loader
Vibindo wataka ada za leseni ziondolewe

Vibindo wataka ada za leseni ziondolewe

Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Gaston Kikuwi alisema jana kuwa viwango vilivyowekwa na Serikali kwa sasa, siyo rafiki kwa wafanya biashara wadogo, kwani ni vikubwa mno.

Alisema wafanyabiashara wameonesha katika utafiti waliofanya, kumudu viwango visivyozidi Sh 20,000 kwa mijini na Sh 10,000 vijijini.

Alitaka viwango hivyo vilipwe mara moja tu; na siyo kila mwaka, ili kuwavuta wananchi wengi kuingia katika biashara iliyo rasmi.

“Baada ya Serikali kurudisha ada za leseni za biashara, tumefanya utafiti na kugundua kuwa viwango hivyo vya Sh 50,000 kwa miji na halmashauri, Sh 30,000 wilayani na Sh 10,000 kwa wafanyabiashara wa vijijini, bila kujali kiasi cha mtaji alichonacho mtu, vitawaondoa wengi na kuwafanya washindwe kujikimu kimaisha,” alisema Kikuwi.

Alifafanua kuwa mwaka 2003, Serikali iliondoa ada za leseni baada ya kuonekana kuwa zilikuwa ni kero kubwa, ambayo ilizuia malengo ya Serikali ya kukuza biashara na hasa biashara ndongo ili kuinua kipato cha mwananchi wa kawaida na kupunguza umasikini.

Lakini mwaka 2011, Serikali ilianza tena mchakato wa kurudishwa ada hizo kupitia Sheria ya Fedha Namba 5 ya mwaka 2011.

Mwaka huo serikali ilitunga sheria ya usajili wa biashara, iliyoruhusu mabadiliko ya ada hizo na biashara tofauti, kuwekewa ada tofauti, mijini, wilayani na vijijini.

Kikuwi alisema cha kushangaza zaidi ni kwamba viwango hivyo, vilikuwa vikubwa zaidi ya vile vilivyokuwa vimerudishwa kupitia Sheria hiyo ya Fedha Namba 5 ya mwaka 2011.

Alisema lengo la Vibindo, kufanya utafiti wa athari za ada hizo, lilikuwa kujua viwango ambavyo wafanyabiashara ndogo wangependa vitumike.

Aliongeza kuwa utafiti huo ulifanyika katika miji ya Dar es Salaam, Mwanza, Morogoro, Songea na Masasi na ulihusisha wafanyabiashara ndogo na wakati wapatao 616.

“Asilimia 98 ya wafanyabiashara ndogo na wa kati waliohojiwa, walieleza kutofurahishwa na kurudishwa kwa ada hizi na vile vile kupanda kwake, wakitoa sababu kuwa biashara zao nyingi zina mitaji isiyozidi Sh 200,000,“ alisema Kikuwi.

Alisema ada hizo za leseni ni sehemu tu ya mlolongo wa ushuru, ambao wafanyabiashara wadogo na wakati, hulazimika kulipa ili kuweza kufanya biashara.

Ushuru mwingine ni wa soko, malipo ya kukodi duka/sehemu ya kufanyia biashara, ushuru wa usafi, malipo kwa ajili ya ulinzi, kodi ya mamlaka ya mapato, kodi ya huduma na malipo ya ukusanyaji taka.

Kikuwi alisema duniani kote Ripoti ya Maendeleo Duniani ya mwaka 2005, zimeonesha kwamba kuweka mazingira mazuri ya kukuza ajira za uhakika na kuruhusu ukuaji wa biashara ndogo na za kati ni vitu muhimu, iwapo Serikali itadhamiria kuondoa umaskini katika jamii.

“Pamoja na kwamba takwimu za mwaka 2012 za Wizara ya Viwanda na Biashara zinaonesha kuwa Tanzania ilikuwa na biashara ndogo na za kati zinazofikia 3,100,000, utafiti wetu umebainisha kuwa endapo Serikali haitafikiria kuondoa au kupunguza viwango hivi vipya vya ada za leseni, biashara ndogo na za kati 300,000 zipo hatarini kufungwa,” alisema.

Kufungwa kwa biashara hizi, ambazo ni asilimia 10.3 ya wafanyabiashara waliohojiwa, kutaathiri maisha yao na ya familia na kuongeza kwa kiasi kikubwa tatizo la ukosefu wa ajira nchini.

Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Misaada la taifa hilo ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi