nikaenda kwenye mkutano na hiyo ilikuwa siku ya nane, nikatoa pendekezo langu la Mwinyi, watu wote kwenye mkutano wakapiga makofi, wakashangilia, wakarukaruka na akinamama wakapiga vigelegele,” anasimulia Kombo. Anasema baada ya hapo Ali Hassan Mwinyi alipelekwa kwenye jukwaa na umati ukacheza naye kwa furaha, ndipo Mwalimu Nyerere akawauliza hakuna anayepinga? Wote wakajibu hakuna.

Akauliza tena, wote mnaafiki wakajibu wote tunaafiki, na mara ya tatu alipouliza hakuna aliyetokea kupinga. Anasema ndipo Nyerere akatangaza kwa niaba ya Halmashauri Kuu ya Taifa kwamba Ali Hassan Mwinyi ndiye Rais wa Zanzibar kwa muda wa miezi mitatu hadi uchaguzi utakapofanywa, na kwamba wakati huo yeye (Kombo) alikuwa haoni kwa sababu ya operesheni ya jicho.

“Nikamuuliza Mwalimu je, inatosha maana nataka kurudi hospitalini Moshi, akasema bado, mchukue Mwinyi hadi Zanzibar akalishwe amini mbele ya wazee na kukaa kwenye kiti chake ndipo urudi Moshi, utakwendaje Moshi na kuacha mambo katikati?” Anasema Kombo akikariri maeneno ya Mwalimu Nyerere.

Anasema alimpeleka Mwinyi Zanzibar na wazee wakafurahi, wakamwombea dua na kwa bahati nzuri Rais Mwinyi akafanikiwa kuzima moto ule wa hali ya hewa katika kipindi hicho.

“Utaona kwamba mara zote mbili hali ya kuchafuka kwa siasa Zanzibar zilisababishwa na watu wasioupenda Muungano, na hawakuupenda tangu zamani kwa sababu unaviza maslahi yao binafsi, wala usione ajabu kesho wakazuka wengine, lakini kamwe hawawezi kuuvunja Muungano wetu uliobarikiwa na Mungu, kuwe uwe na utakuwapo daima,” anasimulia hayati Thabiti Kombo.

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi