loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

‘Mlio kazini baada ya kusoma kwa mkopo rejesheni pesa’

Mikopo hiyo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ilianzishwa mwanzoni mwa miaka ya 1990 baada ya kuanzishwa kwa sera ya uchangiaji ambapo mwanafunzi na mzazi wake walipaswa kulipia sehemu ya gharama za vyuo.

Awali, mpango huo wa uchangiaji uliokuwepo baada ya Azimio la Musoma la mwaka 1974, wanafunzi walitakiwa kufanya kazi miaka miwili baada ya kumaliza kidato cha sita na kupitia mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ndipo wajiunge na vikuu na vile vya elimu ya juu.

Mfumo huo ulibadilika na ndipo mwaka 1992, Serikali ilianzisha sera mpya ya uchangiaji wa elimu ya juu. Chini ya sera hiyo, wanafunzi walinza kulipia gharama za nauli za kwenda na kurudi chuoni, ada za maombi na kuandikishwa chuoni pamoja na ada ya serikali ya wanafunzi. Pia walilipia gharama za matibabu, gharama za kitambulisho na ada za mitihani.

Baadaye mwaka 1994, wanafunzi na wazazi waliongezewa mzigo mwingine wa uchangiaji na kuanza kulipia gharama za malazi na chakula, ambazo awali zilikuwa zikitolewa na serikali kupitia vyuo. Kwa kuwa gharama hizo zilionekana kubwa na baadhi ya wanafunzi kushindwa kuzimudu, serikali ilianzisha mpango wa kuwakopesha kupitia iliyokuwa Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu.

Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi na mahitaji ya mikopo, serikali iliamua kuanzisha Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) mwaka 2005.

Malengo ya kuanzishwa kwa bodi ni kuwa chombo cha kusimamia uendeshaji wa mfuko wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na kuweka utaratibu wa kuwatambua wahitaji wa mikopo, kupokea, kuchambua maombi na kutoa mikopo kwa waombaji wahitaji, na kuweka kumbukumbu za wanafunzi wanaokopeshwa, na ukusanya marejesho ya mikopo yote iliyotolewa tangu mwaka 1994.

Chini ya utaratibu huo mpya wa utoaji mikopo kupitia bodi, wanafunzi wanatakiwa kuchangia ada za mafunzo, utafiti, mahitaji maalum ya vitivo na mafunzo kwa vitendo. Tangu kuanzishwa kwa mpango wa ukopeshaji wa wanafunzi kupitia serikali na baadaye bodi, jumla ya sh. 1,843,483,686.58 zimetolewa kwa wanafunzi 260,150 wahitaji waliohitimu na walioko katika taasisi za elimu ya juu.

Kiasi hicho cha fedha ni hadi Desemba, mwaka jana. Pamoja na kukopeshwa, wanafunzi wanaohitimu wanapewa muda maalum wa kuanza kurejesha ambapo Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Cosmas Mwaisobwa, anasema kuwa urejeshaji huo umeanza kuwa na mafanikio.

Anasema hadi Desemba, mwaka jana, urejeshaji wa mikopo ulifikia asilimia 64 ya fedha zinazotakiwa kurejeshwa na kwamba hayo ni mafanikio makubwa ikizingatiwa kuwa mwaka 2007 urejeshaji huo ulikuwa asilimia 0. “Bodi ilifanikiwa kurejesha Sh 43,013,087,604.12 hadi Desemba 31, 2013 kutoka kati ya Sh 68,436,028,641.95 zinazostahili kuwa zimerejeshwa. Kwa jumla haya ni mafanikio makubwa,” anasema.

Pamoja na mafanikio hayo, Mwaisobwa anasema wakati leo nchi inasherehekea Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani bado zipo changamoto kadhaa zilizojitokeza hivyo kusababisha kutofikiwa malengo yaliyokusudiwa katika urejeshaji wa mikopo kutoka kwa wahusika na hata kupunguza kasi ya uendeshaji wa bodi.

Anazitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na za kisera ambapo sera ya uchangiaji wa elimu ya juu bado haijakubalika kama ilivyo kwa sehemu zingine kama vile maji, afya, elimu ya msingi na sekondari. “Hatua hii imesababisha wanafunzi kuendelea kudai asilimia 100 katika vipengele vyote vya mikopo na hata kudai kupatiwa mikopo katika vipengele ambavyo haviko kwenye sheria iliyoanzisha Bodi ya Mikopo,” anasema.

Mkurugenzi huyo anasema katika kukabiliana na changamoto hiyo, bado kuna umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa umma na kwa wadau kuhusu umuhimu wa uchangiaji katika elimu ya juu ili sera hii iweze kueleweka, kuzoeleka na kukubalika. Anasema kumekuwa na mtazamo potofu kwa baadhi ya watu kuwa fedha zinazotolewa na bodi ni ruzuku badala ya mikopo.

Hali hiyo, anasema imesababisha waombaji wengi na wananchi kuendelea kudhani kuwa fedha zinazotolewa ni ruzuku. Kwa mujibu wa Mwaisobwa, na hali hiyo imesababisha kuongezeka kwa idadi ya waombaji mikopo ikijumuisha hata wale ambao wazazi wao wana uwezo wa kuwagharimia, na hata baadhi ya wazazi, walezi na waajiri na wafadhili kujitoa kugharimia watoto na wafanyakazi wao katika elimu ya juu, kwa kutegemea mikopo inayotolewa na bodi.

“Hii pia imesababisha wanafunzi kutaka kupewa mikopo zaidi hata katika maeneo ambayo wangeweza kuchangia. Katika hili tuna kazi ya kuhakikisha tunatoa elimu ili waombaji watambue kwamba fedha zinatolewa ni mikopo na si ruzuku. Hii itawezesha pia kasi ya ukusanyaji mikopo kuongezeka,” anabainisha.

Kuwepo kwa mikopo ya elimu ya juu, anasema kumesababisha baadhi ya vyuo kupandisha ada za mafunzo maradufu kwa lengo la kupata fedha zaidi kutoka bodi. Kutokana na hali hiyo, anasema bodi imekuwa na mzigo mkubwa na hata kutokuwa na uwezo wa kukopesha wanafunzi wengi zaidi.

Anasema hali hiyo itaondoka au kupungua iwapo serikali itaweka viwango elekezi vya ada kwa kila kozi inayotolewa na pia kuendelea kusimamia ukomo wa ada katika vyuo vya umma na kuendelea kuweka viwango vya mikopo ya ada kwa vyuo binafsi. Changamoto nyingine, kwa mujibu wa Mwaisobwa ni wanafunzi kuhama chuo au kubadilisha kozi walizopangiwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE).

Anasema wanafunzi wengi wa mwaka wa kwanza huhama kutoka vyuo walivyopangiwa na kwenda vyuo vingine na hivyo kusababisha malalamiko yasiyokuwa ya lazima kwa bodi kwa kuwa wakati huo bodi inakuwa imeshapeleka fedha zao katika vyuo walivyopangiwa.

Wanafunzi hao wakifika katika vyuo walivyohamia, kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, wanaanza kudai tena mikopo upya. Pia anasema kuna wanafunzi wanaohama kutoka kozi moja hadi nyingine kama ualimu, ili waweze kukopesheka na wakishafanya hivyo huanza kudai mikopo.

Tatizo la bajeti ni changamoto nyingine inayosababisha ufanisi wa mikopo kuwa mdogo. Hiyo ni kwa sababu bajeti ya fedha za ukopeshaji kuwa ndogo ikilinganishwa na mahitaji. Kuhusu ufinyu wa bajeti, Mwaisobwa anasema unatokana na kiasi kidogo cha fedha kinachotengwa katika bajeti ya serikali na pia ongezeko la udahili wa wanafunzi katika vyuo vya elimu ya juu.

Matatizo mengine ambayo yamekuwepo katika kufanikisha ukopeshaji ni ya kiutendaji ikiwemo wanafunzi kukataa au kuchelewa kusaini marejesho ya fedha zinazotumwa vyuoni.

Vyuo vya elimu ya juu kuchelewesha matokeo ya mitihani ambayo ndiyo yanayotumiwa na bodi katika kujua nani anaendelea na masomo, nani ameachishwa masomo, nani ameahirisha masomo ni tatizo kwani hatua hiyo huchelewesha utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo.

Sambamba na hilo, vyuo vimekuwa vinachelewesha uwasilishaji wa orodha ya wanafunzi wanaotakiwa kwenda kwenye mafunzo kwa vitendo na hivyo kuchelewesha utoaji wa mikopo hiyo kwa wakati na hivyo kuisababishia bodi lawama kutoka kwa wanafunzi.

Anasema vyuo vingi vya elimu ya juu huchelewesha uwasilishaji wa orodha ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliosajiliwa chuoni ambayo inapaswa kutumiwa na Bodi ya Mikopo katika utayarishaji wa malipo ya mikopo kwa wanafunzi hao kwa robo pili ya mwaka, hivyo kusababisha malalamiko ya wanafunzi.

Ugumu wa kuthibitisha taarifa za waombaji nalo ni tatizo kwani anasema kukosekana kwa vitambulisho vya utaifa kunafanya kazi ya uchambuzi wa taarifa za waombaji mikopo pamoja na urejeshwaji wake kuwa mgumu zaidi. “Kwa kuwa taarifa za aina hizo ndizo zinatakiwa kutumika katika mchakato wa kutambua uwezo wa waombaji mikopo.

Hii inasababisha malalamiko kutoka kwa waombaji juu ya hali na viwango vya uhitaji vinavyotolewa na chombo cha kupimia uwezo. Ufanisi wa utoaji na urejeshwaji wa mikopo unaweza kuwa mzuri iwapo jamii itatambua umuhimu wa uchangiaji wa elimu ya juu na pia taasisi husika na serikali kwa jumla zitawajibika ipasavyo.

Hata hivyo, suala la urejeshwaji wa mikopo kutoka kwa walionufaika linapaswa kupewa uzito unaostahili kwani fedha hizo zinahitajika ili kuweza kuwakopesha wanafunzi wengine ili wanufaike na elimu ya juu kwa maendeleo ya taifa.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi