loader
Serikali yatenga bandari kavu kwa majirani

Serikali yatenga bandari kavu kwa majirani

Hatua hiyo ya kutenga ekari 160 katika eneo la Jitegemee, upande wa barabara ya Mandela inayolenga kuongeza ufanisi wa bandari hiyo kubwa hapa nchini na kuifanya kuwa shindani.

Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe alitangaza hatua hiyo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam katika mkutano wa kuhitimisha ziara ya ujumbe wa maofisa wa serikali na wafanyabiashara kutoka jimbo la Katanga, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Ujumbe huo uliokuwa na lengo la kuimarisha biashara kati ya nchi hizo uliongozwa na Naibu Gavana wa jimbo hilo, Guibert Tshibal na waziri wa Uchukuzi wa jimbo hilo, Laurent Kahozi Sumba.

Waziri Mwakyembe aliwaambia waandishi wa habari kuwa sehemu ya ardhi hiyo itawekwa kwa ajili ya jumuiya ya wafanyabiashara wa Kongo DRC.

“Tunafanya hivi kwa nia ya kuimarisha bandari yetu na pia biashara na majirani zetu,” alisema.

Mizigo ya DRC imekuwa ikiongezeka kwa asilimia takribani 24 kwa mwaka tangu mwaka 2004 ikiongezeka kutoka tani 155,611 hadi tani 1,117,249 mwaka 2013. Nchi ya DRC ni ya pili kwa kupitisha mizigo mingi katika bandari ya Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, mizigo ya DRC inachukua asilimia 25 ya mizigo yote ya nchi jirani inayopita katika bandari hiyo. Pamoja na mambo mengine, ujumbe huo ukiwa nchini ulitembelea eneo hilo pamoja na bandari ya Dar es Salaam.

Waziri Mwakyembe alisema kuwa kamati ya ufundi iliyoundwa na wajumbe wa nchi hizo imekubaliana kushughulikia kero zote zinazokwamisha biashara kati ya nchi hizo. Kwa upande wake, Kahozi Sumba alisifu juhudi za Tanzania kwa hatua inazochukua kuimarisha bandari ya Dar es Salaam.

“Tutazidi maradufu kutumia bandari hii,” alisema. Alisema kuwa bandari hiyo ni njia kuu ya kupitishia mizigo kwa nchi yake hivyo kuimarishwa kwake kutaleta nafuu ya maisha katika jimbo hilo na nchi ya DRC kwa ujumla.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Madeni Kipande alisema kamati hiyo ya ufundi imekubaliana pia kuwa na orodha ya kampuni za wakala wa kupakia na kupakua mizigo katika nchi zote ili kuepuka wizi na matatizo mengine.

Pia ilikubaliwa ianzishwe bandari kavu katika eneo la mpaka wa DRC na Zambia la Kasumbalesa ili kupunguza na kuondokana na tatizo sugu la msongamano wa malori ya mizigo. Kwa upande wake, Tshibal alisifu juhudi zinazofanywa na Dk Mwakyembe na serikali nzima za kuimarisha sekta ya usafiri.

“Dk Mwakyembe ni hazina kwa Tanzania...ni mtu wa vitendo,” alisema Naibu Gavana huyo. Ziara hiyo imekuja kufuatia ile iliyofanywa na wenzao wa Tanzania katika jimbo hilo mapema mwezi Mei mwaka huu ambapo TPA ilifungua ofisi yake ndogo ya mawasiliano katika mji wa Lubumbashi.

WADAU wa Sekta ya Kilimo nchini wameshauriwa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi