loader
Ukimwi, malaria bado tishio kwa Taifa

Ukimwi, malaria bado tishio kwa Taifa

Akizungumzia malaria, Makamu wa Rais alisema watu bilioni 3.3 sawa na nusu ya idadi ya watu waliopo duniani kote, wako hatarini kupata ugonjwa huo. Alisema hiyo ni kwa takwimu zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Hata hivyo, alisema kutokana na hatua zilizochukuliwa na dunia katika kuzuia na kupambana na ugonjwa huo, sasa vifo kutokana na malaria, vimepungua kwa asilimia 33 barani la Afrika.

Alifafanua kwamba nchini, malaria ni moja ya magonjwa ambayo husababisha vifo kwa kiwango kikubwa.

“Takwimu zinaonesha kuwa ugonjwa wa malaria ni tishio la maisha ya Watanzania pamoja na juhudi za Serikali za kupambana na tatizo hilo, natumia nafasi hii kuwahimiza Watanzania wenzangu kuhakikisha tunafuata sheria na ushauri wa wataalam pindi dalili za malaria zinapojitokeza. Lakini ni lazima pia tuhakikishe kuwa kasi ya upatikanaji wa dawa za mseto za malaria na kasi ya kutoa matibabu kwa wagonjwa inaongezeka, kutumia vyandarua vyenye dawa na matumizi sahihi ya dawa kwa akina mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano yaongezeke na kupewa kipaumbele,” alisema.

Makamu wa Rais pia aliwataka Watanzania kutambua kuwa Ukimwi nao ni tishio kwa taifa, ambapo ripoti ya viashiria vya ugonjwa huo nchini, vinaonesha kuwa mwaka 2011/012 asilimia tano ya Watanzania wenye umri kati ya miaka 15-49, walikuwa wanaishi na VVU na Ukimwi.

Alisema ripoti hiyo, pia inaonesha kuwa kiwango cha maambukizi kwa wanawake kiko juu kwa asilimia sita, ukilinganisha na asilimia nne ya wanaume.

Akizungumzia Mwenge wa Uhuru, Makamu wa Rais aliwakumbusha Watanzania kukumbuka bila kuchoka falsafa za Mwenge wa Uhuru za busara, hekima, uzalendo na upendo kama zilivyoasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kabla ya Uhuru.

“Sisi tunataka kuwasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo mahali palipo na chuki na heshima palipo na dharau, ” Dk Bilali alinukuu falsafa hizo za Mwalimu Nyerere.

Alisema kuwa matukio ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru, miaka 50 ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar, yamedhihirisha uwepo wa umoja na mshikamano wa wananchi. Aliwaomba Watanzania kuweka maslahi ya Taifa mbele kuliko kitu kingine chochote.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fabian Massawe alisema Mwenge huu umulike na kuchoma pale penye malumbanano ya kisiasa na kidini na kuondoa makandokando yaliyopo baina ya wananchi wa Kagera ili kuleta maendeleo.

WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso ...

foto
Mwandishi: Angela Sebastian, Bukoba

Post your comments