loader
Wachimbaji wadogo nchini kaeni mkao wa kula

Wachimbaji wadogo nchini kaeni mkao wa kula

Miongoni mwa mikakati yake ni kuhakikisha kuwa wachimbaji wadogo wanawezeshwa kwa kupatiwa mashine za kisasa za uchimbaji na kuhakikisha Watanzania nao wanafaidika na rasilimali za madini zinazosimamiwa na shirika hilo.

Pia Stamico inataka ianze kutoa gawio kwa Serikali ili iwe kama yalivyo mashirika mengine ya umma ambayo kila mwaka sehemu ya faida yake inapelekwa Hazina ambayo ndiyo mwenye mali.

Viongozi wa Stamico wanasema kwamba lengo lao ni kuhakikisha wachimbaji wadogo wanawezeshwa kuwekeza na kuchimba kisasa zaidi ili pia watoa mitaji ambao ni benki wawe na uhakika wa fedha zao kurejeshwa.

Hii ina maana kwamba Stamico ina mpango wa kuwawekea dhamana wachimbaji wadogo ili wakakope kwenye taasisi hizo za fedha baada ya kuboresha taarifa zao na kuhakikisha kuwa linakuwa ni kundi ambalo linaweza kukopesheka.

Ni jambo la kutia moyo kuwa Stamico imeanza kukifanya kile ambacho kimekuwa kinapigiwa kelele na Watanzania walio wengi wa kutaka wachimbaji wadogo wa madini wasaidiwe na Serikali yao.

hatua hii ya Stamico inapaswa kupongezwa na wapenda maendeleo. Sio wasaidiwe fedha, ila wamekuwa wanaomba Serikali iwakopeshe vifaa vya kuchimbia madini ili waweze kuipata rasilimali hiyo iliyoko chini ya ardhi kirahisi kama ilivyo kwa wawekezaji wakubwa ambao wana zana za kisasa.

Wachimbaji wadogo wamekuwa wanataka wasaidiwe kupatiwa zana za kuchimbia ili nao waweze kufaidika na rasilimali za taifa lao.

Mfano ni kule Mererani ambako wachimbaji wadogo wanatumia zana dhaifu kuchimba madini ya tanzanite wakati wawekezaji wa Kampuni ya Tanzanite One wanatumia zana za kisasa.

Matokeo yake ni kwamba mwenye mitambo ya kisasa ya uchimbaji madini wanafaidika kwa kuchimba zaidi na kufika maeneo ambako wachimbaji wadogo hawawezi kufika.

Hali hii imefanya wawekezaji wa kigeni kufaidika zaidi kupata tanzanite na kuwaacha wachimbaji wadogo ambao ni wazalendo na wazawa wakisuasua kwa kupata mawe machache.

Hili wanalofanya Stamico la kuwanunulia mashine za kisasa wachimbaji wadogo ni vyema liwe la kudumu na liwe endelevu ili sekta hiyo ya wachimbaji wadogo iweze kukua na kuwa na manufaa kwa taifa.

Kada hii ya wachimbaji wadogo ni kundi ambalo lina watu wengi ambao maisha yao, familia zao na ndugu zao yanategemea uchimbaji mdogo wa madini.

Lakini pia iwapo watakuwa na zana za kisasa pia watatoa mchango mkubwa kwa Serikali kwa kulipa kodi kubwa kuliko ilivyo sasa. Hivyo kwa sasa uchimbaji mdogo ni shughuli kubwa ya uchumi kama ilivyo kilimo na ajira rasmi.

Kila Mkoa hapa nchini ukienda, lazima utakuta kundi hili la wachimbaji wadogo wakihangaika kuchimba madini ili waweze kupata fedha ya kujikimu.

Ukienda Kahama, Nzega, Tunduru, Singida, Tarime, Mererani, Biharamulo na maeneo mengi utakuta kuna makundi mengi ya vijana ambayo yanavamia maeneo ambako wanaamini kuna dhahabu au madini mengine yamegundulika.

Juzi tumesikia huko Loliondo namna maelfu ya watu watu walivyomiminika huko kwa ajili ya kwenda kuvuna dhahabu ambayo imeripotiwa kuwa imegundulika huko.

Hivyo ni jukumu la Serikali kupitia shirika hilo la Stamico kuhakikisha kuwa kundi hili la wachimbaji wadogo nalo linaanza kufaidika na rasilimali zetu.

Madini ni zawadi ambayo nchi hii imepewa kutoka kwa Mungu, naamini kama kungekuwa na mipango mizuri ya kuwaendeleza hawa wachimbaji wadogo, leo hata makundi ya vijana ambao hawana ajira mitaani yangepungua.

Hivyo napongeza hatua hii ya Stamico ya kutaka kuanza kuwawezesha wachimbaji wadogo ambao kwa miaka mingi wamekuwa wanalilia namna ya kuwezeshwa na Serikali yao ili waweze kufanya shughuli zao kwa tija zaidi.

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) inazidi kuimarika.

foto
Mwandishi: Shadrack Sagati

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi