loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ugonjwa wa mnyauko waiua Kagera kiuchumi

Takwimu zilizopo zinaonesha kwamba asilimia 80 ya wakazi wa Kagera hutegemea ndizi kwa chakula ama kujipatia kipato na hivyo kama ugonjwa huo unaoendelea kujichimbia mkoani humu usipodhibitiwa mapema kwa kuwekewa mikakati stahili na sheria kali, utasababisha madhara makubwa zaidi.

Deus Edward, mfanyabiashara wa ndizi katika soko kuu la Bukoba na ambaye pia husafirisha katika mikoa jirani ya Mwanza na Shinyanga, anasema mwaka 2010 walikuwa wakinunua mkungu mmoja wa ndizi kwa kati ya Sh 3,000 mpaka Sh 5,000 lakini kutokana na upungufu wa ndizi kwa sasa wananunua mkungu mmoja kwa Sh 30,000 hadi Sh 40,000.

“Kwa msingi huo, ili upate faida unalazimika kuuza mkungu kwa bei ya juu, kati ya Sh 50,000 mpaka 60,000,” anasema.

Edward anasema kupanda kwa bei ya ndizi mkoani humo kumesababishwa zaidi na ugonjwa wa mnayauko, kwani sehemu kubwa ya migomba imeathirika na kufanya ndizi kutopatikana kwa wingi hasa katika wilaya za Karagwe na Kyerwa ,ambako asilimia 80 ya ndizi zinazolimwa mkoani humo hutokea. Wilaya hizo mbili ndizo zilizokumbwa na ugonjwa huo kwa asilimia kubwa.

Mariam Kasilima, ambaye naye ni mfanyabiashara wa ndizi, anasema hali ya uchumi kwa wafanyabiashara wa zao hilo mkoani Kagera inaendelea kuporomoka siku hadi siku kwani upatikanaji wa ndizi umekuwa mgumu tofauti na siku za nyuma kabla ugonjwa wa mnyauko kuukumba mkoa.

“Kwa kweli hali ya pato la wafanyabiashara wa ndizi kama mimi limepungua sana. Kwa miaka yote tumekuwa tukitegemea kwenda vijijini, hasa Karagwe na Muleba kukusanya mikungu ya ndizi na kusafirisha kuleta kuuza katika soko kuu la Bukoba au kupeleka mikoa ya Mwanza na Shinyanga, lakini siku hizi ukusanyaji huo umekuwa mgumu.

“Unaweza kukodisha gari ukasafiri kwenda Karagwe, umbali usiopungua kilometa 150, lakini unakuta mzigo (ndizi) hakuna. Unalazimika kurudi na mzigo nusu au bila mzigo kabisa na hivyo unaingia hasara ambayo hukuitarajia. Kama ambavyo ugonjwa huu unarudisha nyuma maendeleo ya wafanyabiashara kiuchumi, ndivyo pia unavyoathiri wakulima ambao wanategemea ndizi kama chakula na pia kuuza ili wapate fedha ya zaida kwa ajili ya matumizi mengine,” anasema Kasilima akionesha masikitiko.

Anasema wao kama wafanyabiashara wanaiomba Serikali kulitazama hili kwa makini na kuchukua hatua madhubuti haraka, la sivyo kilimo cha migomba kitakuwa historia katika mkoa wa Kagera, kwani hali inazidi kuwa ngumu siku hadi siku.

“Kwa kweli mimi nafikiria kubuni mradi mwingine utakaonisaidia kujikwamua na umasikini kwa sababu biashara yangu kubwa ilikuwa kuuza zao la ndizi ambayo sasa ni kama imeshindikana,” anasema Kasilima.

Rutahwa Mubezi, mkulima wa ndizi kutoka katika Wilaya ya Karagwe, anasema anamiliki shamba la ndizi lenye ekari sita ambamo miaka minne iliyopita alikuwa ana uhakika wa kuvuna wastani wa tani tatu hadi nne za ndizi na kuwauzia wafanyabiashara watokao Bukoba na Mwanza ambapo alikuwa na uhakika wa kutia kibindoni kiasi cha shilingi milioni 30 kwa msimu mmoja tu, lakini hivi sasa huambulia nusu tani ama hata chini ya hapo kwa msimu.

Anasema kutokana na ugonjwa huo, miche ya migomba shambani mwake imekuwa ikiathiriwa vibaya na ‘unyanjano’ na kumfanya avune kiasi kidogo sana, jambo ambalo anasema limesababisha uchumi wake kushuka.

“Pato langu linazidi kuporomoka kutoka shilingi milioni 30 nilizokuwa ninapata kwa msimu hadi kati ya shilingi 700,000 hadi Sh milioni moja. Yaani pato limepungua sana kiasi kwamba malengo yangu yamepotea. Kwa mfano nilipanga kununua gari la kunisaidia kubeba mizigo pale ninapofuata mzigo vijijini ili ile fedha ambayo ninatumia kukodisha magari iwe kama faida. Ugonjwa huu umenipa pia wakati mgumu katika kusomesha watoto wangu,” anasema mkulima huyo.

Anasema kwa vile hawezi tena kununua gari kutokana na kipato kutoka shambani kwake, anajipanga kuchukua mkopo ili atimize malengo yake hayo ambapo gari hilo linaweza pia kutumika kwa biashara zingine za kubeba mizigo na kumuingizia kipato. Costansia Katunzi ni mama aliyejiajiri kwa kuuza pombe ya kienyeji aina ya lubisi inayotengenezwa kwa kutumia ndizi.

Anasema malengo yake yamepotea kwani upatikanaji wa ndizi za kutengenezea pombe hiyo umekuwa mgumu kutokana na mashamba mengi kushambuliwa na unyanjano. Kutokana na hali hiyo, Katunzi ambaye hana taaluma nyingine ya kumuingizia kipato zaidi ya kupika lubisi, anasema hata kipato chake kimeshuka sana kwani ndizi zimepanda sana bei licha ya kupatikana kwa taabu.

“Zamani, lubisi ilikuwa inaniingizia Sh 300,000 mpaka 400,000 kwa mwezi, lakini kwa sasa mapato yangu yameshuka sana. Ninajikuta kwa mwezi mzima ninapata kati ya Sh 50,000 mpaka 70,000 tu, kiasi ambacho ni kidogo na hata nashindwa kuendesha maisha yangu kwani hicho kinachopatikana ndio mtaji wangu niliouingiza wakati naanza biashara hiyo,” anasema.

Mtafiti Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Mazao na Kilimo (ARDI) Maruku, kilichoko Bukoba Vijijini, Sayi Bulili, anasema ugonjwa wa mnyauko (unyanjano) unaenezwa na vimelea aina ya bakteria ambao hushambulia migomba na kwamba uko tofauti na magonjwa mengine ambayo pia yamekuwa yakishambulia zao hilo.

Anasema bakteria hao wakishashambulia mgomba lazima mmea huo ufe tofauti na magonjwa mengine ambayo hayaui kabisa mgomba. Bulili anasema ugonjwa huo ambao mpaka sasa hauna dawa inayoaminika hushambulia aina zote za migomba isipokuwa migomba aina ya Fia ndiyo inayouhimili kwa muda mrefu, ingawa nayo huathiriwa kwa kiasi fulani.

Anasema kwa Tanzania ugonjwa ulionekana kwa mara ya kwanza mwaka 1952 katika mkoa wa Kagera lakini serikali ya Kikoloni iliweka sheria ambayo iliwabana wananchi na kuweza kuutokomeza ndani ya kipindi kifupi.

Anasema mnyauko uliingia tena Tanzania mwaka 2006 katika kata ya Izigo Wilaya ya Muleba mkoani Kagera ukitoka nchi jirani ya Uganda, na kwamba kwa sasa ugonjwa huo umeenea hadi katika mikoa mingine ya jirani inayolima migomba japo si kwa wingi kama vile Mara, Kigoma, Geita na Wilaya ya Ukerewe.

Anakiri kwamba jitihada za haraka zinatakuwa kuchukuliwa ili kunusuru wananchi wanaotegemea zao hilo kwani kadri ugonjwa huo unavyozidi kujichimbia ni hatari zaidi kwa wananchi. Anasema Wilaya ya Kyerwa inaongoza kwa ugonjwa huo kwa kuwa na mashamba asilimia 85 yaliyoathirika, Karagwe aslilimia 70, Bukoba asilimia 65, Muleba asilimia 60, Missenyi asilimia 55, Ngara asilimia 35 na Biharamulo ina asilimia 25.

Anasema ugonjwa huo unaweza kudhibitiwa kwa urahisi kama wakulima na wadau wengine watazingatia kanuni zilizotolewa na wataalamu ambazo ni za gharama nafuu kama vile kuondoa ua dume kwa kutumia mti mkavu wenye panda pale chane ya mwisho inapojitokeza ili kuzuia wadudu kama nyuki wasisambaze vimelea vya ugonjwa wakati wa kufyonza utomvu mtamu kutoka kwenye ua dume.

Njia nyingine anasema ni kutotandaza maganda ya ndizi nje ya shamba na badala yake kuyafukia shimoni ama kuyachoma.

Njia zingine anasema ni kutotandaza takataka za migomba ambazo mtu hafahamu zilikotoka, kuchimbua migomba iliyoathirika na kuikatakata vipande vidogo vidogo na kuirundika pamoja na kisha kuitia kiberiti au kuchimba shimo na kuifukia, kunawa mikono baada ya kuhudumia mimea iliyoathirika na kusafisha vifaa vilivyotumika kwa kutumia JIK na maji au vifaa hivyo kuvipitishae katika moto ili kuua vimelea visije kuathiri shamba zima.

Bulili anazitaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni majani ya mgomba iliyoathirika kuwa ya njano na kukauka huku ndizi zikibadilika rangi na kuwa za kahawia ambapo ikimenywa hutoa harufu mbaya. Bulili anaamini kwamba endapo wananchi watakubali kufuata masharti ya wataalamu huku wanaokaidi wakibanwa na sheria ugonjwa huo unaweza kutokomezwa kwani Uganda wameweza kuutokomeza kwa njia hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fabian Massawe anasema mkoa umeanza operesheni tokomeza unyanjano kwa kuhakikisha kila mtu anawajibika kutokomeza ugonjwa huo ambapo kamati za ulinzi na usalama zimewekwa kuanzia ngazi ya vijiji. Anasema kamati hizo zitakuwa mstari wa mbele kusimamia wakulima kudhibiti kuenea kwa ugonjwa na kuleta taarifa za udhibiti wa ugonjwa huo kila mwezi katika uongozi wa mkoa ili kujua kama hali inaimarika ama la.

foto
Mwandishi: Angela Sebastian

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi