loader
Mfumo wa umeme Dar kufumuliwa

Mfumo wa umeme Dar kufumuliwa

Mkakati huo wa Serikali ulibainishwa jana wakati wa warsha ya kupitia Ripoti ya Mradi wa uundaji wa Mpango Mkuu wa kuboresha Mfumo wa Umeme iliyotayarishwa na wataalamu wa Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) na Shirika la Umeme Tanzania(TANESCO) na kupitia Ripoti ya Mpango Mkuu wa Kuboresha Mfumo wa Umeme 2012 iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Ngosi Mwihava katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Kamishna Msaidizi wa Nishati anayeshughulikia masuala ya gesi, Norbert Kahyoza alisema warsha hiyo ni kwa ajili ya kupitia ripoti ya wataalamu ya namna ya utekelezaji wa mradi utakaosaidia kuboresha mfumo wa umeme na kuwezesha wananchi kupata umeme wa uhakika.

“Mradi huu utakapoanza kutekelezwa maeneo yaliyokuwa yakipata kero ya umeme kama vile kukatika katika wataanza kufurahia huduma bora zaidi. Kwa sababu baada ya warsha hii tutakuwa tumepata dira ya namna ya kuendeleza huduma ya nishati ya umeme,” alisema.

Alisema baada ya kukamilika kwa maandalizi ya mpango huo na kuanza kutekeleza mradi huo Watanzania watarajie kupata huduma bora zaidi za nishati ya umeme na kwamba upatikanaji mzuri wa umeme utawawezesha kutekeleza shughuli zao za maendeleo na kujikwamua na umasikini.

Alisisitiza kuwa, baada ya mpango huo kukamilika wataalamu watafumua miundombinu yote ya umeme na kisha kuweka mfumo uliobora zaidi na ndio maana serikali imejipanga na kuahidi kuwajibika kwa nafasi yake kwa kushirikiana na timu ya wataalamu kutoka JICA na washirika wengine wa maendeleo.

“Hadi hatua hii ni dhahiri serikali imedhamiria kuhakikisha inaboresha huduma za umeme hapa nchini. Ingawa serikali ina kiwango chake cha kutekeleza, ndio maana upande mwingine inawashirikisha wataalamu kutoka nje kama hao wa Japan, lengo ni kuhakikisha Watanzania nchi nzima wanapata huduma zilizobora zaidi,” alisema.

Kamishna Msaidizi wa Nishati, Innocent Luoga alisema warsha hiyo ni kwa ajili ya maandalizi ya Mpango Mkuu wa kuboresha umeme nchi nzima na kwamba utaanza kutekelezwa 2016 Dar es Salaam na Pwani na utadumu kwa miaka 24 hadi 2040.

“Mpango huu ni wa miaka 24, yaani kila mwaka miradi itakuwa ikitekelezwa katika maeneo mbalimbali mpaka kufikia nchi nzima Watanzania watakuwa wamepata huduma iliyo bora zaidi ya umeme, bila kero tena, mfano umeme kukatika, taa kuwaka kwa mwanga mdogo na changamoto zingine kama hizo,” alisema.

Mwakilishi Mkuu wa JICA Tanzania, Yasunori Onishi alisema sekta ya nishati imekuwa ni eneo muhimu katika ushirikiano baina yake na Tanzania kwa kile alichoeleza ni sekta muhimu katika kukuza uchumi na kuondoa umasikini na kuahidi kuwa JICA itaongeza wigo wa ushirikiano katika sekta hiyo.

Onishi alisema mahitaji ya umeme yanaongezeka na yataongezeka zaidi kutokana na kukua kwa haraka kwa uchumi wa Tanzania, hivyo ni vyema kuweka Mpango madhubuti utakaowaongoza wadau kuwekeza zaidi katika sekta hiyo sambamba na juhudi za serikali.

“JICA iko tayari kuwajibika kwa nguvu zote kwenye nafasi yake na naomba Serikali ya Tanzania pia kuwajibika katika nafasi yake ili kuhakikisha mradi huu unatekelezwa kwa mafanikio makubwa,” alisema.

Warsha hiyo imeshirikisha wadau kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Fedha, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Viwanda na Biashara, Shirika la Umeme Tanzania(TANESCO), Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Wakala wa Umeme Vijijini (REA), Mamlaka ya Udhibiti wa Umeme na Maji (EWURA), wataalamu kutoka Japan na JICA.

AS Tanzania celebrates its 60th anniversary of independence on ...

foto
Mwandishi: Angela Semaya

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi