loader
Dstv Habarileo  Mobile
Moto wateketeza vibanda 63 Dodoma

Moto wateketeza vibanda 63 Dodoma

Chanzo cha moto huo uliozuka usiku wa kuamkia jana, hakijafahamika na walioathiriwa ni wale wanaofanya kazi zao kwenye soko la Sarafina mtaa wa Relini kata ya Tambukareli. Wafanyabiashara walioathirika ni wale wa kuuza nguo, viatu, saluni, mafundi cherehani na mamalishe.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana, Mwenyekiti wa soko hilo, Azizi Msafiri alisema kuwa chanzo halisi cha moto huo hakijafahamika licha ya kuwa na tetesi kuwa ulisababishwa na hitilafu ya umeme.

Alisema hata mfumo wa kuunganisha umeme ni mbovu kutokana na wafanyabiashara wengi kujiunganishia umeme kiholela bila kufuata utaratibu wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco).

Alisema hata ukosefu wa barabara ulichangia moto huo kushindwa kuzimwa kutokana na mabanda mengi kujengwa kiholela.

“Kulingana hasara hii iwapo serikali itaturuhusu kujenga tena shughuli zote za ujenzi wa vibanda itabidi kufuata utaratibu ikiwemo kuweka miundombinu ya barabara na watu watatakiwa kuunganisha umeme kwa kufuata utaratibu,” alisema.

Mmoja wa wafanyabiashara aliyekuwa akiuza viatu, Neema Mdeche alisema kama miundombinu ya barabara ingekuwepo kikosi cha Zimamoto kingepata nafasi ya kuzima moto huo.

Alisema zimamoto ilifika kwa wakati lakini wameshindwa sehemu ya kupitishia mipira na hivyo kulazimika kuzima moto huo kupitia nje ya ukuta wa kanisa la Kilutheri ili kunusuru mabanda mengine yasiungue.

Kaimu Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, Regina Kaombwe aliziomba Mamlaka husika Manispaa na CDA ambazo zinatoa maeneo kuhakikisha wanatoa maeneo yenye miundombinu ya kupitisha magari.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema moto huo ulitokea saa 2.40 usiku wa kuamkia jana.

Chanzo cha moto huo hakijajulikana na polisi wanaendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo. Pia aliwataka wananchi na mamlaka husika kuhakikisha wanakuwa na mipango mizuri wanapojenga nyumba au vibanda vya biashara kwa kuhakikisha wanaacha nafasi ya magari ya huduma kama zimamoto na polisi.

Alisema moto huo ulishindwa kudhibitiwa haraka kutokana na waliojenga vibanda hivyo kutoweka njia ya magari ya zimamoto kuingia na kuzima moto huko.

foto
Mwandishi: Sifa Lubasi, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi