loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mkoa wa Mara unavyojiimarisha kiuchumi

Wastani wa pato la mtu mmoja mmoja kwa mwaka limeongezeka kutoka shilingi 741,357 (Kitaifa 869,436.30) kwa takwimu za mwaka 2011 hadi kufikia shilingi 946,107 huku kitaifa pato hilo likiwa shilingi 1,025,038 kwa takwimu za mwaka 2012.

Akizungumzia hali ya ukuaji wa uchumi wa mkoa wa Mara katika kipindi cha kuanzia Januari 2012 hadi Machi mwaka huu, Katibu Tawala wa mkoa wa Mara, Benedict Ole Kuyan anasema: “Kwa takwimu hizi, hii ni hatua kubwa kwa maendeleo ya wananchi wa Mkoa wa Mara.”

Ole Kuyan anafafanua kwamba sehemu kubwa ya pato hilo linawahusu wananchi walio katika sekta inayoajiri wengi, kilimo. Anasema ongezeko la pato limetokana na mkoa kuhamasisha wananchi wake kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za uzalishaji mali hususan kilimo, ufugaji, uvuvi, biashara na ajira za maofisini.

“Tumepata mafanikio makubwa tangu mwaka 2011 tulipoanza kutekeleza ilani ya uchaguzi ya chama tawala na hivyo tumeweza kukuza pato la mwananchi na mkoa kwa ujumla,” anasema. Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, idadi ya watu mkoani Mara imeongezeka kutoka 1,368,602 mwaka 2002 hadi watu 1,734,830.

Anasema kwa takwimu za sasa mkoa una ongezeko la asilimia 2.5 ya watu kwa mwaka. Mgawanyo wa watu na idadi yao kwenye mabano kiwilaya ni Bunda (335,061), Butiama (241,732), Serengeti (249,420), Tarime (339,693), Rorya (265,241), Musoma Vijijini (178,356) na Manispaa Musoma (134,327).

Anasema katika kipindi hicho, Januari 2012 hadi sasa mkoa umeweza pia kutekeleza kwa kasi mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN) na kuweza kukamilika kwa miradi kadhaa ya maendeleo katika sekta za maji, afya, miundombinu, kilimo, mifugo na elimu.

Katika utekelezaji wa BRN kimapato, Ole Kuyan anasema macho yameelekezwa kwa Mamlaka ya Mapato (TRA) ambapo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014 mkoa ulipanga kukusanya Sh 110,328,100,000.00, yaani Idara ya forodha na ushuru wa bidhaa Sh 95,180,600,000.00 na Idara ya kodi za ndani Sh 15,147,500,000.00.

Anasema malengo ya makusanyo ya mapato kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba 2013 ilikuwa ni kukusanya jumla ya Sh 54,466,700,000.00 (Idara ya Forodha na ushuru wa bidhaa Sh 47,577,700,000.00 na Idara ya kodi za ndani Sh 6,889,000,000.00).

Ole Kuyan anasema hadi kufikia mwezi Desemba mwaka 2013, mkoa ulikuwa umefanikiwa kukusanya kiasi cha Sh 41,897,217,687.50 (Idara ya Forodha na ushuru wa bidhaa Sh 35,840,617,687.50 na Idara ya kodi za ndani Sh 6,056,600,000.00).

“Katika ukusanyaji wa mapato kutokana na vyanzo vya ndani kwa Halmashauri za Mkoa wa Mara mwaka 2012/13 ilikuwa Sh 6,564,623,815.93 sawa na asilimia 65.4 ya makisio. Hii ni idadi kubwa kiasi ikilinganishwa na mapato ya Sh 6,386,501,284 ya mwaka 2011/12 sawa na asilimia 69 ya makisio na hivyo ongezeko la mapato ya ndani ni asilimia 2.8,” anasema.

Kwa upande wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali za mitaa, anasema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/14 Mamlaka za Serikali za mitaa zilikadiria kukusanya Sh 11,762,358,000 kutoka katika vyanzo vya ndani vya mapato na katika kipindi cha Julai- Desemba, 2013 halmashauri hizo zilikusanya Sh 4,016,095,008, sawa na asilimia 68 ya lengo.

Utekelezaji wa Matokeo Makubwa Sasa Katibu Tawala, Benedict Ole Kuyan anasema katika kipindi hicho wananchi kwa kushirikiana na mkoa wameweza kutekeleza miradi mingi ya kimaendeleo katika sekta zote muhimu za kijamii. Anasema hatua hiyo imewezesha Serikali na wananchi kuimarisha ujenzi wa miundombinu katika sekta ya elimu, ambapo wamejenga madarasa 37, nyumba za walimu 27, maabara za sekondari 24 na matundu ya vyoo 13 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Anasema wananchi wameonesha ushirikiano mkubwa kwa kuchangia michango yao ya kujitolea na Serikali kumalizia baadhi ya maeneo ya ujenzi na hivyo kufanikisha ujenzi wa miundombinu hiyo. Anasema kuimarika kwa miundombinu ya elimu, kumewezesha uwiano wa Mwalimu kwa wanafunzi kutoka 1:60 (mwalimu mmoja kwa watoto 60) kwa mwaka 2011 hadi kufikia uwiano wa 1:47 kwa mwaka huu.

“Viwango vinavyotakiwa ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi 25, lakini pia tulikuwa na uwiano wa vitabu wa 1:3 (mwanafunzi mmoja kwa vitabu vitatu) mwaka 2011, lakini hadi mwezi Machi mwaka huu uwiano wa kitabu kimoja kwa wanafunzi unazidi kuwa mzuri. Tunajitahidi tufikie uwiano wa kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja,” anasema.

Kwa upande wa madawati, anasema uwiano wa dawati kwa mwanafunzi umeendelea kubaki wa dawati moja kwa mwanafunzi mmoja (1:1) hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu. “Hii ni kutokana na wazazi kuchangia dawati wakati watoto wao wanapojiunga shuleni na tunawashukuru kwa kuchangia katika suala la madawati,” anasema.

Anasema kumekuwepo na upungufu wa idadi ya wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza, ambao wamepungua kutoka 26,022 mwaka 2012 hadi kufikia 17,335 ikiwa ni sawa na asilimia 38.2 ya wanafunzi 45,351 waliotahiniwa kwa mwaka jana.

“Viwango hivyo ni chini ya lengo lililowekwa katika Mkakati wa Taifa wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (Mkukuta) kwa asilimia 6.8, ikiwemo changamoto ya upungufu wa walimu kwa shule za msingi na sekondari na hasa wa masomo ya Hisabati, Kiingereza na Sayansi,” anafafanua.

Anasema kumekuwepo pia na upungufu wa vitendea kazi kwa Maofisa Elimu Sekondari, miundombinu na vifaa vya kufundishia na kujifunzia. Anasema mikakati iliyopo ni kuendelea kushirikiana na wananchi katika kuimarisha miundombinu mbalimbali katika taasisi za elimu, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa samani na vifaa vya kufundishia mashuleni.

Lingine anasema ni kuhamasisha wananchi kufuatilia mahudhurio na maendeleo ya wanafunzi shuleni. Vifo vya uzazi vyapungua Anasema mkoa umepunguza vifo vitokanavyo na uzazi kutoka jumla ya vifo 121 kwa mwaka 2012 hadi vifo 97 kwa kila akinamama 100,000 kwa mwaka jana.

Anasema kupungua kwa hali hiyo kumetokana na kiwango cha wajawazito wanaojifungulia kwenye vituo vya tiba kuongezeka na kufikia asilimia 37 kwa mwaka jana.

Kwa upande wa chanjo, Katibu Tawala wa mkoa wa Mara, Benedict ole Kuyan, anasema kiwango cha utoaji chanjo kwa watoto wenye umri chini ya mwaka mmoja kimeongezeka hadi kufikia asilimia 90 kwa mwaka 2013 na hivyo kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka 5 hadi kufikia 62 kwa kila watoto 1,000.

Anazitaja aina za chanjo zilizopokelewa na mkoa na kusambazwa kwa kila robo mwaka kuwa ni Kifua Kikuu (BCG) 15030, Polio (OPV) 24715, Pentavalent (DPT-HB) 21900, Surua 7940, Surua ya Pepopunda (TT) 15,690, Nimonia (PCV) 125830 na Rotavirus 113775. “Chanjo hizi zimetolewa kwa watoto wote walio na mahitaji.

Wakati wote mkoa utahakikisha zinakuwepo chanjo za kutosha kabisa,” anasema. Mkoa wa Mara una hospitali nane, vituo vya afya 36 na jumla ya zahanati 224. Kadhalika mkoa una asilimia 66 ya watumishi wa afya na hivyo unajitahidi katika kupambana na upungufu huo wa wahudumu.

“Tunaendelea na uboreshaji wa vituo vya afya kwa Manispaa ya Musoma na maeneo mengine. Vi tuo vinavyoboreshwa ni vya Nyasho (Musoma Mjini), Murangi na kituo cha Kiagata kilichoko katika wilaya ya Butiama. Vituo vingine vinavyoboreshwa ni vya Kinesi na Changuge wilayani Rorya na hatua hiyo inaendelea kwa wilaya za Serengeti, Bunda na Tarime,” anasema Ole Kurian.

Anasema mkoa umeendelea kuwasajili wajawazito na kuwafuatilia ili kuhakikisha kuwa wanajifungulia katika vituo vya afya na zoezi hilo pia limeanza katika halmashauri za Bunda na Musoma Vijijini. Anasema kituo cha damu salama kimeanzishwa katika eneo la hospitali ya mkoa sanjari na ufuatiliaji wa vifaa vya upasuaji wa damu kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

“Vifaa vyote vimekwishaletwa na vimesambazwa katika halmashauri zetu zote na tumeanzisha kitengo cha kuhudumia wagonjwa wa dharura maarufu kama ‘baba yale’,” anasema.

Katika kutokomeza maambukizi mapya ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Ukimwi (VVU), Ole Kuyan anasema kwa mwaka wa fedha wa 2013 mkoa umeongeza vituo vya kutolea huduma ya ushauri kutoka 41 hadi kufikia vituo 48 “Vilevile kuna vituo 10 vya huduma ya ushauri/nasaha, upimaji na utoaji wa dawa kwa wenye maambukizi ya VVU,” anasema na kuongeza kuwa Kata 10 kati ya 13 zinatoa huduma ya wagonjwa majumbani katika Manispaa ya Musoma na kata nane kati ya 17 katika wilaya ya Musoma Vijijini.

Kadhalika kuna kata nane kati ya 17 wilayani Butiama na Kata 12 wilayani Bunda, 24 wilayani Tarime, Rorya kata 21 na Serengeti kuna jumla ya kata 14 ambazo hutoa huduma hizo,” anasema.

Kwa upande wa Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM), Ole Kuyan anasema katika mwaka wa fedha wa 2013/14 hadi mwezi Machi, mkoa umetumia kiasi cha Sh 3,987,199,000 kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ambapo umejenga zahanati 39, vituo vya afya viwili, nyumba za watumishi 64 na kukarabati zahanati 83, vituo vya afya 15 na ukarabati wa majengo mengine unaendelea na uko katika hatua za mwisho.

Changamoto ya maji Anasema kiwango cha upatikanaji maji vijijini mkoani Mara kimeongezeka na kuwafanya wananchi wa vijijini na mijini kuondokana ama kupunguza adha upatikanaji wa maji katika mkoa huo ulio kando ya Ziwa Victoria. Anasema mwaka 2012 upatikanaji wa huduma ya maji vijijini ulikuwa uko kwa wastani wa asilimia 44.6 huku mijini ukifikia asilimia 53.

Anasema hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu, upatikanaji wa maji vijijini umeongezeka na kufikia wastani wa asilimia 45.5. “Kwa upande wa vijijini, wilaya ya Serengeti ndiyo inayoongoza kwa asilimia 57.2 ya upatikanaji wa maji, ikifuatiwa Bunda (asilimia 48.8), Butiama (47.4), Rorya (42.9) na Tarime asilimia 31.5,” anasema.

Kwa upande wa mijini upatikanaji wa maji Ole Kuyan anasema umefikia asilimia 53.5, ambapo Manispaa ya Musoma inaongoza kwa asilimia 76, ikifuatiwa na mji wa Mugumu asilimia 60, Tarime 48 na Bunda asilimia 29.9. Anasema miradi mingine ya maji inatarajia kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.

Anasema kuwa mkoa unaongeza juhudi ili kuhakikisha kuwa lengo la taifa la kuongeza huduma ya maji safi na salama kufikia asilimia 65 vijijini na 75 mijini linakamilika ifikapo mwaka 2015.

“Katika kutekeleza mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN), ujenzi wa jumla ya miradi ya maji 25, mitano kwa kila halmashauri iliyopangwa kutekelezwa katika awamu ya kwanza iliyokuwa inatarajia kukamilika mwezi Desemba mwaka jana katika vijiji vya Korotambe, Nyagisa na Natta Motukeri imekamilika na miradi mingine imekamilika kwa asilimia 100,” anasema.

Kuhusu ujenzi wa vituo vya kuchotea maji, anasema lengo la mwaka 2013/14 lilikuwa ni kujenga vituo 142, na kwamba hadi kufikia mwezi Desemba mwaka 2013 mkoa ulijenga vituo 235 ikiwa ni sawa na asilimia 165.5.

Anazitaja changamoto zinazoukabili mkoa kuhusu upatikanaji wa maji vijijini ni kuwepo kwa wizi na uharibifu wa miundombinu ya maji unaofanywa na baadhi ya watu wasio waaminifu, uharibifu wa mazingira unaosababisha kukauka kwa vyanzo vya maji na ubora wa maji. “Kumekuwepo na ushiriki duni kwa wananchi kuchangia mifuko ya maji.

Hii imesababisha uharibifu wa mitambo ya kusukuma maji na mabomba na dhana iliyopitwa na wakati ya wananchi kuendelea kushinikizwa wapatiwe huduma ya maji bure. Changamoto nyingine ni upungufu mkubwa wa wataalamu kwenye sekta ya maji kwa upande wa halmashauri na wilaya zetu,” anasema.

Kwa upande wa mijini, anasema changamoto iliyopo ni kuwepo kwa ufanisi mdogo wa makusanyo, ubora wa maji yanayotolewa, upotevu mwingi wa maji unaosababishwa na uhaba wa dira za maji na hujuma ndogondogo za miundombinu ya maji.

“Tunajitahidi kukabiliana na changamoto hizi kwa kujenga miradi mipya ya maji. Tunahimiza utunzaji wa ardhi na vyanzo vya maji vilivyopo ili kuhifadhi maji mengi na yenye ubora katika vyanzo vyetu vya maji,” anasema. Anasema mkoa umekamilisha ujenzi wa Kivuko cha MV- Musoma kinachofanya kazi kati ya Mwigobero, Musoma Mjini na Kinesi wilayani Rorya kwa gharama ya Sh 2,367,819,329.

Anasema ukamilishaji wa ujenzi wa kivuko hicho ni ahadi iliyotolewa na Serikali kuwajengea wananchi wa maeneo hayo kivuko hicho ili waweze kukitumia katika shughuli za usafirishaji ili kuboresha vipato vyao. Anasema kuwa kivuko hicho chenye tani 85 kina uwezo wa kubeba watu 330, magari 10 aina ya Station Wagon na mizigo mingine kwa wakati mmoja.

“Kukamilika kwa kivuko hiki kumeondoa adha kwa wananchi waliokuwa wanazunguka umbali wa kilometa 54 kwenda eneo la umbali wa kilometa saba tu, hivyo kuwapunguzia gharama kubwa waliyokuwa nayo na muda na kimeepusha ajali zilizokuwa zinatokana na mitumbwi iliyokuwa ikipoteza maisha ya watu kutokana na kutokuwa imara ama kujaza abiria na mizigo kupita uwezo,” anafafanua.

Anasema kukamilika kwa ujenzi wa kivuko hicho kumeongeza ajira kwa wananchi ambao hufanya biashara ndogondogo zilizoboresha maisha yao, na wana uwezo wa kusafirisha mazao yao ya samaki, maziwa na ya nafaka kwenda kwenye masoko.

Anasema changamoto iliyopo ni baadhi ya wavuvi wanatega nyavu zao kwenye njia ya kivuko ambazo hunasa kwenye propela ya injini na kusababisha uharibifu na hivyo kulazimika kutumia fedha nyingi kwa ajili ya matengenezo na wakati mwingine kuahirishwa mara kwa mara kwa safari.

Ujenzi wa Mwalimu Nyerere Medical Centre Anasema zaidi ya Sh bilioni 37 zitatumika katika kujenga hosipitali ya mkoa wa Mara, itakayojulikana kwa jina la Muasisi wa taifa letu, “Mwalimu Nyerere Medical Centre katika eneo la Kwangwa, nje kidogo ya mji wa Musoma. Anasema mkoa umeamua kuendeleza majengo ya hospitali ya Kwangwa kwa kuifanya kuwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mara, ambayo itakuwa na uwezo wa kutoa huduma za kibingwa katika fani zote muhimu.

“Hospitali hii itajengwa kwa awamu tatu, awamu ya kwanza ambayo itakuwa ni kukamilisha ujenzi wa jengo lililopo utagharimu kiasi cha Sh bilioni 37, ambapo awamu ya pili itakuwa ni kujenga chuo cha wataalamu wa afya kwa kujenga madarasa, hosteli za wanafunzi na nyumba za wafanyakazi,” anasema.

Anasema awamu ya tatu itahusisha ujenzi wa miundombinu na kuajiri wataalamu ili kuiwezesha hospitali hiyo kuwa na kitengo maalumu cha kutibu magonjwa ya figo. “Baada ya hospitali hii kukamilika, hospitali ya sasa ya mkoa itakuwa ya Manispaa ya Musoma,” anasema.

Anasema katika mwaka wa fedha 2012/13 serikali ilitoa kiasi cha Sh bilioni 2.1 na mwaka 2013/14 ilitenga kiasi hicho kwa ajili ya kuanza ujenzi wa hospitali hiyo, ambapo mkoa umeamua kuanza ujenzi kwa kujenga ghorofa ya chini na ya kwanza.

“Zabuni ya ujenzi ya awamu ya kwanza ilitangazwa na mkandarasi anatarajiwa kuanza ujenzi mwanzoni mwa mwezi Mei mwaka huu na hadi sasa ujenzi wa kuzunguka eneo la hospitali umeanza na unaendelea,” anasema Chuo Kikuu Butiama.

Kwa upande wa elimu ya juu, anasema mkoa umeazimia kuanzisha Chuo Kikuu katika wilaya ya Butiama kwa ajili ya kumuenzi Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere “Chuo hicho kitakuwa Chuo cha Sayansi, teknolojia na ubunifu kikiwa na mchepuo unaendana na masuala ya kilimo,” anasema na kuongeza kuwa eneo la ujenzi kwa ajili ya chuo hicho limekwishapatikana huku Mamlaka za Serikali za mitaa mkoani humo zikiwa tayari zimetoa maeneo kwa ajili ya ujenzi wa vitivo vya chuo.

Gharama za ujenzi wa chuo hicho zitafikia kiasi cha Sh 283,343,738,563. Kuhusu vivutio vya uwekezaji anasema mkoa una eneo la hekta 1,115,035 linalofaa kwa kilimo lakini ni hekta 512,537 zinazolimwa sasa, sawa na asilimia 46 ambapo hekta 210,000 zinafaa kwa kilimo cha umwagiliaji ingawa ni hekta 4,600 sawa na asilimia 2.1 ndizo zinamwagiliwa.

“Mkoa una zaidi ya mifugo 2,212,256, ng’ombe 1,330,901, mbuzi 640,744 na kondoo 240,611. Uwekezaji unawezekana kwenye viwanda vya nyama, maziwa na bidhaa nyingine za mifugo, uhamilishaji na unenepeshaji wa mifugo,” anasema.

Anasema mkoa una utajiri mkubwa wa madini, hususan dhahabu, chokaa, vito na madini ya ujenzi yakiwa yamesambaa karibu robo tatu ya eneo la ardhi la mkoa. Anasema wapo wachimbaji wazalendo wenye maeneo yenye madini na wanakaribisha wabia kuwekeza.

Anahitimisha kwa kusema: “Ni mkoa pekee unaohifadhi mazalia ya samaki walioadimika aina ya sato, gogogo, nembe, ningu na samaki aina ya perege. Uwekezaji kwenye ufugaji wa samaki ndani ya eneo la Ziwa Victoria unawezekana.”

UJENZI wa mfereji wa Suez nchini Misri ulioanza mwaka 1859 ...

foto
Mwandishi: Nashon Kennedy

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi