loader
Reli zinazopita barabarani zifanyiwe ukarabati

Reli zinazopita barabarani zifanyiwe ukarabati

Reli hizo zimeharibika kwa kuchimbika kiasi ambacho kimefanya mashimo yanayoleta usumbufu kwa magari yanapopita na kuharibu magurudumu ya magari.

Nimemsikiliza jana ofisa habari wa Shirika la Reli katika mahojiano yake na kituo kimoja cha Redio akijaribu kufafanua baada ya watu kulalamikia kupasuka kwa magurudumu katika reli hizo akisema kwamba wanaopasua magurudumu hao sio madereva bali ni waendesha magari.

Lakini ikumbukwe kwamba barabara hizo zimekaa katika hali hiyo kwa muda mrefu bila Shirika la Reli iwe ile ya Tazara au Reli ya Kati kufanyia marekebisho, wakati huo huo magari yanapita hapo kila kukicha pengine zaidi ya mara mbili au tatu.

Gari hata lipite katika eneo hilo pole pole kiasi gani utalisikia linavyogonga kwa chini kwenye reli, kwa kuwa reli imeharibika kwa kufanya mashimo pembeni yake.

Kuna maeneo mengi ambayo inapita reli imechimbika na kuleta usumbufu mkubwa kwa magari. Kuliko kuanza kuwalalamikia madereva wanapitisha gari zao kwa mwendo wa kasi kwenye gari, kwa kuwa tatizo linaonekana kwa macho, mamlaka zinazohusika na kufanya ukarabati huo zifanye marekebisho kuondoa tatizo hilo kwasababu ni wazi hilo ni tatizo.

Mbali na kuharibu magurudumu ya magari na madari madogo kugongwa na reli kwa chini, reli hasa inayopita karibu na mataa ya kuongozea magari ya Chang’ombe imekuwa ni tatizo kubwa kwa magari yanayotoka Ilala.

Reli hiyo inasababisha msongamano mkubwa sana ingawa askari wa usalama barabarani wanaosimama katika eneo hilo wanajitahidi sana kuvuta magari yanayotoka Ilala.

Kinachotokea magari yanayotoka Ilala yanapita polepole sana kutokana na mashimo yaliyopo kwenye reli, madereva wakihofia kupasua magurudumu yao pamoja na kuharibu magari hasa kwa wenye magari madogo.

Askari anayeongoza magari anapoona inachukua muda mrefu wakati magari yanayopita ni machache wakati pande nyingine yaani magari yanayotoka Chang’ombe na yanayotoka Tazara kwenda mjini hali kadhalika ya mjini kuelekea Tazara yanakuwa yanasubiri tu anaamua kuzuia na kuwaruhusu wengine jambo ambalo linafanya upande wa Ilala kuwa na magari mengi.

Usumbufu huu ni mkubwa sana kwa madereva na hasa abiria wanaokuwa wamesimama kwenye daladala hasa nyakati za mchana jua kali, watu wanajikuta wanasimama muda mrefu sana huku mkishuhudia maeneo mengine magari yanaendelea kwenda lakini inapofika upande wa Ilala zikipita gari mbili tatu zimeshazuiliwa.

Binafsi nimeshawahi kukumbwa na adha hiyo ambapo niliamua kupiga simu Kikosi cha usalama barabarani kuuliza nini tatizo katika barabara ya Kawawa kutokea Ilala kuvuka mataa ya Chang’ombe lakini nilijibiwa kuwa tatizo ni reli inayopita ambayo imechimbika kusababisha magari kwenda polepole sana huku pande zingine zinapoitwa zinaenda haraka.

Sasa ifike mahala tatizo hili lichukuliwe kwa umuhimu wake kwanza kujali mali za watu ambazo mtu anapata gharama ya kununua magurudumu au kutengeneza gari mara kwa mara na kwa wanaopata shida ya kusimama kwenye daladala kwa muda mrefu waondokane na adha hiyo.

Mamlaka zinazohusika zifanye ukarabati wa reli zinazopita kwenye barabara ili ziwe rafiki pia kwa watumiaji wengine wa barabara maana reli zinapoharibu magari ya watu hakuna adhabu yoyote wanayopata lakini inapotokea gari imegonga treni dereva anashitakiwa.

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) inazidi kuimarika.

foto
Mwandishi: Regina Kumba

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi