loader
Dstv Habarileo  Mobile
Utafiti wa gesi Z. Tanganyika kazi ngumu-Muhongo

Utafiti wa gesi Z. Tanganyika kazi ngumu-Muhongo

Profesa Muhongo alisema hayo bungeni jana alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi), aliyesema kuwa utafiti huo umekuwa ukisuasua kutokana na makosa ya Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC).

Mkosamali alitaka Serikali ieleze imechukua hatua gani, na kama kuna hasara iliyotokea, ni kiasi gani na inawahakikishia nini wananchi wa Kigoma na Watanzania kwa ujumla kuhusu mwenendo wa wawekezaji na utafutaji mafuta katika mkoa huo.

Akifafanua zaidi, Profesa Muhongo alisema mwekezaji aliyekuwa akifanya utafiti hapo, Kampuni ya Total, ni moja ya kampuni tano duniani zenye uwezo wa kufanya utafiti huo, lakini aliondoka kwa kuwa haukuwa na maslahi kwake na hakusababisha hasara yoyote kwa nchi.

Awali, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga, alisema Serikali ina dhamira ya dhati ya kumpata mwekezaji katika utafutaji mafuta na gesi asilia katika Bonde la Ziwa Tanganyika eneo la Kaskazini.

Alisema katika mchakato wa kumpata mwekezaji, Serikali huzingatia maslahi ya taifa na kuhakikisha kwamba mwekezaji anapata nafasi ya kurudisha gharama za uwekezaji na faida stahiki.

Alifafanua kwamba kulikuwa na majadiliano kati ya Serikali kupitia TPDC na mwekezaji Total, lakini yalivunjika baada ya upande wa Serikali kubaini mambo matatu ambayo hayakuwa na maslahi kwa Taifa.

Kwa mujibu wa Kitwanga, katika majadiliano hayo Serikali ilibaini kuwa Total haikuwa tayari kulipa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), ilikuwa inataka kutoa mgawo mdogo wa mapato kwa Serikali na ilikataa kufuata taratibu za kiuhasibu za Makubaliano ya Kugawana Kitakachozalishwa (PSA).

Baada ya kuvunjika kwa mazungumzo hayo, Kitwanga alisema Serikali ilitangaza kuwa eneo la Ziwa Tanganyika Kaskazini kuwa liko wazi na Oktoba mwaka 2013 ilizindua duru ya nne ya kuitisha zabuni za utafutaji mafuta kwenye vitalu saba vya baharini na kitalu cha Ziwa Tanganyika Kaskazini.

Zabuni hiyo ilifunguliwa Mei 15, 2014. Alisema Serikali inafanya jitihada za kutafuta wawekezaji wenye uwezo wa kifedha na kiteknolojia, ili wafanye kazi ya kutafuta mafuta na gesi katika Ziwa Tanganyika.

Alisisitiza kuwa Serikali itahakikisha kuwa wawekezaji watakaopatikana wanazingatia maslahi ya wananchi wa Kigoma na Taifa kwa ujumla, endapo kutakuwa na ugunduzi wa mafuta au gesi katika Ziwa Tanganyika.

HALMASHAURI ya Manispaa ya Morogoro imepata nmkopo ...

foto
Mwandishi: Joseph Lugendo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi