loader
Tutumie fursa ya kupata vitambulisho vipya vya kura

Tutumie fursa ya kupata vitambulisho vipya vya kura

Tume hiyo ilieleza kuwa katika uboreshaji huo, vitambulisho vyote vya kupiga kura nchini, vitatolewa vipya kwa wananchi wote, huku ikibainisha kuwa baada ya kutolewa vipya, vile vya awali vitakuwa havitambuliki.

Katika kuhakikisha hilo linafanikiwa, NEC ilisema wamejipanga kukamilisha uboreshaji huo na vitambulisho kutumika katika kupiga kura za maoni kupata Katiba mpya, baada ya mchakato wa Bunge Maalumu la Katiba kumalizika.

Aidha, ilieleza kuwa vitambulisho hivyo, ndivyo vitatumika katika kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwakani ili kuweza kupata viongozi bora, huku ikihamasisha vyombo vya habari na viongozi wa dini, kuhamasisha wapigakura kujitokeza kujiandikisha na pia kupiga kura.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva alisema katika uboreshaji huo, itatumika Teknolojia mpya ya Biometric Voter Registration (BVR), ambayo ni kuchukua au kupima taarifa za mtu za kibaiolojia au tabia ya mwanadamu na kuzihifadhi katika Kanzidata (database) kwa ajili ya utambuzi.

Taarifa za kuanza uboreshwaji wa daftari hilo la wapigakura, imefika muda muafaka na kutoa matumaini kwa wadau wengi, ambao walikuwa wakilalamikia daftari la awali kuwa na kasoro mbalimbali.

Tume hiyo ilikiri kuwapo kwa kasoro hizo ; na kueleza kuwa mfumo mpya wa uandikishaji utakaotumiwa katika uboreshaji huo, utasaidia katika kuondoa kasoro hizo za awali na kuboresha vitambulisho hivyo na kuwa vya plastiki, kuliko vya awali ambavyo viliweza kuchezewa na watu kwa kutengeneza vitambulisho feki.

Napenda kuipongeza NEC na Serikali kwa hatua hiyo na mikakati madhubuti ya kuhakikisha suala hilo linafanikiwa.

Lililobaki ni wadau wa kada tofauti, kuhamasisha wananchi kujitokeza na kujiandikisha ili waweze kupata haki yao ya msingi ya kupiga kura.

Pia, wananchi wenye sifa ya kupiga kura, wanatakiwa kutumia fursa hiyo vema kwa nia ya kuweza kupiga kura na kujenga demokrasia katika nchi yetu, kwani sasa kila mtu anafahamu umuhimu wa vitambulisho hivyo.

Ni jambo la kushangaza, ikiwa wananchi watashindwa kujitokeza kupata vitambulisho hivyo, ambavyo ni msaada katika masuala mbalimbali mbali na kupiga kura wakati huu, ambao mchakato wa kupata vitambulisho vya taifa ukiendelea.

Tume iliwaomba viongozi wa dini na vyombo vya habari kwa muda huu kuhamasisha wananchi.

Pia iliwataka wadau wote, wanaopata nafasi ya kukutana na wananchi, kuhamasisha kushiriki uandikishaji huo. Imani yangu ni kuwa iwapo viongozi wa dini, kwa umoja wao watatumia nafasi zao za kusikika na kuaminika, kuhamasisha jambo hili kwa waumini wao, ambao ni wapigakura, jambo hili litafanikiwa.

Kufanikiwa kwa wapigakura kujiandikisha, pia ni mafanikio ya kuongezeka kwa wapigakura, ambao NEC imeeleza wamekuwa wakipungua kila wakati, kutokana na sababu na changamoto mbalimbali.

Napenda kuipongeza Tume kwa kuona changamoto hizo na baadhi yake kufanyiwa kazi, ikiwa ni pamoja na uandikishaji kufanyika katika ngazi ya vitongoji, vijiji na mitaa, tofauti na awali ambapo ulikuwa katika ngazi ya mtaa.

Katika uandikishaji na wapigakura kwa sasa, vituo vimeongezeka kutoka 24,919 hadi 40,015 ili kuwa karibu na wananchi na kuongeza mwamko wa kujiandikisha na kupiga kura. Hatua hii itasaidia kuondoa misongamano katika vituo na kurahisisha mazoezi hayo.

Lakini wakati mipango ya uboreshaji ikiendelea, ni vema NEC ikafanyia kazi ushauri uliotolewa na viongozi wa dini, ambao ni pamoja na kuangalia siku ya kupiga kura kutokuwa ya ibada, kuajiri wasomi badala ya walimu na muda wa kujiandikisha na kupiga kura kuongezwa hadi saa 12 jioni.

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) inazidi kuimarika.

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi