loader
Msitumikishe watoto kupika wala kuuza pombe

Msitumikishe watoto kupika wala kuuza pombe

 

Kufanya biashara, hata kama ni ya pombe za kienyeji si vibaya, ilimradi viwango vya pombe na masharti ya utengenezaji wake yazingatiwe, ikiwa ni pamoja na kufuata sheria za nchi wakati wa kufanya biashara hiyo.

Baadhi ya watu walio na nafasi nzuri kifedha sasa wamepitia katika kukusanya mitaji kwa kupika na kuuza pombe hizo; kangara, mbege, gongo na nyinginezo. Wanaandaa na kuuza gongo kwa kificho kukwepa kukamatwa. Huo ndio ukweli.

Hata hivyo, hoja yangu si kuzungumzia aina ya pombe zilizonyanyua mitaji ya watu wala kuongelea kama pombe hizo zinaruhusiwa kisheria au la, bali kuwatumikisha watoto wazipike na kuziuza ndio suala la msingi ninalolikemea leo.

Kuna ushahidi wa kutosha kwamba baadhi ya watu, wanawake na wanaume wanawatumia watoto wa ndugu zao, marafiki zao au jirani zao wasio na uwezo wa kifedha, kuwazalishia mali, kupitia biashara ya pombe za kienyeji.

Tena wapo wanaowachukua kutoka katika familia zao kwa maelezo kwamba wanakwenda kuwasomesha au kuwatafutia kazi nzuri za kufanya, lakini, matokeo yake wanaishia kuwakabidhi mafiga ya moto na senti za kununua kuni ili wapike pombe.

Wanaobahatika, hupelekwa shule kweli, lakini malipo wanayoyapata ni kusoma katika mazingira magumu yenye ushawishi wa hatari, kwa kuwa, baadhi yao huuza pombe hizo katika vyumba vyao vya kulala.

Haijalishi wanamuuzia nani, mara nyingi muda wanaotakiwa kuuza pombe hiyo huishia usiku, jambo linalowapa nafasi wanunuzi wasio waaminifu kuwatendea vitendo visivyofaa, hasa ikizingatiwa kuwa watoto hao wanakuwa na hofu ya kuvipinga kutokana na woga wa kuchapwa au kuadhibiwa na wanaowatuma kufanya biashara hiyo ya pombe.

Ninaandika waraka huu nikimaanisha ninachokiandika na wala si ndoto za alinacha. Wapo watoto wanaochukuliwa kutoka katika familia zao na kusafirishwa kwenda kwenye mikoa ya mbali kupika pombe.

Hawachukuliwi wakielezwa kuwa wanakwenda kupika na kuuza pombe, bali wanapelekwa wanakopelekwa ili kuhamia kwenye shule nzuri, jambo ambalo ni ndoto ya mchana.

Wanaowatumikisha kufanya biashara hiyo ya pombe, milele hawawezi kukubali ifanywe na watoto wao kwa kuwa wanafahamu madhara yake. Nina mifano mingi ya watoto waliowahi kutumikishwa kupika pombe baada ya wazazi wao au mmoja wa wazazi wao kufariki.

Wamekuwa wakifanyishwa kazi hiyo na watu wa karibu na familia zao wakiwemo shangazi, mama wadogo na mama wakubwa wanaowachukua kwa gia ya kuwasomesha.

Wenye akili na misimamo, licha ya kuwa katika mazingira magumu, huweza kusoma na kumaliza elimu ya msingi lakini wale wasioweza kujitetea kabisa au wasio na watu wanaofika kuzuia wasiendelee kufanyishwa kazi hiyo, huishia kuwa walevi pia.

Wanaokaa na ndugu wasio na huruma huwekwa mbali na familia zao huku mbinu mbalimbali za uongo zikitumika kuhakikisha kuwa hawatafutwi au kutakiwa warudi walikotoka.

Wapo wanaowadanganya ndugu kuwa watoto wao hawataki kurudi mapema kuwatembelea, wengine husema uongo kuwa wametingwa na masomo hivyo hawawezi kufika wanapohitajika na wengine hudiriki kudanganya kuwa wamepata kazi, ambazo viongozi wao hawatoi ruhusa mpaka baada ya miaka kadhaa.

Haya yanatokea na baadhi ya watoto wanaofanyiwa mambo ya aina hii hawawezi kufungua midomo yao kueleza kinacho wasibu. Upishi wa pombe na uuzaji wa pombe kwa watoto ni makosa na uonevu ambao wazazi, walezi, ndugu, jamaa na marafiki wanapaswa kuukemea.

Kwa sababu wanaozalishiwa mali na fedha na watoto hao ndio wanaofaidika, imekuwa kawaida kuona watoto wazalishaji hao wakiishia kwenye umasikini, ulevi na tabia nyingine mbaya.

Ni kwa sababu wanapedwa ili watumikishwe na katu si kuendelezwa. Kutokana na ukweli huo, naiomba Serikali ianzishe vita dhidi ya wanaowafanyisha watoto biashara hiyo kwa kuwa hawawatakii mema wala kuwajali baadaye.

Swali la kujiuliza, kama upishi wa pombe ni mzuri, mbona watoto wanaowazaa wao hawasogelei mafiga hata kuikoroga?

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) inazidi kuimarika.

foto
Mwandishi: Namsembaeli Mduma

Post your comments