loader
UKAWA kurudi bungeni kufuata posho ni aibu

UKAWA kurudi bungeni kufuata posho ni aibu

Bunge hilo Maalumu lilianza Jumanne Februari 18, mwaka huu na kuzinduliwa rasmi na Rais Jakaya Kikwete huku likiwa na idadi kubwa ya wajumbe lakini sasa linatarajiwa kusitishwa likiwa na wajumbe wachache tofauti na lilivyoanza mapema mwaka huu kutokana na changamoto kadhaa zilizojitokeza.

Nasema hivyo, kutokana na kundi la wabunge linalounda Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutoka vyama vya Chadema, Cuf na NCCRMageuzi wakiwamo pia baadhi ya vyama vingine na wale wa kundi la wajumbe 201, wakiwa wamesusia mkutano huo.

Ingawa Ukawa walijiengua bungeni, shughuli za Bunge ziliendelea kama kawaida siku iliyofuata hadi lilipoahirishwa kupisha Sikukuu ya Pasaka, na baada ya sikukuu hiyo wajumbe waliobaki walitakiwa kujaza fomu kwa ajili ya kupewa posho ya vikao.

Lakini kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Bunge hilo la Katiba, Samuel Sitta baadhi ya wajumbe wa Ukawa walionekana katika ofisi za Mhasibu wa Bunge hilo kujaza fomu ili kupatiwa posho bila kuhudhuria vikao hivyo wakidhani wafanyakazi wa Idara ya Fedha hawatawafahamu na kuwalipa posho.

Si nia yangu kutoa msimamo juu ya hatua ya Ukawa ya kususia Bunge, lakini ukweli unabaki kuwa sababu ya wajumbe hao kutoka katika vikao vya Bunge hilo ni madai kuwa mchakato huo hauendi sawa kwa maslahi ya Taifa sasa iweje tena wanarudi na kutaka posho?

Ninafikiri kila mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, bila kujadili chama chake, au hisia zake za ndani anajua fika kwamba ana wajibu mkubwa wa kuhakikisha kwamba Tanzania inapata Katiba mpya kama ilivyopangwa kulingana na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Tena Katiba hiyo iwe kwa maslahi ya nchi kwani wao wako pale wakiwakilisha Watanzania wengi walio nje ya Bunge hilo Maalumu lakini kwa kitendo na kutaka posho bila kufanya kazi waliyotumwa ni sawa na wizi na wameonesha wazi kuwa wako kwa ajili ya maslahi yao na si maslahi ya nchi.

Ni aibu kwa wajumbe hao waliotoka katika kikao hicho kurudi na kudai posho mbalimbali ambazo ni fedha za wananchi bila hata aibu kwani inaonekana wazi kuwa wako katika kikao hicho kwa ajili ya posho na si kuhakikisha nchi inapata Katiba bora tena kwa maridhiano.

Napenda kupongeza uongozi wa Ofisi ya Bunge kwa kufuatilia suala hilo la kulipa posho na kuhakikisha wale ambao hawakuingia katika kikao hicho hawapati posho hizo bila kufanya kazi ikiwa ni pamoja na fedha za kujikimu ambazo zinatolewa kwa mjumbe aliyepo Dodoma na kutohudhuria kikao kwa idhini ya Mwenyekiti wa Bunge.

Lakini, napongeza uongozi huo kwani hawakufanya kwa wajumbe wa Ukawa pekee bali kwa wote ambao hawahudhurii vikao bila sababu kwani ni dhahiri kuwa wajumbe hao walichaguliwa kwa ajili ya Bunge Maalum la Katiba na si kwa ajili ya kupewa posho hata kama wahajahudhuria vikao hivyo.

Katika suala hili, ninawasihi Ukawa kumaliza tofauti zao na kurejea bungeni mara litakapoanza tena kwani ni vyema kupeleka hoja zao katika Bunge hilo Maalum na si kukaa nje na kutaka kupewa posho kwani huko si kuwatendea haki Watanzania waliowatuma kuwawakilisha katika Bunge hilo.

KATIKA ukurasa wake wa habari za kimataifa ...

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi