loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Raawu na mikakati ya kupanua fursa za ajira

Naibu Katibu Mkuu wa Raawu Taifa, Winston Makere, anasema chama hicho kimenunua kiwanja eneo la Tuangoma jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujenga chuo hicho ili kuunga mkono jitihada za serikali na jamii ya kimataifa za kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana.

Anasema ujenzi wa chuo hicho ni sehemu ya miradi ya muda mrefu ya chama hicho kinachojumuisha wafanyakazi wa taasisi za Elimu ya Juu, Utafiti, Ufundi Stadi (Veta), Taasisi zinazojihusisha na masuala ya Sayansi na Teknolojia, Taasisi za Ushauri wa Kibiashara, Taasisi za Habari na Taasisi za Kimataifa.

Mradi mwingine wa muda mrefu ni kujenga jengo la ofisi za Raawu, ukumbi wa mikutano ambao utatumika kwa shughuli za chama pia kukodisha ili kuboresha kipato cha chama. Muungano wa Wafanyakazi wa taasisi hizo umesajiliwa kwa mujibu wa Sheria namba 6 na 7 za mwaka 2004 zinazosimamia vyama vya wafanyakazi.

Raawu ni miongoni mwa vyama vya wafanyakazi vilivyotokana na mabadiliko katika historia ya Vyama vya Wafanyakazi nchini. Awali vyama vya wafanyakazi kwa maana ya Chama cha Wafanyakazi Tanzania (Nuta) na Jumuiya ya Wafanyakazi Tanzania (Juwata) ambavyo vilifanyakazi kati ya mwaka 1964 hadi 1991 viliendeshwa chini ya mfumo wa chama kimoja cha siasa.

Baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa siasa vya vyama vingi, mwaka 1992 vyama vya wafanyakazi vililazimika kubadilisha mfumo wa kujiendesha kwa kutenganisha shughuli zake na zile za chama pamoja na kujiendesha kwa uhuru ambapo Wafanyakazi waliruhusiwa kujiunga na vyama vyao kulingana na sehemu au sekta wanazotoka.

Raawu ni miongoni mwa vyama huru 11 vilivyoundwa chini ya Sheria ya Chama cha Wafanyakazi Tanzania (OTTU) namba 20 ya mwaka 1991 na kuthibitishwa rasmi Novemba 1994 baada ya mkutano mkuu kupitisha Katiba na kuchagua viongozi wa kitaifa. Kama ilivyo kwa vyama vingine vinavyokua, mwaka 2000 Raawu iliitisha Mkutano Mkuu wa Tatu ambao ulifanya marekebisho ya Katiba na kuchagua viongozi wapya wa kitaifa.

Aidha mkutano huo ulipitisha maazimio yenye lengo la kuboresha maisha ya wanachama na jamii kwa ujumla kwa kuzingatia dira, lengo na madhumuni ya chama hicho. Dira ya Raawu ni kuwepo kwa jamii yenye watu wenye haki ya kufanya kazi, vyama imara vya wafanyakazi vinavyoendeshwa kidemokrasia na kuhakikisha wafanyakazi wanapatiwa mahitaji yao ya kijamii na kiuchumi.

Ili kufanikisha dira hiyo, Raawu imejiwekea lengo la kuboresha mazingira ya kazi kwa wanachama wake, kushirikisha wanachama katika kufikiwa kwa maamuzi ya chama, kushinikiza juu ya kuwepo kwa sera zitakazoinua na kukuza nafasi za ajira na kuhakikisha kwamba wafanyakazi wanakuwa na maisha bora wakiwa kazini na baada ya kustaafu.

Makere anasema Raawu inashirikiana na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) pamoja na Shirikisho la Kimataifa linalohudumia wafanyakazi wa sekta za huduma kwa Umma (PSI) katika utekelezaji wa malengo yake. Raawu ina malengo mengi ikiwa ni pamoja na kuboresha na kuendeleza hali nzuri ya wanachama katika maisha wakiwa kazini na baada ya kustaafu.

Pia inashirikiana na kujadiliana na waajiri katika kudumisha amani mahala pa kazi. Pia kujadiliana na kuondoa tofauti zinazojitokeza baina ya mwajiri na mwanachama, au mwanachama mmoja na mwingine kwa njia ya makubaliano ya amani kadri inavyowezekana.

Malengo mengine ya Raawu ni kushiriki katika kusaidia utekelezaji wa mikataba ya hali bora za kazi, tuzo, kanuni za nidhamu na kanuni zozote zile ambazo zinatumika nchini. Kushirikiana na kubadilishana ujuzi na vyama vingine vya wafanyakazi nchini pamoja na vile vya kimataifa.

Pia chama hicho kina jukumu la kuwasiliana na Serikali kuhusu utungaji wa sheria sahihi za kazi na kuandaa sera nzuri za kuendeleza maisha ya jamii na pia kulinda maslahi ya wanachama kwa kuhimiza Serikali kuepukana na uandaaji wa sera ambazo ni hatari kwao.

Makere anasema Raawu inajitahidi kutekeleza majukumu yake ili kuhakikisha kuwa mfanyakazi anayejiunga na chama chao anafaidika na chama hicho kwa kupata haki zote stahiki ikiwa ni pamoja na haki zake za ajira kulindwa na Chama, haki ya kutetewa na Chama katika chombo chochote kile kinachotoa haki pale itakapodhihirika kuwa mfanyakazi ameonewa na mwajiri au kiongozi wake ambapo chama hugharimia kesi na mchakato mzima wa kuhakikisha haki inapatikana.

Faida nyingine ya kujiunga na Raawu ni mfanyakazi kuboreshewa maisha yake kazini kupitia mikataba ya hali bora za kazi inayotokana na majadiliano ya pamoja baina ya Chama cha Wafanyakazi na Waajiri au Serikali. Mikataba hiyo humuwezesha mwanachama kupata maslahi bora zaidi mbali na yale yaliyowekwa kisheria.

Mfanyakazi aliyejiunga na Raawu atakuwa na kauli zaidi mahali pake pa kazi kwa kuwa kupitia chama, maoni, malalamiko au ushauri wake utasikika. Mwanachama wa Raawu anapata elimu na maarifa mbalimbali yenye manufaa kwa maisha na ajira yake. Pia atapata fursa ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika chama na kuwakilisha wenzake kwenye vyombo mbalimbali vinavyohusika na masuala ya wafanyakazi.

Atashiriki katika shughuli zote za Chama kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za Chama. Kupitia Raawu maisha ya mfanyakazi yataboreshwa kupitia miradi mbalimbali ya kiuchumi inayoanzishwa na chama sehemu za kazi kwa lengo la kuwapunguzia wafanyakazi makali ya maisha.

Masuala yanayohusiana na nyongeza za mishahara, marupurupu, kuthibitishwa kazini, kupanda madaraja, mifuko ya hifadhi ya jamii na mafao mbalimbali yatafuatiliwa na kufanikishwa na Chama. Mfanyakazi anahakikishiwa mazingira bora ya kazi yanayozingatia kanuni za afya na usalama mahali pa kazi.

Mfanyakazi mwanamke atapata fursa ya kuungana na wanawake wenzake ndani ya chama na hivyo kushiriki katika kuendeleza harakati za ukombozi wa wanawake nchini na nje ya nchi. Tangu kuanzishwa kwake, chama cha Raawu kimefanikiwa kutekeleza malengo yake na kuongeza idadi ya wanachama ambapo hivi hivi sasa kina wanachama zaidi ya 15,000.

Chama hicho kimekamilisha uanzishwaji wa ofisi za Kanda zote na kuzipatia vitendea kazi vya kutosha yakiwemo magari na kompyuta kwa kila Kanda. Mwaka 1995 Raawu ilianza kutetea mishahara ya wafanyakazi kwa kushirikiana na chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) ambapo hoja ilifikishwa Mahakama ya Kazi ya kutaka kima cha chini cha mshahara kiongezeke ili mfanyakazi aweze kumudu kulipia gharama za mahitaji ya msingi.

Mahakama ilikubaliana na hoja hiyo na kuishauri Serikali ilipe kima stahili ambapo Serikali ilitoa ahadi ya kulipa kwa awamu. Raawu iliwatetea wafanyakazi wa taasisi za Serikali walionyimwa haki ya nyongeza ya mishahara mwaka 1998 na utetezi huo uliwezesha wafanyakazi kulipwa haki zao za msingi.

Raawu imetoa mchango mkubwa kwenye marekebisho na utungaji wa sheria mbalimbali za kazi. Pia imeshiriki kuandaa sera ya Vyama vya Wafanyakazi kuhusu Ugonjwa wa Ukimwi. Pia chama hicho kimeshiriki katika kushinikiza ushirikishwaji kwenye uandaaji na utekelezaji wa sera za kuondoa umasikini nchini na ushirikishwaji katika suala zima la ubinafsishaji.

Raawu imeshatoa elimu ya sheria mpya za kazi katika mikoa yote yenye matawi ya Raawu, kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kupigania kupandishwa vyeo na kuthibitishwa na nyongeza ya mishahara ya watumishi wa umma. Makere anafahamisha kuwa Raawu imejipanga vyema kutekeleza mikakati yake ya mipango ya baadaye hasa kuhakikisha kuwa Sheria Mpya za Kazi namba 6 na 7 zinafahamika kwa viongozi na wanachama katika matawi yote.

Pia Raawu ina mpango wa kuendelea kushirikiana TUCTA na vyama vingine vya kimataifa, katika kupigania maslahi na mazingira bora ya kazi. Kuwashawishi wanachama wanawake kujitokeza na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika chama. Chama hicho kinaendeleza mipango yake ya kushirikiana na kujadiliana na waajiri katika kudumisha amani mahala pa kazi.

Kuhamasisha wafanyakazi wote walio kwenye sekta za RAAWU kujiunga na Chama. Kutoa taarifa za mara kwa mara kuhusu Chama kwa wanachama na wasio wanachama. Chama hicho kimeazimia kuimarisha mawasiliano baina yake, wafanyakazi na wanachama na wadau wengine ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuongeza huduma kwa wanachama.

Pia Raawu imejipanga vyema kuhakikisha mabaraza ya wafanyakazi yanaundwa katika sehemu zile ambazo mabaraza hayo hayajaundwa. Kushauriana na Serikali katika kupunguza matabaka ya wafanyakazi katika taasisi za Serikali yanayosababishwa na nyaraka nyingi za mishahara.

foto
Mwandishi: Kaanaeli Kaale

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi