loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Msitu wa Rutamba walemewa na wavunaji haramu

Wavunaji hao huwalaghai wananchi wanaoendekeza njaa kwa kuwapa Sh 70,000 ili wawaoneshe miti ya mbao bila kufuata utaratibu. Mkazi wa kijiji cha Rutamba ya zamani, Rashidi Maiko, ameyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa kutambulishwa kwa Mradi wa Usimamizi na Ulinzi Shirikishi wa Rasilimali unaosimamiwa na shirika lisilo la kiserikali la PEMWA.

Mradi huo unaofadhiliwa na shirika la kimataifa lisilo la kiserikali la WWF umedhamiria kuokoa mazingira katika kijiji cha Rutamba, Lindi Vijijini, ambako pia kuna ziwa linalokabiliwa na uharibifu mkubwa wa mazingira. Maiko anaweka wazi kwamba wafanyabiashara, hususan wanaopenda kuvuna misitu kwa njia haramu, wamekuwa wakiwalaghai wananchi kwa kuwatumia kuwatafutia miti ya mbao baada ya kuwapa fedha.

Anasema wananchi na wafanyabiashara hao ‘wanaomaliza’ msitu huo wanafahamika lakini hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi yao na mamlaka husika huku msitu ukitoweka bila mapato kufahamika. Anasema kuwa wavunaji hao haramu wamekuwa wakitumia misumeno ya minyororo (chain saw) katika kukata mbao ambapo mapato yanayopatikana hayanufaishi jamii inayozunguka msitu huo.

Mkazi mwingine wa Rutamba, Bakari Juma, anasema kuna uvamizi mwingine unaofanywa na wananchi wanaofanya kilimo cha kuhamahama kwani wamekuwa wakivamia msitu huo kwa kukata miti bila ya utaratibu na hivyo kuufanya kuwa katika hatari ya kutoweka.

Anasema kwamba mbali na kilimo hicho cha kuhama hama uchomaji moto unaofanywa na jamii, hususan wakati wa kusafisha mashamba umekuwa pia ukiathiri msitu huo na viumbe vilivyomo kila mwaka.

Maule Mohammed ni mkazi mwingine wa eneo hilo ambaye anasema kwenye msitu huo pia kuna wawindaji haramu wanaoua wanyama kama tembo, chui na wanyama wingine jamii ya swala wanaoingia kwenye msitu huo mara nyingi wakitokea katika msitu mwingine wa Rondo.

Anasema kuwa uwindaji haramu katika eneo hilo umedumu kwa zaidi ya miaka 30 sasa, lakini hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa na mamlaka za msitu kudhiti jambo hilo. Hata hivyo, anasema pale mwananchi anapotaka kibali cha kukata miti kwa ajili ya kukarabati nyumba yake inakuwa vigumu sana kupata, lakini kwa wavunaji haramu wanaotoa ‘mlungula’ wanafika na kuingia msituni wanavyotaka.

Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Rutamba ya Zamani, Ali Ng’ombo, anathibitisha kuwapo kwa uvunaji wa msitu huo unaofanywa na watu wasiotaka kufuata taratibu. Anafafanua kwamba msitu unaovunwa ni ule unaomilikiwa na serikali kuu ambao uko chini ya Wizara ya Maliasili na Utaalii, na siyo ule ambao wananchi wenyewe waliubuni wa Nyang’anyi.

Anasema kuwa jamii haishiriki kikamilifu kufanya ulinzi shirikishi kwenye msitu huo kwa kilichodaiwa kuwa si mali yao bali kazi ya maliasili. Naye mtendaji wa kijiji cha Michee, Frank Kasanga, anathibitisha kuwapo kwa uvunaji haramu wa msitu wa Rutamba na Litipo unaofanywa na wafanyabiashara wasiotaka kufuata utaratibu.

Anasema kuwa kuna uvunaji na uwindaji haramu kwenye msitu huo, hali inayosababisha miti kukatwa ovyo na wanyama kukosa mazingira yao ya asili na hivyo kutoweka. Hata hivyo, anasema kuna wakati mamlaka huwa inaweka mitego ya kuwakamata wavunaji haramu, lakini jamii inatoa siri kwa watuhumiwa, kwa hiyo zoezi hilo linakwama.

Kasanga anasema kuwa iko kamati ya maliasili ambayo imekuwa ikisaidia suala zima la kupambana na wavamizi hao na hatimaye kuweza kuwakamata, lakini kumbukumbu zilizopo kwa siku za karibuni waliweza kukamata wahalifu watatu ambao walipigwa faini huku mbao zao ‘zikitaifishwa’.

Anasema kwamba wakati akianza kazi mwishoni mwa 2012 uharibifu wa msitu na uwindaji haramu ulikuwa umekithiri lakini kwa sababu kuna afadhali kidogo. Anasema lugha inayotumiwa kuwa msitu ni mali ya serikali imekuwa ikiifanya jamii kutoshiriki ipasavyo kupambana na wahalifu na kwamba hiyo ni chanagamoto kubwa kwani msitu ni kama umekosa usimamizi huku baadhi ya wananchi wakishirikiana na wafanyabiashara kuhujumu msitu huo.

Mkazi mwingine wa kijiji cha Michee, Hamisi Killiani anasema wavunaji haramu wamekuwa wakiendesha shughuli zao bila wasiwasi na kwamba kila kukicha unaweza kusikia misumeno yao ikikata mbao. “Kwa kweli ukataji miti uko juu sana na watu wanakata miti bila wasiwasi ingawa hawana vibali halali. Hali hii ikiendelea kwa kweli baada ya muda hakutakuwa na msitu hapa labda jangwa kwa sababu misitu inayosaidia kuvuta mvua kama wanavyosema watalaamu itakuwa imatoweka,” anasema.

Anasema uvunaji wa mkaa nao uko juu, kwani kila kukicha utaona magunia yanatolewa msituni humo tayari kwa kusafirishwa. Rashid Idd ambaye pia ni mkazi mwingine wa kijiji cha Michee anatupa lawama zake kwa serikali ambayo anasema imeshindwa kusimamia mapato ili yanufaishe jamii na kuwadhibiti wavunaji haramu.

Anasema wakazi wengi wa Michee hawana elimu ya kutosha kwa hiyo wamekuwa wanaburuzwa na wafanyabiashara kutokana na kwamba wengi hawajui haki zao wala hasara zitakazoikumba jamii pale msitu utakapotoweka kabisa. Anashauri iundwe kamati ya usimamizi na ulinzi shirikishi huku akitaka serikali ya kijiji isishirikishwe kwani kinachotakiwa ni jamii yenywe kushiriki kikamilifu kulinda msitu.

Mratibu wa mradi wa usimamizi na ulinzi shirikishi wa rasilimali kutoka shirika lisilo la kiserikali la Pemwa, Selemani Namkoma, anawaambia wakazi wa vijiji vinavyozunguka msitu wa Rutamba kwamba kimsingi hizo ni rasilimali zao wananchi wenywe na hivyo wanatakiwa kuzilinda.

Anasema kuwa ni jukumu la wananchi wenyewe kulinda rasilimali hizo kwa makini huku wakiwa wanafuata sheria za serikali zilizowekwa.

Namkoma anasema kuwa ni muhimu viwepo vikundi vya ulinzi na usimamizi shirikishi katika msitu huo ili viwe vinafanya ulinzi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho. Anasema kwa kuwa na kamati za ulinzi shirikishi jamii itakuwa makini na wageni wanaofika kwenye maeneo hayo na kuwatambua na ni vizuri kuepusha migogoro ya ardhi kabla ya kutokea.

foto
Mwandishi: Kennedy Kisula

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi