loader
Dstv Habarileo  Mobile
Taasisi, idara ziache utaratibu mbovu wa kuendesha usaili

Taasisi, idara ziache utaratibu mbovu wa kuendesha usaili

Siku chache zilizopita, hali kama hiyo ilijitokeza katika usaili wa nafasi za kazi katika Idara ya Uhamiaji, ambayo ilifanya usaili wa watu 10,000 katika Uwanja wa Taifa, wakati nafasi zilizokuwa zinatakiwa kujazwa ni 70 tu.

Matokeo yake watu wengi walilalamikia usaili huo. Wakati tukishangaa ya Uhamiaji, Alhamisi Shirika la Viwango Tanzania(TBS) nalo lilianza kufanya usaili wa watu 6,740 wakati nafasi zilizokuwa wazi ni 47 tu, ambazo zilitangazwa Aprili mwaka huu.

Usaili wa TBS ulifanyika kwa siku mbili katika Ukumbi wa Yombo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo wasailiwa walikusanyika wakiwa na vyeti vyao halisi na walijisajili wakisubiri kuingia katika chumba cha kufanyia usaili, ambao ulisimamiwa na taasisi mbalimbali za Serikali.

Hoja yangu hapa ni nini? Ni huu utaratibu mbovu wa taasisi na idara za Serikali, kuita watu ‘kibao’ kwenye usaili, wakati nafasi zinazotakiwa kujazwa ni chache. Kwa mfano, katika usaili huo wa TBS kwenye nafasi ya Mhasibu Msaidizi, wanaohitajika ni watu watatu, lakini walioitwa kwenye usaili ni 700.

Sasa kwa nini kusumbua watu wote hao, kwa ajili ya nafasi tatu tu? Mfano mwingine ni nafasi ya Ofisa Rasilimali Watu, wanaotakiwa ni watatu, lakini walioitwa katika usaili ni 800.

Jamani, kwa nini kusumbua watu wote hao, wakati mnafahamu fika wanaohitajika ni watu watatu? Kwanza ni kuwapotezea watu muda na kuwafanya watoto tu.

Ikumbukwe kuna vijana na watu wengi, wamemaliza kusoma wanatafuta ajira kwa udi na uvumba, sasa anaposikia nafasi kama hizi, anajaribu, na bila huruma wahusika wanakubali tu maombi ya kila mtu, wakati nafasi zinazotakiwa ni chache.

Hii si haki hata kidogo! Lazima, wahusika watumie ubinadamu na utu, kwa kutangaza sifa wanazotaka, badala ya kutangaza nafasi za ujumla na matokeo yake wanajitokeza watu wengi bila sababu na kuwasumbua tu siku nzima, wakati mwisho wa siku hapati nafasi hiyo ya kazi.

Hali hii ya kusumbua watu, kwa kuwaita wengi katika usaili, ndio inakatisha tamaa watu wengine, kutafuta kazi na kuamua kujibweteka tu, kwa sababu sio wote wenye akili za kujiajiri ama kutafuta ajira mbadala binafsi, kwa kuwa wanajiona wana vyeti na wana haki ya kufanya kazi ofisini.

Kwa hili la TBS, inanipa wasiwasi huenda yanaweza kutokea kama yaliyotokea kwa Idara ya Uhamiaji, kwa sababu nafasi anatakiwa kujaza mtu mmoja au watatu, mtachambuaje kuchagua anayestahili bila kuwa na upendeleo?

Haya sio tu kwa TBS na Idara ya Uhamiaji, yanatokea katika taasisi na idara nyingi tu, wanaitwa watu wengi kufanya usaili, wakati wahusika tayari wana watu wao wanaotaka kuwaingiza kujaza nafasi hizo, kama ni hivyo kwa nini kuwapotezea watu muda bila sababu.

Ninachoamini kabla ya usaili, wahusika hupokea maombi, ni kwa nini msichambue mfano kama nafasi inahitajika watu watatu na wameomba wengi, chambueni tazameni wale wenye sifa mnazotaka, angalau hata watano waiteni, wafanyieni usaili mpate watatu mnaoona ndio bora zaidi, lakini sio nafasi za watu watatu, mnasaili watu 800, inakuja kweli?

Hata kama taasisi husika, itaamuru usaili kusimamiwa na watu wengine ili kuepuka upendeleo, bado tatizo lipo la kuwasumbua watu wengi kutoka mbali, kuja kufanya usaili kwa nafasi moja au mbili. Hili ni suala la ustaarabu na kukaa kwenye nafasi ya mtu yule, unayemsumbua bila sababu.

Wito wangu kwa Wizara ya Kazi na Ajira, Wizara ya Utumishi, taasisi na idara za Serikali, kujipanga upya wakati wa kuajiri na kuwafanyia usaili watu na kutafuta njia bora zaidi ya kuangalia mazingira na njia bora zaidi ya usaili.

Ni vizuri kuachana na utaratibu huu mbovu, ambao ni kero na usumbufu kwa wananchi wanaotafuta ajira.

WIKI iliyopita umefanyika uzinduzi wa siku ...

foto
Mwandishi: Angela Semaya

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi