loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Sheria za kazi siyo kwa wafanyakazi wa umma pekee

Hivyo ni vyema kujifunza au kujikumbusha sheria na kanuni za kazi Tanzania kama sehemu ya kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani.

Baadhi ya waajiri na waajiriwa wana dhana potofu kuwa Sheria na kanuni za kazi Tanzania zinahusu watumishi wa umma pekee lakini ukweli ni kwamba Sheria za kazi zipo kwa mujibu wa mkataba wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) hivyo zinahusu wafanyakazi wote ikiwa ni pamoja na walioajiriwa katika sekta binafsi.

Saa za Kazi

Saa za kazi ni moja ya mambo makubwa yanayosababisha hali ya kutokuelewana kati ya mwajiri na mfanyakazi hasa katika sekta binafsi.Kipengele kidogo B cha Sheria ya Ajira na Mahusiano ya Kazi ya mwaka 2004 kinaelezea kuhusu saa za kazi. Kwa mujibu wa kipengele hicho, kiwango cha juu kabisa cha saa za kazi ambacho mfanyakazi anaruhusiwa na sheria kufanya kazi ni saa 45 kwa juma ambayo ni sawa na saa tisa (9) kwa siku.

Saa tisa hazijumuishi saa moja inayotolewa kwa ajili ya chakula cha mchana. Mapumziko hutolewa baada ya mfanyakazi kufanyakazi kwa saa tano mfululizo. Mfano mfanyakazi anaingia kazini saa mbili kamili muda wake wa mapumziko utakuwa kati ya 7:00- 8:00 mchana. Kwa wale wanaoanza kazi saa moja na nusu asubuhi watapumzika saa 6:30-7:30.

Wafanyakazi wanaoingia kazini kwa shifti pia wanahitaji muda wa kupumzika baada ya kufanya kazi kwa saa tano mfululizo. Wafanyakazi wengi wanadhani kwamba muda wa saa moja ni kwa ajili ya chakula cha mchana pekee. Hata hivyo, sheria inaeleza kuwa muda huo wa mapumziko haulipwi na ni muda wa mfanyakazi pekee hivyo mfanyakazi anaweza kuutumia kusoma kitabu au magazeti, kufanya manunuzi yake binafsi, kufanya mazoezi au kuzungumza na wageni wake.

Muda wa ziada Muda wa ziada zaidi ya saa 45 kwa juma lazima ulipwe kama saa za ziada. Pia sheria inakataza mfanyakazi kufanya kazi zaidi ya saa 12 kwa siku. Mfanyakazi anaruhusiwa kufanya kazi siku sita za wiki na kupumzika siku ya saba. Mwajiri haruhusiwi kumtaka au kumruhusu mfanyakazi kufanya kazi kwa saa za ziada kama hawana makubaliano kuhusu malipo ya muda wa ziada.

Hata panapokuwa na makubaliano mwajiri na mfanyakazi hawaruhusiwi kuzidisha wastani wa muda wa saa za ziada kama ilivyoelezwa katika sheria za kazi, ambazo ni saa 50 kwa mwezi. Kwa hiyo sheria imeweka kikomo cha saa za ziada ambacho mfanyakazi anaweza kufanya kazi. Kipengele cha 19 (3) kinakataza mfanyakazi kufanya kazi zaidi ya saa za ziada zinazozidi 50 katika mzunguko wa wiki nne.

Kufanyakazi saa 12 bila malipo ya ziada Sheria inatamka kuwa mfanyakazi anapaswa kufanyakazi kwa saa tisa kwa siku.Hata hivyo mfanyakazi anaweza kufanyakazi kwa saa 12 bila malipo ya ziada endapo kutakuwa na mkataba au makubaliano ya maandishi kati ya mfanyakazi na mwajiri kuwa mfanyakazi anapaswa kufanyakazi hadi saa 12 kwa siku bila ya kupata malipo yoyote ya ziada.

Hata hivyo, mfanyakazi anayefanyakazi kwa saa 12 kwa siku hataruhusiwa kufanya kazi zaidi ya siku 5 za wiki, zaidi ya saa 45 kwa wiki na zaidi ya saa 10 za ziada kwa wiki. Makubaliano ya pamoja kati ya mwajiri na chama cha wafanyakazi yanaweza pia kuweka wastani wa saa za ziada na saa za kawaida katika kipindi fulani cha makubaliano.

Kama ilivyo katika makubaliano ya maandishi, makubaliano ya pamoja hayatoruhusu mfanyakazi kufanya kazi zaidi ya wastani wa saa 40 kwa wiki zinazokokotolewa katika kipindi cha makubaliano, saa 10 za ziada kwa wiki na haitokubali kuzidi kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja ili kulinda afya ya mfanyakazi.

Siku za mapumziko

Wafanyakazi wana haki kupata walau siku moja kwa juma , yaani saa 24 mfululizo. Kwa kawaida siku hiyo ya mapumziko ya juma kwa Tanzania hufanyika Jumapili. Kwa wale wanaokwenda kazini Jumapili wanapaswa kupewa siku nyingine ya mapumziko kwa mujibu wa Sehemu ya 24 ya sheria ya kazi na mahusiano kazini ya mwaka 2004.

Wafanyakazi wana haki ya mapumziko ya sikukuu zenye malipo kwa maana ya sikukuu za kiserikali na zile za kidini zilizoainishwa kitaifa. Siku za mapumziko kitaifa hutangazwa na Serikali ambapo Tanzania ina siku 17 za mapumziko kwa mwaka. Siku za mapumziko za kitaifa zinaratibiwa chini ya Sheria ya sikukuu za kitaifa ya mwaka 1966.

Wafanyakazi wote walioajiriwa katika seta binafsi na ya umma wana haki ya kupumzika katika sikukuu hizo kwa mujibu wa sheria. Sheria haitamki wazi ikimtaka mwajiri kutoa mapumziko kwa ajili ya fidia kwa mfanyakazi aliyefanya kazi siku ya mapumziko ya juma au katika sikukuu za kitaifa.

Sheria inasema mwajiri atatakiwa kumlipa mfanyakazi si chini ya moja na nusu ya mshahara wa mfanyakazi kwa muda wa saa za ziada uliyotumika.

Iwapo mfanyakazi atafanya kazi siku za mapumziko ya juma au sikuu za kitaifa atakuwa na haki ya kupata asiimia 200 ya mshahara wake wa siku wa kawaida na hii ni kwa mujibu wa Sehemu ya 24 na 25 ya sheria ya kazi na mahusiano kazini ya 2004 na kwa mujibu wa sehemu ya 7 ya sheria ya mshahara ya 2010.

Hii ina maana kuwa ikitokea saa za ziada zikatumika katika siku za mapumziko ya wiki au katika sikukuu za kitaifa basi mfanyakazi atalipwa kwa kiwango cha mara mbili zaidi ya malipo ya kawaida kwa kila saa aliyofanya kazi. Mfano kama ukigawanya mshahara wa mwezi na kubaini malipo yako ya siku ni Sh 4,000 basi kazi za ziada kwa siku ya Jumapili au sikukuu za kitaifa itakuwa mara mbili, yani Sh 8,000 kwa siku.

Malipo ya ziada kwa kazi za usiku

Kwa mujibu wa Sheria za kazi, usiku ni kipindi kati ya saa 12 jioni na kabla ya saa 12 asubuhi. Mfanyakazi anayefanyakazi muda wa usiku anatastahili kulipwa angalau asilimia 5 ya mshahara wake kwa kila saa anayofanya kazi usiku na kama ni saa za ziada basi asilimia 5 itakokotolewa katika kiwango cha saa za ziada.

Hata hivyo, si kila mfanyakazi anayefanya kazi usiku anastahili ziada ya asilimia tano ya mshahara wake. Malipo hayo ni kwa wale tu ambao kwa kawaida hufanya kazi muda wa mchana lakini kwa sababu za dharura watahitajika kufanya kazi usiku. Kundi la wafanyakazi ambao kazi zao ni za usiku kama vile walinzi, wauguzi wanaofanya kazi kwa zamu, wahudumu wa migahawa na hoteli wafanyao kazi kwa zamu hawastahili asilimia tano ya ziada.

Sheria inakataza baadhi ya makundi ya watu kufanya kazi usiku ikiwa ni pamoja na mfanyakazi aliyethibitishwa kuwa mgonjwa na hivyo kushindwa kufanya kazi za usiku, mfanyakazi mjamzito mwenye miezi miwili kabla ya kujifungua au yeyote aliyethibitishwa na daktari kushindwa kufanya kazi za usiku.

Sheria inakataza Wanawake waliyopo kwenye kipindi cha uzazi kufanya kazi za usiku baada ya kutoa vithibitisho kuwa afya zao haziruhusu kufanya kazi za usiku au afya ya mtoto hairuhusu mama kufanya kazi za usiku.

Likizo ya mwaka na likizo ya uzazi

Kwa mujibu wa Sehemu ya 31 ya sheria ya kazi na mahusiano kazini ya mwaka 2004, kila mfanyakazi anahaki ya kupata siku 28 za likizo ya mwaka yenye malipo baada ya kufanya kazi kwa miezi 12.

Sehemu ya 3 sheria ya kazi na mahusiano ya 2004 inampa mfanyakazi mwanamke haki ya walau wiki kumi na mbili (siku 84) za kilizo ya uzazi na kuendelea kupata mshahara wake. Atapata walau siku 100 za likizo ya uzazi endapo amejifungua watoto zaidi ya mmoja (mapacha). Pia anahaki ya kupata siku nyingine 84 za likizo endapo mtoto wake atafariki dunia kabla ya kutimiza mwaka mmoja.

Mwajiri anatakiwa kutoa likizo ya uzazi bila ya kumkata mshahara mfanyakazi si zaidi ya mara nne kwa kipindi chote atakapokuwa na mfanyakazi huyo. Pia sheria hiyo inaeleza kuwa mama anayenyonyesha ataruhusiwa kupata saa mbili kwa siku ili kunyonyesha mtoto (watoto) wake na muda huo haupaswi kukatwa kwenye mshahara wake.

Sehemu ya 34 ya sheria ya kazi na mahusiano ya 2004, inatoa fursa ya likizo ya uzazi kwa mwanaume/baba ya angalau siku 3 (ndani ya mzunguko wa likizo wa miezi 12) kama itaombwa ndani ya kipindi cha siku 7 tangu kuzaliwa kwa mtoto.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi