loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wafanyakazi sekta isiyorasmi walalamikia manyanyaso

Wafanyakazi wanaolalamika ni pamoja madereva wa magari ya mizigo na mabasi ya abiria maarufu kama daladala, mabasi ya safari ndefu, mafundi cherehani katika viwanda vidogo, watumishi wa ndani na wauza maduka makubwa jijini Dar es Salaam.

Saleh Hashim ambaye amefanya kazi ya kuendesha daladala zinazofanya safari zake katikati ya jijini Dar es Salaam anasema amefanya kazi kwa miaka mitatu kwa saa 14 kila siku pasipo kupata likizo wala fidia kutokana na ajali.

Hashimu anasema ni jambo la kawaida kwa dereva kuondoka nyumbani kwake saa 10 alfajiri na kurudi kati ya saa sita na saa saba kila siku baada ya kuwa kazini kuanzia saa 11:00 alfajiri. Anasema wafanyabiashara waliowekeza katika sekta ya usafiri wanakandamiza wafanyakazi kwa kuwalipa ujira mdogo, kuwanyima likizo na haki ya kupumzika siku za sikukuu za kitaifa.

Hali kadhalika baadhi ya madereva wa mabasi ya safari ndefu wanalalamika kuwa wanafanya kazi kwa muda mrefu kutokana na ubahili wa waajiri wao wa kuajiri madereva wawili katika basi moja.

Hamsa Sulemani ambaye anayendesha mabasi yanayofanya safari zake Kigoma kwenda Dar es Salaam anasema kwa kawaida basi la safari inayozidi saa 10 linapaswa kuwa na madereva wawili lakini mabasi mengi yana dereva mmoja pekee, jambo linalowalazimu kuendesha gari kwa zaidi ya saa 12 bila kupumzika.

Samson Mallya ambaye anaendesha lori la mizigo kutoka Tanzania kwenda nchi za jirani, hasa Rwanda na Burundi anasema hufanyakazi kwa muda mrefu bila kupumzika kwa sababu baadhi ya waajiri huajiri dereva mmoja na msindikizaji mmoja bila kujali kuwa safari ni ndefu.

Lakini kubwa wote hao wanalalamika kufanya kazi bila mkataba rasmi na mwajiri unaowawezesha kupata haki nyingi za msingi ikiwemo matibabu na akiba ya uzeeni. Juliana Kimaro anayefanya kazi ya ufundi ya kushona katika kiwanda kidogo cha mjasiriamali aliyebobea katika biashara ya nguo anasema kuwa yeye na wenzake sita wanafanyakazi kwa saa 13 katika siku sita za kazi bila malipo ya ziada.

Kimaro anaeleza kuwa Siku ya Jumapili hufanyakazi kuanzia saa nne hadi saa 12 jioni na hakuna malipo yoyote ya ziada wala hawapewi likizo ya mwaka wala siku za mapumziko. Pia wauzaji wa maduka makubwa ni miongoni mwa wafanyakazi wanaolalamikia ukiukwaji wa haki za wafanyakazi kwa kufanyishwa kazi muda mrefu bila malipo ya ziada, kunyimwa likizo na muda wa mapumziko.

“Nimefanya kazi kwa miaka miwili bila kupumzika hata siku moja… Tunaomba serikali ituangalie sisi watumishi wa sekta isiyo rasmi kwa kuwa waajiri wetu hawatutendei haki,” anasema Abbas Masambele. Masambele ni miongoni mwa wafanyakazi wanaouza maduka makubwa eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam ambao wanalalamikia vitendo vya ukiukaji wa sheria na kanuni za kazi katika sekta isiyo rasmi.

Masambele anasema baadhi ya wajasiriamali ambao wamefanikiwa kufungua maduka makubwa jijini Dar es Salaam wana tabia ya kunyanyasa wafanyakazi na kuwanyima haki zao za msingi ikiwa ni pamoja kuwanyima muda wa mapumziko, likizo, ujira mdogo na kumkata mfanyakazi sehemu ya mshahara kufidia hasara anayopata mwajiri.

Baadhi ya wafanyakazi wanaouza maduka makubwa huingia kazini saa moja asubuhi kwa lengo la kupanga bidhaa na kufanya usafi kabla kisha kuuza bidhaa kati ya saa 2:30 asubuhi hadi saa 11:30 jioni. Baada ya kufunga duka huchukua tena saa moja hadi saa moja na nusu kwa kuwa ni lazima wafanyakazi hao wahesabu na kuhakiki fedha za mauzo ya siku kabla ya kuondoka. Pia hulazimika kuhakiki bidhaa zilizobaki na kuzirudisha kwenye ghala ambako kuna ulinzi imara zaidi.

“Wafanyakazi wa maduka tunafanyakazi kati ya saa 11 hadi 12 kwa siku bila malipo ya ziada na mchana tunapewa kati ya dakika 10 hadi 30 kwa ajili ya chakula cha mchana na anayezidisha nusu saa anaweza kufukuzwa kazi kwa kosa la uvivu na uzembe kazini,” anasema Masambele.

Idadi kubwa ya wafanyakazi hawa wanafanya kazi siku zote isipokuwa Jumapili ambapo maduka mengi hufunguliwa kati ya saa nne asubuhi hadi 10 jioni, hivyo katika siku ya mapumziko ya juma wafanyabiashara hao hufanya kazi kwa saa sita hadi tisa.

“Wafanyakazi wengi wa maofisini na watoto wa shule hutumia siku za kupumzika ya wiki na sikukuu za kitaifa kufanya manunuzi hivyo sisi tunalazimika kuwa kazini muda wote pasipo malipo ya ziada,” anasema mfanyakazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Amos Sadiki. Sadiki anasema tatizo la ukosefu wa ajira linatumiwa kama kiboko cha kuwachapa wafanyakazi katika sekta isiyo rasmi kwa sababu wanapojaribu kuzungumzia haki zao wanafukuzwa kazi na wengine wapya huajiriwa mara moja.

“Hapa Kariakoo hutakiwi kuzungumzia haki za wafanyakazi… Ukiumwa na kushindwa kufika kazini kwa siku mbili unafutwa kazi, hakuna mapumziko ya wiki wala likizo ya mwaka na hata ukifiwa kupata ruhusa ni taabu sana,” anasema Sakidi. Sadiki anaendelea kusema, “Jambo la kusikitisha ni kwamba baadhi ya waajiri huwakata wafanyakazi mishahara kufidia hasara inayotokana na manunuzi yao ya jumla, pia maduka yanapofungwa kutokana na mgomo unaoitishwa na waajiri wenyewe.”

Akitoa mfano Sadiki anasema, baadhi ya waajiri waliwakata watumishi wao mshahara kwa madai kuwa walipata hasara kutokana na kitendo cha kufunga maduka kwa lengo la kupinga bei za mashine za kielektriniki za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Pia mfanyakazi akisababisha hasara hata kama ni ndogo hufukuzwa kazi mara moja na kutakiwa kufidia hasara hiyo vinginevyo utashtakiwa kwa kosa la wizi.”

Sadiki anasema ingawa wanatamani kujiunga na vyama vya wafanyakazi wanashindwa kufanya hivyo kutokana na ukosefu wa ajira pia mazingira ya kazi ambapo idadi kubwa ya waajiriwa katika maduka ni ndugu, jamaa na marafiki wa wafanyabiashara wenye maduka.

Idadi ndogo ya wafanyakazi katika duka moja inasababisha wafanyakazi hao kushindwa kufungua chama cha wafanyakazi kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Namba 6 na 7 ya mwaka 2004 ambayo inaeleza wafanyakazi wapatao kumi mahala pa kazi wanayo haki ya kuunda tawi la chama chao husika.

Kwa nyakati tofauti wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi wanaomba Serikali kufanya utafiti juu ya matatizo yao na kurasimisha shughuli za wajasiriamali wa kipato cha juu na kile cha kati ili kutoa haki kwa wafanyakazi wanaopata ajira katika sekta hiyo.

Akizungumzia matatizo wa wauza maduka, Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa hifadhi ya mahoteli, majumbani, huduma ya jamii na ushauri (CHODAWU) anasema wauzaji wa maduka makubwa hawapaswi kujiweka kwenye kundi la sekta isiyo rasmi badala yake wanakuwa kwenye sekta binafsi kwa sababu waajiriwa wao wamesajiliwa na wanalipa kodi kwa mujibu wa sheria za nchi.

Anasema wafanyakazi wa maduka makubwa wanastahili malipo kwa kufanya kazi kwa muda wa ziada na kwamba kitendo cha kufanyakazi siku za mapumziko ya juma na katika sikukuu za kitaifa kinapaswa kuwa cha maridhiano kati ya wafanyakazi na waajiri pasipo kushurutishwa.

“Kuna mazingira yanayowafanya watu wawe kazini kipindi cha sikukuu za kitaifa au siku ya mapumziko ya wiki… Lakini ni lazima kuwe na maridhiano kati ya muajiri na muajiriwa,” anasema Wamba.

Wamba anafafanua kuwa sehemu ya 24 na 25 ya sheria ya kazi na mahusiano kazini ya 2004 na sehemu 7 ya sheria ya mshahara ya 2010 zinaeleza kuwa mfanyakazi atakayefanya kazi siku za mapumziko ya juma au wakati wa sikuu za kitaifa atakuwa na haki ya kulipwa asilimia 200 ya mshahara wake wa siku.

“Kama muuza duka analipwa Sh 2,000 kwa siku atapaswa kulipwa Sh 4,000 ikiwa watafanya kazi siku ya mapumziko ya wiki pia atalipwa kiasi hicho wakati wa sikukuu za taifa zikiwamo za kiserikali na zile za kidini,” anaeleza Wamba. Anasisitiza kuwa muda rasmi wa kufanyakazi ni saa tisa kwa siku na saa 45 kwa wiki, hivyo Mwajiri haruhusiwi kumtaka mfanyakazi kufanya kazi kwa saa za ziada kama hawana makubaliano kuhusu malipo ya muda wa ziada.

Hata panapokuwa na makubaliano mwajiri na mfanyakazi hawaruhusiwi kuzidisha wastani wa muda wa saa za ziada ambao ni saa 50 kwa mwezi. Pia wafanyakazi hao wanapaswa kupewa likizo ya siku 28 kwa mwaka, likizo ya uzazi na siku za mapumziko kutokana na ugonjwa au kuuguliwa na mtoto, hivyo waajiri wa sekta binafsi wanapaswa kuzingatia sheria za kazi.

Sikukuu ya wafanyakazi huadhimishwa duniani kote Mei Mosi kila mwaka kwa namna mbalimbali ambapo wafanyakazi wanapata fursa ya hutathmini mafanikio ya kazi, kuimarisha umoja na mshikamano na kupima hali ya mahusiano na ushirikiano baina ya waajiri, wafanyakazi na serikali.

Chimbuko la vyama vya wafanyakazi linatokana na kukua na kukomaa kwa ubepari ambao ulizua matatizo mengi kwa wafanyakazi ikiwemo kufanyishwa kazi kwa saa nyingi, kati ya 14 hadi 18 kwa siku. Mishahara midogo iliyolipwa kwa ubaguzi, mazingira machafu ya kazi, ajali nyingi kazini, kufukuzwa kazi kiholela, kukithiri kwa vitendo vya uonevu, unyanyasaji na udhalilishaji.

Mazingira yaliyosababisha kuundwa kwa vyama vya wafanyakazi katika karne ya 18 bado yapo hadi leo hii, kutokana na tabia ya matajiri (waajiri) kuwanyonya na kuwakandamiza wafanyakazi, jambo linalojitokeza pia nchini kwa waajiri wanaojiweka katika sekta siyo rasmi ili kukwepa kulipa haki za wafanyakazi.

foto
Mwandishi: Kaanaeli Kaale

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi