loader
Tujenge tabia ya kutoa takwimu sahihi

Tujenge tabia ya kutoa takwimu sahihi

Tunasema zinasikitisha kwa kuwa takwimu sahihi ndizo zinazoweza kutoa picha kamili ya Bajeti Kuu ya Serikali, mwongozo kwa watunga sera, dira ya maendeleo na uwajibikaji wa kila sekta.

Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni mjini Morogoro, Meneja wa Takwimu za Pato la Taifa wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Daniel Masolwa alisema kumekuwa na tatizo la kutopata takwimu sahihi katika mchanganuo wa faida.

Kulingana na maelezo yake, ni vigumu NBS kupata takwimu za wafanyabiashara hasa wa madini na pia katika ngazi ya familia, wanaofanyabiashara rasmi na zisizo rasmi, kwa kuwa huficha kiasi wanachopata.

Ni kutokana na kufichwa kwa takwimu hizo muhimu zilizo sahihi, Masolwa amesema imekuwa ikisababisha kutokuwa na takwimu zinazoelezea uhalisia wa Pato la Taifa kwa kuwa pato hilo, hutegemea pato la mwisho la kaya, usahihi wa faida wanazopata wawekezaji na wafanyabiashara ndogo na kubwa nchini.

Kutokana na maelezo ya Masolwa, maendeleo hayawezi kuja kwa kubuni. Sera za nchi haziwezi kuendana na hali halisi kwa kuwa hata tafiti zozote, ambazo zinahitajika katika kupanga maendeleo ya nchi huanzia kwenye takwimu.

Hata hivyo, kulaumu tu bila kutoa suluhisho hakuwezi kutatua changamoto hii. Nadhani jibu pekee linalowakabili Watanzania, ambao wamewaambukiza na hata wawekezaji kutoka nje ya nchi ni kuendelea kutoa elimu ili waone umuhimu wake.

Tunaweza kusema kuwa eneo hilo, hakuna elimu ya kutosha, ndio maana Watanzania wengi hawataki kuwa wawazi katika pato lao, kwa kuwa wanataka kukwepa kodi.

Ukienda kwa muuza duka yeyote, mfanyabiashara ya mitumba au mama ntilie, utaona kuwa hawako tayari kusema kwa siku wanakusanya kiasi gani. Tabia hii imejengeka sana.

Na mbaya zaidi inaanzia kwa mtu binafsi, kundi hadi kampuni kubwa. Nenda kwa kampuni za wachimba madini ya ndani na nje katika machimbo. Hawatoi takwimu sahihi kuhusu makusanyo licha ya baadhi ya maeneo kuwa na ofisi za Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA).

Yapo mambo mengi yanayosababisha watu kuhofia, kutoa takwimu na mengine yamesababishwa na watendaji wenyewe kukumbatia rushwa, kutaka njia za mkato na kuendekeza udugu katika masuala nyeti kama hayo.

Kutokana na watu kuhofia kutoa takwimu ili zisije kuwa kigezo cha kulipa kodi kubwa, ndio maana hata mashine za malipo kwa njia ya elektroniki zimekuwa zikikimbiwa na wanyabiashara, kwa kuwa wanataka kukwepa kodi na kuwepo kwa mashine hizo kutawaumbua wengi, kwani takwimu zitakuwa ziko sahihi. Watu wanataka kuishi kwa ujanja ujanja.

Na pengine tabia hii imekuwa kubwa, kwa kuwa hata makusanyo ya fedha, yamekuwa hayaoneshi kulenga mlipa kodi moja kwa moja, hivyo ni vema kuliona hili ili watu waelimishwe kulipa kodi na ikikusanywa, waione ikitumika kwa faida yao.

Nchi zilizoendelea kulipa kodi ni sifa. Hapa kwetu mkwepa kodi ndiye shujaa. Haya ni mambo ambayo ni lazima yabadilike kwa wadau, kupewa elimu ya kutosha ili wajifunze kutoa takwimu sahihi na takwimu hizo ziwezeshe Serikali kupanga mipango ya bajeti, sera na huduma za maendeleo kwa usahihi.

Masolwa katika mkutano huo na waandishi wa habari, aliwataka wananchi kila wanaponunua bidhaa, kudai stakabadhi, ikiwa ni hatua ya kuwezesha Taifa kupata faida na takwimu sahihi kwa maendeleo ya nchi.

Akifafanua kuhusu hali halisi ya ongezeko la Pato la Taifa na umasikini kwa mwananchi wa kawaida, alisema Pato la Taifa ni mwongozo na hali ya shughuli za kiuchumi na haliwakilishi ustawi wa mtu pekee.

Pia, akasisitiza kwamba ukuaji wa uchumi, unaweza kutokana na sekta chache, ambazo zimeshikwa na wawekezaji wakubwa au wa kati, huku inayogusa watu wa kawaida ikawa haikui.

Hata hivyo, katika suala la elimu, alisema ofisi yao inaendelea kutoa elimu kwa umma kwa kushirikiana na wadau wengine, kuhusu umuhimu wa taarifa sahihi kwa maendeleo ya taifa zima.

Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk Albina Chuwa, hakusita katika mkutano huo, kuwataka waandishi wa habari kuelimisha umma, kuhusu umuhimu wa kutoa taarifa sahihi za kitakwimu, kuwezesha serikali kujipanga zaidi kupambana na umasikini.

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) inazidi kuimarika.

foto
Mwandishi: Bantulaki Bilango

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi