loader
Mkenya kortini hasara ya bil 6.8/-

Mkenya kortini hasara ya bil 6.8/-

Onyango alifikishwa mahakamani hapo jana mbele ya Hakimu Mkazi Devotha Kisoka na kusomewa mashitaka saba chini ya Sheria inayosimamia huduma ya posta na mawasiliano ya kielektroniki pamoja na Sheria ya Uhujumu Uchumi.

Alisomewa mashitaka na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka akisaidiwa na Wakili Mwanaamina Kombakono na Mwanasheria Mkuu wa Mamalaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambaye pia ni Wakili wa Serikali, Jonnes Karungura.

Wakili Kweka alidai kati ya Julai 2010 na Novemba 2013 katika eneo la Kariakoo Dar es Salaam, kwa lengo la kufanya udanganyifu na kukwepa malipo, Onyango alitoa huduma za simu za kimataifa bila kutumia njia halali zilizotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Alidai kuwa, katika tarehe hizo Onyango alitoa huduma za simu za kimataifa bila kuwa na leseni kutoka TCRA.

Aliendelea kudai katika mashitaka mengine kuwa kati ya Januari na Novemba mwaka jana katika eneo la Kariakoo, Onyango alitumia kadi za simu namba 0778350683, 0778498179, 0774395401, 0774552099, 0774552122, 0774802243 pamoja na namba nyingine zote hazijasajiliwa.

Katika mashitaka mengine, Kweka alidaiwa kuwa, siku isiyofahamika Onyango alisimika na kuendesha mitambo ya mawasiliano ya kielektroniki yakiwemo makasha manne ya kadi za simu (Sim Box) bila kuwa na kibali kutoka TCRA.

Aidha alidai Novemba 22 mwaka jana katika eneo la Kariakoo Dar es Salaam, Onyango alitumia mitambo hiyo ambayo haijathibitishwa na mamlaka husika.

Kweka alidai kati ya Julai 2010 na Novemba mwaka jana, Kariakoo Dar es Salaam, bila kuwa na leseni, Onyango alichepusha mawasiliano ya simu ya kimataifa kwa kutumia njia ambazo hazijaidhinishwa na TCRA na kusababisha hasara ya Sh bilioni 6,842,880,000 kwa Serikali na mamlaka husika.

Mshitakiwa alikana mashitaka na upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Hakimu Kisoka alisema dhamana ipo wazi endapo mshitakiwa ataweka fedha taslimu Sh bilioni 3.4 mahakamani, awe na wadhamini wawili watakaotoa dhamana ya maneno ya Sh 50,000, mmoja awe mfanyakazi wa Serikali.

Mshitakiwa alishindwa kutimiza masharti hayo na kurudishwa rumande hadi Aprili 8 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.

MWENGE wa Uhuru unaendelea ...

foto
Mwandishi: Flora Mwakasala

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi