loader
Turekebishe kasoro zilizojitokeza ili tuimarishe Muungano wetu

Turekebishe kasoro zilizojitokeza ili tuimarishe Muungano wetu

Kwa nyakati mbalimbali, waasisi hao walituasa kuwa kuunda Serikali ya Tanganyika, kutasababisha kuvunjika kwa Muungano wetu na pia kunaweza kuchangia kutengeneza dhambi kubwa ya ubaguzi dhidi ya wengine.

Kwamba aina hii ya dhambi ukishaifanya, inakuwa vigumu kuachana nayo, kwani kundi fulani la watu kutoka sehemu fulani, watajiona ni bora kuliko wenzao wanaotoka sehemu nyingine.

Wataanza kujitambulisha kwa maeneo wanayotoka, mfano Kanda ya Ziwa, Kanda ya Pwani, Unguja na Pemba. Kama tunafahamu ni kwa jinsi gani dhambi hii ya ubaguzi itatutafuna, hivi Watanzania wa leo tunataka nini hata baadhi ya wanasiasa wachache huku na huko, kutaka kufumua muundo wa sasa wa Muungano wetu?

Kama leo, kuna watu wanajiona wao ni Watanganyika, kwa nini baadaye wasijione wao ni wa kanda fulani, au wale Waunguja wasijione bora kuliko Wapemba na hata kutaka kila mmoja abaki na kisiwa chake?

Mwalimu Nyerere ambaye ni sawa na nabii, kutokana na uwezo wake wa kuona mbali, alituasa sana juu ya hili, akisema ndani ya Muungano hakuna Zanzibar wala Tanganyika, bali nje ya Muungano kuna wale Wapemba na hawa Waunguja, nje ya Muungano hakuna Tanganyika, kuna hawa Wabara na hao ni wa Pwani. Kwa mantiki hii, tusijidanganye kuwa tukiunda Tanganyika tutabaki salama.

Kamwe hatutabaki salama na huo utakuwa mwanzo wa kuvunjika kwa Muungano huu, unaotimiza umri wa miaka 50 sasa. Na ukivunjika, utakuwa ni wakati wa kila kanda na hata mkoa, kutaka kujitambua na kuunda serikali yake na kujiamulia mambo yake, ndugu zangu hapo tutakuwa salama?

Tuangalie mifano ya mataifa makubwa, yaliyojaribu kuunda serikali zao mfano Russia, walipounda serikali yao ndani ya Shirikisho la Jamhuri za Kisovieti za Urusi (USSR), huo ndio ulikuwa mwisho wa Taifa hilo kubwa duniani.

Zipo nchi zina Muungano kama wetu. Kwa mfano, Uingereza wana Serikali ya Muungano wa nchi nne na serikali nne na sio tano, yaani England, Uskochi, Wales na Ireland ya Kaskazini.

Kila mmoja ina serikali yake kwa sababu ni nchi ndogo katika Muungano wa Uingereza. Lakini, England kwa sababu ni nchi kubwa katika Muungano huo, madaraka yake yote yako kwenye Serikali ya Muungano.

Sasa hapa kwetu, tatizo ni nini ? Kama tatizo ni Zanzibar kuwa na bendera, wimbo na Rais, mbona hata timu za soka, zina marais, nyimbo zao na bendera zao? Mbona katika muungano kama wa Marekani, kila jimbo lina bendera, wimbo na Gavana wake? Je, hiyo inaondoa Utaifa wao kama Marekani?

Zanzibar ni nchi ndogo katika Muungano, hivyo ni muhimu kupata upendeleo zaidi katika Muungano ili isionekane imemezwa na nchi kubwa Tanzania Bara.

Mifano iko mingi, kama Uingereza, China, Hong Kong na kadhalika. Ndugu zangu ukiachana na jinsi utengano unavyoweza kutafuna, kwa upande mwingine tufikirie pia gharama za uendeshaji wa serikali ya tatu na taasisi zake.

Je, tutaweza kweli kuondoa umasikini, ujinga na maradhi kwa kujiongezea mzigo wa kuhudumia taasisi za serikali? Katika historia ya dunia, hakuna taifa lolote, lililoamua kuunda serikali za nchi (majimbo), yenye nguvu au kubwa ndani ya nchi na likabaki salama na mfano ni USSR, Yugoslavia n a kadhalika.

Kwa wale wanaodai Serikali ya Tanganyika, labda wana malengo mengine zaidi ya malengo makuu, yanayojionesha waziwazi. Lakini, kwa hoja wale wanaodai serikali 3, hawana zaidi ya kutumia rejea za watu ambao wengi wao sasa hivi ukiwauliza, bado wanaamini muundo wa serikali mbili ndio bora.

Nimtolee mfano mwanazuoni, Profesa Issa Shivji ambaye kwa wengi ni kama `darasa’ la masuala ya Katiba. Kama kweli tunataka kuendelea na Muungano wetu ni dhahiri kwamba hatuna haja ya kuunda serikali ya tatu.

Badala yake, turekebishe kasoro zilizojitokeza ili tuimarishe Muungano wetu wa Tanganyika na Zanzibar. Tukibaki na mfumo wa sasa, tutaendelea kubaki salama na kwa kuwa tunaelekea kupata Katiba mpya, bila shaka miaka 50 ijayo tutakuwa tumepiga hatua kubwa kimaendeleo.

Mungu Ibariki Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wale wanaotaka kutugawa kwa sababu zao binafsi, washindwe na walegee.

Mwandishi wa wazo hili ni Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kutoka Wilaya ya Temeke.

MOJA ya misemo maarufu ya Rais mstaafu Ali Hassan ...

foto
Mwandishi: Phares Magesa

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi