loader
Dstv Habarileo  Mobile
TFDA ipambane kikamilifu na vipodozi visivyofaa

TFDA ipambane kikamilifu na vipodozi visivyofaa

Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) ndio yenye wajibu wa kutoa elimu kuhusu chakula na dawa, pamoja na matumizi sahihi ya vyakula na dawa, vikiwemo vipodozi kwa faida za afya zetu.

Taarifa zilizowahi kutolewa kuhusu madhara yatokanayo na matumzi ya vipodozi visivyofaa vyenye viambata vya zebaki ni athari za kiafya, hasa kwa wajawazito ambapo kuna uwezekano wa kujifungua mtoto mwenye matatizo ya kiafya pia.

Viambata vingine vinatajwa kuwa ni zirconium na vinyl chloride, vinavyosababisha saratani ya ngozi na mapafu baada ya kutumia vipodozi vyenye kemikali hizo.

Takwimu zilizowahi kutolewa mwaka huu na Ofisa Uhusiano wa mamlaka hiyo, Gaudensia Simwanza zilieleza kuwa kwa kipindi cha mwaka 2012/13, TFDA imeteketeza jumla ya tani 34 za vipodozi visivyofaa, vyenye thamani ya Sh milioni 188.

Katika maelezo yake, Simwanza alisema hatua ya kukamata shehena hiyo ni matokeo ya mfumo thabiti wa udhibiti wa vipodozi, ambao unatumia njia mbalimbali, ikiwa ni pamoja na usajili wa vipodozi na ukaguzi wa majengo ya kuuzia bidhaa hizo.

Pia, mafanikio hayo yanatokana na ufuatiliaji wa vipodozi vilivyoko sokoni, kwa lengo la kujiridhisha, kama vina ubora na usalama unaotakiwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.

Hata hivyo, ipo mikoa kadhaa nchini, ambako bidhaa mbalimbali ambazo si nzuri kwa ubora na usalama wa afya ya binadamu, zimekamatwa.

Kwa mfano, mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu Jeshi la Polisi mkoani Kagera, lilikamata maboksi 568, yakiwa na vipodozi haramu na dawa za binadamu, ambazo si salama kwa matumizi.

Vipodozi hivyo vilikamatwa katika tarafa ya Bugabo wilayani Bukoba, vikiwa ndani ya mtumbwi. Vilikuwa vikiingizwa nchini kutoka nchi jirani ya Uganda.

Nilichojifunza hapa ni kuwa mamlaka hii, bado inakabiliwa na changamoto kadhaa, zinazokwamisha utendaji wao wenye lengo la kutokomeza kadhia hii.

Lakini, wafanyabiashara nao hutumia changamoto hizo, kama mianya ya kuingiza vipodozi visivyoruhusiwa nchini. Mwanya inayoonekana kutumiwa na wafanyabiashara wasio waaminifu, ni kama ule unaolalamikiwa na wakazi wa kata ya Bondeni na Mawenzi katika Manispaa ya Moshi.

Wakazi hao wanadai kuwa wafanyabiashara katika eneo hilo, wamebuni njia mpya ya uuzaji wa bidhaa hizo. Imeelezwa kuwa wanachokifanya kwa sasa ni kuuza vipodozi hivyo kwenye mikokoteni, tofauti na awali ambapo vilikuwa vikiuzwa ndani ya maduka.

Hii inaweza kuwa njia mojawapo ya kukwepa ukaguzi wa kushtukiza, unaofanywa na mamlaka hiyo ndani ya maduka makubwa, kama ambavyo wafanyabiashara wengine, hukamatwa kwa urahisi kwa njia hiyo.

Malalamiko ya wakazi hao, yanaweza kuwakilisha sehemu kubwa ya wakazi wa maeneo mengine nchini, ambao nao wanashuhudia njia mbadala, zinazofanywa na wafanyabiashara ambao si waaminifu.

Hivyo ili mamlaka hii iweze kupambana kikamilifu na tatizo hili, ni heri itambue ujanja au mbinu zinazofanywa na wafanyabiashara wa makundi mawili tofauti. Kundi la kwanza ni wafanyabiashara wanaoingiza nchini vipodozi kwa njia zisizo halali.

La pili ni wafanyabiashara, wanaomfikia mteja wa mwisho ambaye ndio mtumiaji. Baada ya kuzitambua mbinu zao, ndipo wachukue hatua zinazostahili, zitakazokomesha ujanja huo.

Hatua hiyo ya utambuzi, iende sambamba na mabadiliko kulingana na wakati, yaani kadri mbinu mpya zinavyoibuka ndivyo mamlaka nayo inavyobadilika.

WIKI iliyopita umefanyika uzinduzi wa siku ...

foto
Mwandishi: Kiyao Hoza

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi