loader
Rais aagiza ripoti za mahudhurio ya shule kila mwezi

Rais aagiza ripoti za mahudhurio ya shule kila mwezi

Ameagiza pia Kamati za Maendeleo ya Jamii za Halmashauri kuhakikisha zinadai ripoti za mahudhurio kutoka kwa wakuu wa shule. Kikwete alitoa maagizo hayo kwenye mkutano wa hadhara aliofanya mjini Namtumbo juzi katika ziara yake mkoani Ruvuma.

Akiwa ziarani mkoani humo, Rais Kikwete alieleza kushitushwa na kiwango kikubwa cha wanafunzi Ruvuma kushindwa kumaliza shule kwa hatua mbalimbali kwa sababu mbali mbali ukiwemo utoro na mimba.

“Hali ya shule za msingi ni mbaya, hali ya sekondari mbaya. Wako wapi watoto hawa wanaostahili kuwa shule? Kwa nini hawako shule? Na wanafanya nini badala ya kuwa shule? Hali hii ni mbaya, mbaya, mbaya, ni aibu kubwa sana hii,” alisema.

Alisisitiza, “Suala hilo nalirudisha kwenu nyie Madiwani. Kuweni makini hawa ni watoto wenu. Nataka kila miezi sita mpatiwe ripoti ya mahudhurio ya wanafunzi katika shule zote za mkoa huu.

“Na kila mwezi, wakuu wa shule zote nchini watoe taarifa za mahudhurio ya wanafunzi kwa maofisa Elimu. Pia Kamati za Maendeleo ya Jamii za Halmashauri nazo lazima zidai ripoti za mahudhurio kutoka kwa wakuu wa shule.”

Aliagiza viongozi kushirikiana na vyombo vya sheria mkoani na wilayani kukabili tatizo hilo. Rais Kikwete aliagiza wanaume waliooa wanafunzi wasakwe, washitakiwe mahakamani wajibu mashitaka ya ubakaji.

Aidha alisema wasichana wanaopaswa kuwa shuleni lakini hawapo, watafutwe warudi kuendelea na masomo.

“Mtoto wa shule hatakiwi kuwa mama wa nyumbani, mtoto wa shule anatakiwa awepo shuleni,” alisema Rais wakati anazungumza na wananchi nje ya soko jipya la kisasa la Mkenda lililopo katika Jimbo la Peramiho wilayani Songea vijijini.

Rais Kikwete anaendelea na ziara ya kikazi ya siku saba mkoani Ruvuma iliyoanza Julai 17 mwaka huu na alikwenda kufungua soko hilo lililopo katika mpaka wa Tanzania na Msumbiji.

Utoro na mimba za wanafunzi ni mambo ambayo yalizungumzwa na Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa kuwa miongoni mwa changamoto katika wilaya yao.

Kwa mujibu wa takwimu, watoto 155 wameshindwa kumaliza masomo yao ya shule za msingi na sekondari katika miezi 18 iliyopita kwa sababu ya ujauzito.

UJENZI  na ukarabati wa Soko la Kariakoo jijini ...

foto
Mwandishi: Basil Msongo

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi