loader
Dstv Habarileo  Mobile
Suala la ajira serikalini lisimamiwe na taasisi huru

Suala la ajira serikalini lisimamiwe na taasisi huru

Hatua hiyo ilifanyika baada ya kubainika kuwa baadhi ya watumishi hao, waliajiriwa kwa upendeleo, kwa kuwa walikuwa ndugu, jamaa na watoto wa waliosaili. Kati ya ajira 228 zilizofutwa, ajira 28 ni zile zilizotangazwa na ofisi ya Uhamiaji Zanzibar.

Imeelezwa kuwa tume iliyoundwa kuchunguza tuhuma za kuwepo upendeleo katika nafasi hizo, imebaini kuwa baadhi ya wasailiwa waliopata alama za juu za ufaulu, hawakuitwa kazini na hakukuwa na sababu maalumu zilizotolewa.

Pia, wapo wenye umri mkubwa zaidi ya waliohitajika, waliosailiwa na kuitwa kazini, hivyo ajira hizo zitatangazwa upya na mchakato wa ajira hizo sasa utaendeshwa na wizara.

Imeelezwa kuwa waliobainika kufanya upendeleo huo, watatakiwa kujieleza na kuchukuliwa hatua. Tukio hilo la upendeleo katika ajira kwa idara hiyo ni ushahidi wa upendeleo, unaofanywa na ndugu na jamaa katika ofisi mbalimbali za serikali na idara zake, jambo ambalo linatakiwa kufanyiwa kazi kwa nguvu.

Naipongeza Wizara ya Mambo ya Ndani kwa hatua ilizochukua baada ya habari za upendeleo huo kusikika katika mitandao ya kijamii na kutoziacha, bali kuzifanyia kazi, jambo ambalo litasaidia haki kutendeka kwa waliofaulu usaili.

Ninafahamu kuwa katika kukabiliana na tatizo hili la upendeleo katika ajira, serikali wiki hii imeanza mchakato wa kutunga Sheria ya Mgongano wa Maslahi, ambayo kama ikipita itazuia hali hiyo kujitokeza tena, kwani mtu yeyote mwenye jamaa au ndugu kwenye mchakato, atatakiwa kujiondoa.

Ni wazi kuwa mchakato wa kutunga sheria huchukua muda kidogo, hivyo ni vema katika idara na taasisi kubwa zikiwemo za serikali, suala la ajira lisimamiwe na wizara au taasisi huru, ambayo itatenda haki kwa wasailiwa wote.

Nasema hivyo kwa sababu kama suala hili lisipodhibitiwa, hali hiyo itaendelea kwani suala la ajira nchini linazidi kuwa gumu kila siku, hivyo ni vigumu mtu akipewa nafasi ya kusimamia katika idara au taasisi yake, kuacha kumuingiza ndugu, jamaa na hata rafiki.

Kwa sasa ajira zimekuwa ngumu huku idadi kubwa ya vijana wanamaliza vyuo na kuishia mitaani, hivyo inapotokea nafasi kama hiyo, bila kuwepo usimamizi madhubuti, ni vigumu kuepuka hali hii.

Hivyo kwa pamoja tukubaliane kuwa hili lililotokea katika Idara ya Uhamiaji, liwe fundisho kwa watendaji wakubwa wa wizara husika, kuhakikisha Mtanzania yeyote anapata haki ya kufanya kazi katika idara ya serikali, kama anatimiza vigezo, bila hata kuwa na mtu yeyote anayemjua.

Ninaamini kuwa kila mmoja, kwa nafasi yake, lazima awe na moyo wa kutenda haki, hususan katika suala hili la ajira. Iwapo wasaili watagundulika kutotenda haki, wachukuliwe hatua kali kwa mujibu wa sheria ili liwe fundisho kwa wengine.

Nasisitiza wapewe adhabu kali, ikiwemo hata kufukuzwa kazi, ili kuwafanya wanaofanya vitendo hivyo, kuogopa, kwani kama watapewa adhabu ndogo ya kujieleza tu, basi hali hiyo itatoa mwanya kwa wengine kufanya hivyo, ikiwemo hata kushirikiana na watendaji wa wizara husika, watakaosimamia mchakato huo.

TANESCO ni shirika la huduma lakini pia ni ...

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi