loader
Dstv Habarileo  Mobile
Tushirikiane kufichua wahalifu

Tushirikiane kufichua wahalifu

Mapema wiki hii, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, iliwakamata watu wawili, mmoja aliyejifanya askari wa Usalama Barabarani, akiendelea na ukaguzi wa makosa ya usalama barabarani na mwingine mwenye ulemavu wa mguu, akiuza dawa za kulevya.

Inasikitisha, kwa kuwa watuhumiwa wote ni vijana ambao wana nguvu na wanaoweza kufanya kazi halali na kupata kipato halali cha kujikimu wao na familia zao, na pia vijana hao ndio taifa la kesho lakini, kama wao ndio wanaofanya uhalifu, vijana wadogo walio nyuma yao kwa umri wanaiga nini?

Katika tukio la mwenye ulemavu kuuza dawa za kulevya, polisi waliweka mtego baada ya kupata taarifa kuhusu nyendo za kijana huyo, Said Tindwa (30) ambaye anashikiliwa kwa tuhuma za kuuza dawa za kulevya kwa kuzificha kwenye mguu bandia wake.

Kijana huyo ana ulemavu na anatumia mguu bandia wa kulia, hivyo kupitia ulemavu huo, akaona ni vyema yeye kufanya biashara ya dawa za kulevya, ili hali akijua jambo hilo ni kosa na biashara hiyo ni haramu hapa nchini.

Jambo hilo linatia dosari watu wengine wenye ulemavu, kwani ingawa sio mtazamo wa kila mmoja, lakini wananchi wataona kuwa walemavu wanatumia ulemavu wao kufanya maovu, jambo ambalo sio wote wafanyao hivyo, bali ni wachache kama alivyo huyo, Said.

Tukirudi kwa huyo aliyejifanya askari wa usalama barabarani, naye ni kijana mwenye nguvu ambazo angeweza kuzitumia kufanya kazi halali na kuwa mzalendo wa nchi yake, lakini anafanya kosa la udanganyifu.

Kama yapo matukio kama hayo, ni wazi kwamba watu kama hao katika jamii wapo na wanafanya mbinu mbalimbali kupata fedha au kutapeli watu na huenda wengi bado hawajagundulika, au wapo wanaofahamika ila jamii inawafumbia macho.

Mwito wangu kwa jamii, ni kuwafichua watu kama hao kwa kuwa wanachokifanya sio jambo la tija kwao na kwa taifa, bali linabomoa na kujenga kizazi cha utapeli badala ya kubuni mambo halali ya kurutubisha uchumi wa nchi.

Kuwafichua wahalifu kama hao kunasaidia kulinda amani na usalama wetu, kwani vitendo kama hivyo ndivyo vinavyochangia pia kuwapo kwa wahalifu wa ndani na nje ambao baadhi yao hushirikiana na baadhi ya raia wasio wema, kufanya uhalifu.

Tukumbuke kwamba Tanzania itajengwa na sisi, na usalama wa nchi na mali zetu uko mikononi mwetu wenyewe, hivyo ili vyombo vya usalama viweze kufanya kazi yake vizuri, vinahitaji ushirikiano wa Watanzania wote, kwani tunawajibika kutoa taarifa za kufanikisha kuwakamata wahalifu popote walipo.

Ikiwa kila mmoja wetu atashiriki kikamilifu kwenye nafasi yake, uhalifu nchini utaisha kama sio kupungua na kwamba si sahihi kuwaachia polisi au vyombo vingine vya usalama kwa suala la ulinzi wa raia na mali zao, bali ni vyema tushiriki kwa pamoja kwenye harakati za kuhakikisha uhalifu unadhibitiwa.

Ni vema tukaacha tabia ya kukumbatia wahalifu, kwani tunawafahamu kwa kuwa wanaishi ndani ya jamii, ila kwa kuwa tu ni rafiki au majirani zetu, tunashindwa kutoa taarifa ama kwa kuona sio wajibu wetu au wengine kwa kupuuzia tu mambo.

Tuwafichue wahalifu, tujenge taifa safi na vijana wetu wajifunze kufanya kazi halali na kuchukia uhalifu ili baadaye tujivunie kuwa na taifa lenye vijana wanaopenda kazi halali na yenye tija kwao na kwa taifa.

WIKI iliyopita umefanyika uzinduzi wa siku ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi