loader
Dstv Habarileo  Mobile
Sikukuu ya Idd iambatane na matendo mema

Sikukuu ya Idd iambatane na matendo mema

Kwa muda wa siku 30, wenzetu Waislamu wamekuwa katika mfungo huo, ambao lengo lake ni kutimiza moja ya nguzo tano za Kiislamu. Kwa Mwislamu aliyetimia ni lazima unapofika mwezi wa Ramadhani, ajiweke karibu na Mola wake.

Sherehe maana yake ni furaha, kwamba wenzetu ambao walikuwa katika mfungo huo ni lazima leo washerehekee kuhitimisha mfungo huo. Hivyo, wana haki ya kula na kunywa na kufurahi kwa namna yoyote ile watakayotaka kama familia.

Desturi ya mwanadamu kula na kunywa, ndio kilele cha sherehe, kwamba chakula cha siku hiyo kinakuwa tofauti na chakula tulichokizoea siku zingine. Ni ukweli kwamba katika siku ya leo ndani ya nyumba ya Mwislamu, huwezi kukuta ugali na dagaa.

Lakini, niseme kwamba wakati mwingine, baadhi ya watu wenye nia mbaya wamekuwa wanatumia Sikukuu ya Idd, sio kwa makusudi ya kumtukuza Mungu, bali wanajikuta wanamtukuza shetani.

Wanamtukuza shetani kwa sababu kwa siku 30 ambazo wamejinyima kufanya matendo maovu kama ya uzinzi, ulevi, wizi na vurugu zingine za aina yoyote, lakini wanaitumia sikukuu ya leo kuhitimisha mfungo huo kwa kufanya maasi.

Kwa watu wa namna hiyo, kwao Mungu wanamkumbuka wakati tu wa mfungo wa Ramadhani, lakini baada ya mfungo kumalizika, wanarudia njia zao potofu za kumtukuza shetani na Mungu wanamweka pembeni.

Tabia hii sio nzuri, wala haileti picha nzuri kwa jamii. Kwamba mwanadamu aliyejinyima kwa ajili ya kuweka uhusiano wake na Mungu vizuri kwa siku 30, anaamini kwamba maisha yake yako kwa Mola wake kwa kipindi hicho tu.

Leo hii ndio unakuta nyumba zote za kulala wageni katika miji mbalimbali zimejaa, kisa mwezi mtukufu umemalizika. Yaani leo siku ya Idd, watu ndio wamepanga miadi yao ya kutekeleza maovu yao, kwa hakika hili limekuwa linadhalilisha Mfungo wa Ramadhani.

Vitendo vya wizi, uhalifu wa aina mbalimbali, leo hii ndio unafanyika hadi kulazimika polisi muda wote kuranda mitaani, kuhakikisha kuwa watu wanasherehekea kwa amani badala ya kubughudhiwa na watenda maovu.

Tayari Polisi imeshatoa tamko kuwa itakuwa macho wakati wa sherehe za Idd, kuhakikisha kuwa inawadhibiti watu wote wenye tabia ya kufanya uhalifu katika mikusanyiko ya watu wanadhibitiwa.

Lakini, tunaadhimisha Idd wakati jamii ikiwa kwenye taharuki, kutokana na kuwepo matukio ya milipuko ya mabomu katika baadhi ya miji hapa nchini. Matukio ya namna hii, yanafanya watu washindwe kusherehekea sikukuu kwa raha na amani.

Hivyo naiomba Polisi kwa kushirikiana na wananchi wenyewe, kuhakikisha kuwa kwamba tunakuwa macho na watu wote ambao tutawatilia shaka katika mienendo yao. Ulinzi wa raia ni wetu wenyewe, maana raia tuko wengi na polisi ni wachache.

Pia, naikumbushia polisi kuwa iwe macho na ‘disco toto’, ambazo miaka ya nyuma tumeshuhudia zinachangia kukatisha maisha ya watoto wetu, kutokana tu na tamaa za wamiliki wa baadhi ya kumbi kuwajaza watoto, kwa kile wanachoita ni kuwapa watoto fursa ya kusherehekea Sikukuu ya Idd.

Pamoja na rai yangu kwa Polisi, binafsi nawatakia kila la kheri Waislamu wote, ambao leo wanaadhimisha sikukuu kubwa kwa imani zao. Niwaombe tu kwamba wakati wanasherehekea sikukuu hii, watambue kuwa Waislamu na Wakristo, sote ni ndugu ambao tunapaswa kuheshimiana.

Ni kuheshimiana waumini wa dini zote mbili, kutaendeleza amani tuliyo nayo na kuepuka machafuko ya kidini, kama yanayotokea huko Afrika ya Kati. Kuheshimiana na kupendana ndizo silaha, zitakazotuvusha na kutupa ushindi katika kudumisha amani yetu.

WIKI iliyopita umefanyika uzinduzi wa siku ...

foto
Mwandishi: Shadrack Sagati

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi