loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mavazi mtaji mkubwa kwa MC

MC mchafu ni kichefuchefu tosha kwa waandaaji wa shughuli na wageni waalikwa kutokukupenda. Inawezekana MC ukawa umevaa mavazi ya gharama lakini usijue namna ya kujipangilia ukaishia kuwa kituko mbele ya hadhira.

Ukijijulia MC namna ya kuvaa inayokupendeza, utajua kama ni suti ununue mtindo gani na kama ni gauni au sketi na blauzi, uvae za namna gani. Kuna baadhi bado hawajajua namna inayowapendeza na kuishia kuiga wengine na matokeo yake wanakuwa vituko mbele ya hadhira (wageni waalikwa).

Ni vizuri pia kujua uvae nini katika shughuli gani na nini usivae katika shughuli fulani, zipo nguo zisizofaa kabisa kuvaliwa kwenye sherehe ya kufundwa binti (kitchen party) na zipo zisizofaa kwenye harusi.

Kwa mfano, mara nyingi shughuli ya kufundwa binti ambayo huwahusisha zaidi wanawake na mabinti, mavazi mengi huwa ya asili kama vitenge, madera, khanga na nguo za asili.

MC hapa si vibaya ukatokea umetupia katika sehemu ya mavazi yako, kitu chenye utambulisho wa kiasili hata isipokuwa nguo kwani kwa sasa shughuli nyingi za namna hii, huwa na mavazi rasmi (Dress Code).

Ikiwa waandaaji wa shughuli wamebainisha kuwa kuna vazi rasmi ambalo halina nakshi ya uasili, basi MC hapa ndipo una fursa ya kutokea kiasili angalau kwa hereni, bangili, ushungi, mkufu, au vazi la kitenge.

Kama ni MC mwanaume (ambao pia wengi huitwa kuendesha kitchen party siku hizi) unaweza kutupia shati la kitenge ama suti (suruali na shati) lenye nakshi za asili na huwa inapendeza sana. Unaweza kuvaa namna hii pia katika sendoff party.

MC using’ang’anie kuvaa vazi la kitenge kwenye harusi kama ikiwa si vazi rasmi la shughuli. Katika harusi unaweza kutokelezea na vazi na usiku kwa wanawake ama vazi la kitenge lililoshonwa kwa umaridadi, kwa wanaume suti (iwe mchanganyiko au mfanano).

Baadhi yetu huwa tunavaa bila kujitambua wala kufahamu maana ya mavazi husika, nimekumbusha haya machache kwa kuwa ni muhimu sana MC kwenda na mazingira ya shughuli ili usiwe kituko mbele za watu. Inashauriwa kuvaa hivyo katika shughuli nilizodadavua hapo juu kwa kuwa zina maana yake.

Sherehe ya kufundwa binti ni sherehe ya kitamaduni hivyo ni sehemu ya utambulisho wa utamaduni wa binti husika lakini siku hizi sisi tumeifanya kuwa ya kisasa na kusahau maana yake.

Basi ikiwa waandaaji wa shughuli hawajawafunga watu katika mavazi hasa kulingana na ukweli kwamba sherehe nyingi hufanyika mijini ambako tuko mchanganyiko wa watu wengi, itoshe kukumbuka angalau kubaki na misingi ya maana ya shughuli husika.

MC jitambue na uzingatia sana mavazi kupendeza na kusababisha sherehe ipendeze vile vile maana MC ukiwa umevaa vibaya, ovyo ovyo, unaifanya sherehe ionekane ovyo pia. Kama una ushauri au maoni niandikie kwa namba ya simu 0715022555.

KWA sasa nchi nzima ...

foto
Mwandishi: MC GloTe

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi