loader
TLTC yashinda tuzo ya kampuni bora ya mwaka

TLTC yashinda tuzo ya kampuni bora ya mwaka

TLTC ilinyakua kikombe cha kampuni bora kwa mkoa wa Morogoro kwa mwaka 2014, kutokana na mchango wake katika maendeleo ya mkoa na watu wa Morogoro.

Akizungumza katika hafla ya zawadi hizo, iliyoandaliwa na Kituo cha Maendeleo ya Utamaduni Morogoro, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera alisema kampuni hiyo ilikuwa na kila sababu ya kushinda tuzo hiyo.

“TLTC imeshinda kupitia mchujo uliokuwa wa kiushindani. Kushinda kwao, kunaonesha namna ambavyo wamekuwa wakiyagusa na kuyaboresha maisha ya wakazi wa Morogoro,” alieleza.

Bendera alisema uwepo wa kampuni hiyo katika mkoa wa Morogoro, umekuwa na mchango mkubwa katika kukuza maendeleo ya kiuchumi ya mkoa, kupitia mikakati yao ya kimaendeleo ambayo imekuwa ikisaidia sekta za elimu, afya na maji.

Mkuu huyo wa mkoa alisema Morogoro inajisikia fahari kuwa nyumbani kwa kampuni kubwa ya tumbaku, inayofanya kazi katika mikoa tisa na hivyo kusaidia kutoa ajira kwa wananchi wengi pamoja na kampuni yake tanzu, inayoshughulika na kusindika zao la tumbaku (TTPL) yenye kiwanda mkoani Morogoro pia.

“TLTC inastahili kushinda kikombe hiki, kama kampuni bora hapa Morogoro. Imeajiri ndugu zetu wengi, tumeshuhudia ikitoa misaada mbalimbali kwa wana Morogoro, ikiwa ni pamoja na mashine ya ultra sound kwa hospitali kuu ya mkoa wetu yenye thamani ya Sh milioni 65,” alisema wakati anakabidhi kikombe hicho.

Alisema mchango yao mbalimbali na mashine hiyo, imewawezesha wagonjwa kupata huduma ya ultra sound katika hospitali yao, hivyo kuondoa adha za kupewa rufaa za kwenda hospitali za mbali.

“Pamoja na michango mingi kwenye sekta ya elimu na maji kwa wakazi wa Morogoro, kampuni hii inaendelea kuwa mdau wetu mkubwa wa maendeleo kwa mkoa wetu,” alieleza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sheria na Uhusiano wa kampuni hiyo, Richard Sinamtwa alisema kampuni yake imechangia Sh milioni 200 katika miradi mbali mbali ya maendeleo ya jamii kwa mwaka 2013/2014.

Alisema misaada iliyotolewa ililenga maeneo ya afya, elimu na maji ambayo ndiyo kipaumbele chao.

“Tunafurahi kuwa sehemu ya jamii ya Morogoro na tunajivunia kutoa mchango wetu kwa ajili ya maendeleo ya mkoa wetu kwa ajili ya kuboresha maisha ya watu wetu. Kati ya shilingi milioni 200 zilizotengwa Sh mil 130 zimeshakabidhiwa tayari kwa wahusika na kiasi kilichobaki kitatolewa hivi karibuni,” alifafanua.

Mkurugenzi wa Kituo cha Maendeleo Morogoro, Anthony Muhando alisema kampuni ya TLTC imeibuka mshindi kupitia ushikishwaji wa wananchi wa Morogoro kupitia dodoso, mjumbe mfupi wa simu(SMS) simu kupitia redio na barua pepe.

“Ni kupitia njia hizi za kuyatambua makampuni gani bora kwa hapa Morogoro ndipo wananchi waliamua kuichangia kampuni ya TLTC kutokana na mchango wake kwa maendeleo yao,” alieleza Hafla hiyo ilikuwa na aina nyingine za tuzo, zikiwemo ya uongozi bora, ambayo alishinda Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na mbunge wa Morogoro Mjini, Aziz Abood.

Katika tuzo hizo pia waandishi wa habari Juma Mtanda na Idda Mushi, walishinda tuzo za kuutangaza mkoa huo. Benki ya CRDB ilishinda tuzo ya taasisi bora ya fedha kwa mkoa huo, ikiwa na matawi zaidi ya 10 yanayowahudumia wakazi wa Morogoro na wilaya zake.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Morogoro

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi