loader
Dstv Habarileo  Mobile
Taarifa za ebola zizingatie weledi

Taarifa za ebola zizingatie weledi

Ugonjwa huo kwa sasa unaleta hofu kubwa kwa nchi za Afrika, hususani zile zilizo jirani na nchi hizo za Afrika Magharibi na zile zinazofanya biashara au kuwa na uhusiano wa moja kwa moja kwa namna moja au nyingine na nchi hizo.

Tayari nchi mbalimbali za Afrika, zikiwemo za Afrika Mashariki zimeshatangaza tahadhari na kubainisha mipango kabambe ya kupambana na kudhibiti ugonjwa huo, ambao Shirika la Afya Duniani (WHO) limeutangaza kama janga la kimataifa.

Kwa Tanzania, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid pamoja na Naibu wake, Stephen Kebwe, wamebainisha wazi hatua thabiti ambazo hadi sasa Serikali imezichukua, kama tahadhari ya namna ya kukabiliana na ugonjwa huo, endapo utaingia nchini kwa bahati mbaya.

Hatua hizo ni pamoja na kununua mashine maalumu za kupima wageni wote wanaoingia nchini, ambazo zimewekwa kwenye Uwanja wa Ndege vya Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Aidha, mashine hizo pamoja na wataalamu wa afya waliopatiwa mafunzo, wamesambazwa katika maeneo yote ya mipaka ya nchi.

Kila mkoa umetakiwa kutenga kitengo maalumu kitakachoshughulikia mtu au watu wanaoshukiwa kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo. Ukweli ni kwamba pamoja na uhaba wa fedha na ufinyu wa watoa huduma nchini, Serikali imejitahidi kwa hali na mali kuhakikisha inakabiliana na tatizo hilo.

Jambo la msingi kwa sasa ni ushirikiano wa Serikali na wananchi wote kwa ujumla. Hakuna asiyefahamu kuwa kwa sasa kutokana na utandawazi kuna mitandao mingi ya kijamii, inayotoa habari ambazo zinawafikia wananchi punde tu mara baada ya tukio kutokea.

Jambo la msingi katika suala zima la ugonjwa huo ni vyema habari zake kabla ya kuripotiwa, zizingatie weledi kwa maana ya kuwa za uhakika, badala ya kutolewa bila uchunguzi wa kina kufanyika na uhakika wa tukio hilo kuhakikishwa.

Taarifa zozote za uzushi, zinatolewa kuhusu ugonjwa huu pamoja na kuwajaza hofu watanzania, lakini pia zinaiweka pabaya nchi kwa maana ya uchumi, kwa kuwa kwa sasa dunia yote macho na hofu yake kubwa ipo kwa nchi za Afrika Magharibi, ambazo kwa sasa ni kama zimetengwa kiuchumi.

Jambo la msingi ni kusaidiana kueneza elimu juu ya namna ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo, ambayo yanatokana na kugusana na mgonjwa mwenye maambukizi, mate, damu, mkojo, machozi, kamasi, majimaji mengine ya mwili, ikiwa ni pamoja na jasho.

Pia, unaweza kupata ebola endapo utamgusa mtu aliyekufa kwa ugonjwa huo, kugusana na wanyama jamii ya nyani, kuchomwa na sindano au vifaa ambavyo havikutakaswa, kujamiiana, kugusa taka ngumu au maji taka yaliyotokana na kumhudumia mgonjwa wa ebola.

Dalili za ugonjwa huo ni homa kali inayoambatana na kutokwa damu katika matundu yote ya mwili kama pua, njia ya haja kubwa na dogo, mdomoni, masikioni, machoni, kutapika damu, kuharisha damu na fizi kuvuja damu.

Chanzo kamili cha virusi vya ugonjwa huo hakijulikani. Wataalamu wameshabainisha kuwa katika orodha ya watu 10 waliopata kirusi cha ebola, wastani kati ya watano au tisa hufa. Tujihadhari wote kwa kukimbilia hospitali, tuonapo dalili hizo ili kuokoa wengine.

TANESCO ni shirika la huduma lakini pia ni ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi