loader
Dstv Habarileo  Mobile
Shule kisiwa cha Songosongo zitupiwe macho

Shule kisiwa cha Songosongo zitupiwe macho

Kwa mujibu wa habari hiyo, Shule ya Msingi ya Songosongo ina walimu wanane wote wakiwa wa kiume na ya sekondari ikiwa na walimu wa kiume saba.

Kwa mujibu wa Mtendaji wa Kata ya Songosongo, Shamte Bungara tatizo kubwa ni kukosa usafiri wa uhakika kwa watendaji hao muhimu ambao ndio kiini cha elimu, na hasa ikizingatiwa na ukweli wa kisiwa hicho kwamba ni wa mitumbwi, tena ya kubahatisha na kwamba hali ya hewa ikiwa ni mbaya, uwezekano wa mtu kupoteza maisha kwa kufa maji ni mkubwa mno.

Tunasikitika pamoja nao kwa kuwa tunaamini Serikali imesikia kilio hicho. Ni ukweli ulio wazi kwamba Ofisa Elimu wa Mkoa na Wilaya wanajua tatizo hili kwa undani na wanajua fika madhara ya kuwa na shule inayofundishwa na walimu wa jinsi moja.

Hii ni kwamba kuna wakati wa shughuli za masomo na kazi za kila siku za wanafunzi, upo uhitaji wa msaada wa mwalimu wa kike kwa kuwa shule hizo ni mchanganyiko na yapo baadhi ya maeneo ambayo mwalimu wa kiume hawezi kuyatekeleza linapokuja suala la jinsia.

Usafiri wa mitumbwi ambayo kwa mujibu wa ofisa huyo, ni hatari hasa ikizingatiwa kwamba dhoruba ikipiga mtumbwi huo ukapinduka, ni heri ya mwanaume anayeweza kupambana hadi akafika mwaloni, ingawa na hilo linategemea ujuzi na uwezo wa mhusika, lakini kwa wanawake ni hatari zaidi.

Kwa waliokulia katika maeneo yenye maziwa na mito na wamepata kufanya mazoezi ya kuogelea, kazi hiyo yaweza kuonekana si hatarishi sana ikilinganishwa na mtu ambaye hajawahi kufanya mazoezi ya kuogelea.

Ni kutokana na umuhimu huu, baadhi ya shule hasa zile zinazomilikiwa na watu binafsi kutenga muda wa kuwapeleka watoto kufanya mazoezi ya kuogelea.

Jambo hili laweza kuonekana kama ni la kawaida, lakini nashauri pale inapowezekana, watoto wakafundishwe kuogelea kwani ina faida zake.

Pamoja na kujua kuogelea, hilo haliwezi kuondoa tatizo la kisiwa hicho kwani ni vigumu kuwa na wafanyakazi ambao kila kukicha wanahisi hatari ya kufa maji huku Mwalimu Msaidizi wa Shule hiyo ya Msingi, Haji Njechele akibainisha kwamba hata nyumba za kuishi kwa walimu hao ni chache mno, jambo linaloondoa uwezekano wa walimu wa kike kwenda kuishi huko kama juhudi za makusudi hazitafanyika.

Mwalimu huyo anasema na zile za kupanga, gharama zake ni kubwa, hivyo walimu wa kawaida kwa mshahara wao, ni vigumu kumudu gharama hizo, na njia pekee ni kupanda mitumbwi. Mwalimu huyo akatumia nafasi hiyo kuiomba Serikali kuangalia jinsi ya kusaidia wafanyakazi wa shule zilizo katika kisiwa hicho, nami naungana naye kwani elimu ni ufunguo wa maisha, hivyo ni vema kuliangalia hili kwa makini.

Ni kweli kwamba bajeti za elimu kwa kawaida haziwezi kukidhi matakwa yote ndio maana kuna baadhi ya shule watoto wanakaa chini kwa kukosa madawati, lakini angalau wana walimu wa kutosha. Na zile shule zenye uhaba wa walimu na nyumba, lakini zinafikika!

Kilio kikubwa cha walimu hawa ni kuwajengea nyumba ili waishi huko huko wachape kazi lakini pia wapatiwe vivuko vya uhakika ili wanapokuwa wanakwenda huko, wawe na uhakika wa kufika waendako. Serikali imefanya mambo mengi mazuri kwa Watanzania ikiwamo kusogeza elimu ya sekondari kila kata.

Hili nalo naamini, kwa kuwa ni sikivu italiangalia kwa umakini wake ili kuwaondolea adha wanafunzi na walimu wa kisiwa hiki, kwani watoto wa kike wanahitaji uangalizi wa walimu wa kike hasa pale kunapotokea tatizo ambalo mwalimu wa kiume hawezi kulitatua kirahisi.

TANESCO ni shirika la huduma lakini pia ni ...

foto
Mwandishi: Bantulaki Bilango

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi