loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mauzo ya bidhaa nje yaongezeka mwaka hadi mwaka

Hiyo ina maana kuwa, bidhaa zinakuwa na soko la kubahatisha na linalotumia fedha nyingi kuifanya bidhaa ifahamike kupitia matangazo ya biashara. Wakati TBS ikitoa angalizo hilo kwa umma na wafanyabiashara, taarifa ya serikali kuhusu mwenendo wa thamani ya mauzo nje, kuanzia mwaka 1963 hadi 2012 inaonesha yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hivi karibuni, mauzo ya nje yaliongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 170 (takriban Sh 112,581,000,000) mwaka 1963 hadi Dola za Marekani milioni 248.45 (zaidi ya Sh 398,858,000,000) mwaka 1985.

Kadhalika, inaelezwa kuwa mauzo hayo yaliongezeka tena katikati ya miaka ya 1990 kutoka Dola za Marekani milioni 679.2 (Sh 1,092,040,000,000) na kufikia Dola za Marekani milioni 5,912 (Sh 9,508,270,000,000) mwaka 2012.

Sababu za kuongezeka kwa mauzo hayo zimeainishwa katika taarifa hiyo iliyofafanuliwa katika kitabu cha taarifa ya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kilichosambazwa kwa watu mbalimbali wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya muungano huo, Dar es Salaam.

Kitabu hicho kilichochapishwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinaonesha kuwa juhudi za kutangaza bidhaa za nchini nje ya nchi, pamoja na kuwajengea uwezo wajasiriamali wa ndani ndizo zinazosababisha kukua kwa biashara ya nje, hususan kipato kinachotokana na uuzaji wa bidhaa.

Lakini, wataalamu wa masuala ya biashara na uchumi wanasema biashara ya bidhaa inaweza kupata soko la uhakika na linalokua katika nchi zilizoendelea na zinazoendelea, nje ya mahali zinapozalishwa endapo zinakuwa katika viwango vya ubora vinavyokubalika kimataifa.

Aidha, inaelezwa kuwa, kama TBS inavyofanya katika kuhakikisha bidhaa za nje zisizo na viwango vya ubora vinavyokubalika ndani na katika mataifa mengine, haziingii nchini, ndivyo jinsi nchi nyingine zinavyozipima za Tanzania na kuruhusu au kukataa zisiingizwe nchini mwao.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Joseph Masikitiko, anafafanua kuwa ili bidhaa ya nchi moja iingie katika soko la ndani la nchi nyingine, ni lazima ihakikiwe ubora na mawakala wanaohusika na uhakiki huo katika nchi hizo. Anasema, mfanyabiashara mwerevu au mzalishaji anayetaka biashara yake ikue na kupata soko la uhakika, hawezi kukubali kusafirisha bidhaa zisizo na uhakika wa ubora kutoka nchi moja kwenda nyingine, kwa kuwa kufanya hivyo ni hasara.

“Kwa hapa nchini, tukigundua mfanyabiashara au mzalishaji wa bidhaa fulani ameingiza nchini ‘mzigo’ usio na viwango vya ubora vinavyotakiwa tunamchukulia hatua za kisheria, ikiwa ni pamoja na kumwamuru aurejeshe katika nchi alikoutoa kwa gharama zake mwenyewe,” Masikitiko anasema.

Anasema kama hiyo haitoshi, mfanyabiashara huyo anatozwa faini ya asilimia 15 ya thamani ya mzigo huo, ambao hata hivyo, kulingana na uamuzi wa Shirika la Viwango Tanzania, unaweza kuteketezwa kwa gharama za mfanyabiashara aliyeziingiza nchini. “Hivi ndivyo inavyokuwa. Hakuna uhakika wa biashara ya bidhaa ya ndani nje ya nchi kama bidhaa hazina ubora.

Tunavyozuia za wengine zisiingie kwa kuwa ni hafifu ndivyo na zetu zinavyoweza kukataliwa huko kwa sababu hizo hizo,” anasema. Anaweka wazi kuwa ili kuwa katika nafasi nzuri, mfanyabiashara kabla ya kuingiza au kutoa bidhaa zake nje anapaswa kuhakikisha kuwa zimethibitishwa ubora na kuonekana zinafaa kupelekwa katika soko la nje.

“Kwa wale wanaoziingiza, kunakuwa na mawakala wa kuzihakiki katika nchi zinapotoka, kuona kama zinakidhi viwango vya ubora. Zikishahakikiwa zinawekwa alama maalumu kuonesha kuwa zimethibitishwa ubora. Kadhalika, kwa wanaotaka kuzipeleka katika soko la nje, wanapaswa kuhakikisha kuwa zimehakikiwa na kuwekwa alama ya ubora.

“Vinginevyo, uzalishaji unakuwa ni kazi bure hasa zinapokamatwa katika nchi zinakopelekwa, kwa kuwa zinaweza kuharibiwa, mhusika kutozwa faini, kufungwa, au adhabu zote kwa pamoja, kulingana na sheria za nchi husika,” Masikitiko anasema. Matangazo na kukua kwa biashara.

Kwa mujibu wa mtandao wa majibu www.answers.com, kuna uhusiano kati ya kutangazwa kwa biashara na kukua kwa biashara husika, kwa sababu, wateja wapya wanaweza kusikia juu ya bidhaa zinazotangazwa katika biashara hiyo na kutamani kununua ili kuzitumia.

Wanapotamani wengi, kulingana na uwezo wa kipato chao, hufanya uamuzi wa kuzinunua, hivyo kumfanya muuzaji atimize lengo lake la kuuza. Inaelezwa kuwa, matangazo ya biashara yanayolenga bidhaa fulani, yanaweza kuifanya ipendwe zaidi na watu waliokuwa wakiitumia awali, hasa inapokuwa imeleta manufaa kwao lwa kuonesha thamani halisi ya fedha waliyotumia kuinunua.

Mtandao huo unaonesha pia kuwa, uhusiano wa matangazo ya biashara ya bidhaa na kukua kwa biashara hiyo kunategemea zaidi viwango vya ubora wa bidhaa husika.

Unasema, hata kama bidhaa itatangazwa mara ngapi, isipokuwa na viwango vya ubora vinavyoeleweka au vinavyotakiwa na watu wanaotegemea soko, kulingana na sheria za viwango vya ubora vya eneo husika, kukua kwake kunakuwa kwa kubahatisha na kwa muda mfupi, kwa sababu wateja hupeana taarifa za uzuri au ubaya wa bidhaa, hivyo kuamua kuzisusa.

“Kususwa kwa bidhaa sokoni ni uamuzi unaotekelezwa na wateja. Wateja wana nafasi na haki ya kuamua kuua soko la bidhaa moja na kukuza la bidhaa nyingine kulingana na viwango vya ubora wanavyoviona katika bidhaa hizo,” Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBS anasema.

foto
Mwandishi: Namsembaeli Mduma

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi