loader
Swissport yapata ongezeko la faida

Swissport yapata ongezeko la faida

Ongezeko hilo la faida katika kampuni limewezesha pato la kila hisa kuongezeka mpaka Sh 208.22 ukilinganisha na Sh 186.75 iliyoripotiwa mwaka 2012, ikiwapatia wanahisa ongezeko la asilimia 11.5 la hisa zao.

Hayo yalielezwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Swissport Tanzania Plc, Gaudence Temu katika taarifa yake kwa wanahisa wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka uliofanyika juzi jijini Dar es Salaam.

Temu alisema ukuaji wa huduma za Fastjet, mwaka mzima wa uendeshwaji wa Shirika la Ndege la Kenya, uanzishwaji wa safari za ndege kubwa kama Turkish Airlines na Qatar Airways katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), ongezeko la idadi za safari na mabadiliko makubwa yaliyofanywa na Emirates, KLM, Ethiopian Airways, Qatar Airways, South African Airways, Egypt Air na Rwanda Air yamesaidia Kampuni ya Swissport kufanya vizuri.

“Huu ulikuwa mwaka wa mafanikio ambapo tumeweza kutanua shughuli zetu katika viwanja vya ndege vya Mtwara na Songwe. Tumewekeza kikamilifu katika vituo hivi vipya na tumeweza kufanikiwa. Vituo hivi viwili vina umuhimu mkubwa kutokana na kuwa katika maeneo mazuri kijiografia,” alisema Temu.

Alisema kwa mwaka 2013 kampuni iliweza kusimamia jumla ya safari 13,098 za ndege ikiwa ni ongezeko la asilimia 13 ukilinganisha na safari 11,590 zilizosimamiwa na kampuni hiyo kwa mwaka 2012.

Abiria waliohudumiwa na kampuni hiyo kwa mwaka 2013 walikuwa 905,347 ikilinganishwa na abiria 657,072 waliohudumiwa kwa mwaka 2012, ambalo ni ongezeko la asilimia 38 ikilinganishwa na mwaka 2012.

Mizigo iliyosimamiwa kwa mwaka 2013 ilikuwa ni tani 25,126 ikiwa ni ongezeko la asilimia 11 ikilinganishwa na tani 28,354 zilizosimamiwa mwaka 2012.

Ofisa Mtendaji Mkuu huyo aliongeza kuwa pato la jumla la kiuendeshaji la kampuni kwa mwaka huo limeongezeka kwa asilimia 19 mpaka Sh milioni 36,115 ikilinganishwa na Sh milioni 30,353 zilizopatikana katika mwaka 2012.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Swissport, Juan José Andrés Alvez alibainisha kwa wanahisa kuwa mwishoni mwa mwaka wa fedha 2013, kampuni ilianza ujenzi wa ghala la mizigo la kisasa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), ambao utagharimu zaidi ya Dola za kimarekani milioni 6.3.

UKOSEFU wa elimu ya biashara, uthubutu na ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi