loader
Waganga hawa matapeli wa ngono, washughulikiwe

Waganga hawa matapeli wa ngono, washughulikiwe

Waganga hao huku wakijua wazi hawana uwezo, wanatangaza kusaidia watu matatizo mbalimbali wanayojua kabisa kutokana na hayo, lazima mtu atakuwa tayari kufuata masharti yao ili tu aondokane na tatizo hilo.

Miongoni mwa tiba wanazodai kutoa waganga hao ni pamoja na kurudisha mke, mume au mpenzi aliyekuacha, kuongeza nguvu za kiume na maumbile kwa wanaume, kuleta bahati, kutoa majini ya ulinzi, pete za ulinzi na bahati, utajiri, mazindiko na kuwezesha wanawake wagumba kupata mimba.

Baadhi ya waganga hao, pamoja na Serikali kuweka wazi hakuna tiba kwa baadhi ya magonjwa, hujinadi kuyatibu magonjwa hayo ikiwemo Ukimwi.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Temeke, Dar es Salaam jana lilitangaza kuwakamata vijana wawili ambao ni waganga wa jadi. Uganga wao ni kuwaingizia dawa wanawake sehemu zao za siri kwa kufanya nao mapenzi, na kuwaahidi kupata mimba.

Kukamatwa kwa vijana hao kwa mujibu wa Polisi ni baada ya wananchi kulalamika kwa muda mrefu, kufunguliwa kesi kadhaa za utapeli wanaoufanya.

Kibaya zaidi wana leseni waliopewa kwa mgongo wa kutoa tiba asili, kumbe wahuni. Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Englibert Kiondo, watu hao huwaingilia kimwili wanawake wenye shida ya kupata watoto wakiwaambia kuwa wanawaingizia dawa ili waweze kupata mimba na baada ya kukamilika tendo hilo wanaacha nguo zao za ndani kwao.

Kiondo anasema waganga hao wanasambaza vipeperushi kupata wateja sehemu mbalimbali wakijidai kutibu magonjwa mbalimbali ikiwemo kisukari, vidonda vya tumbo, nguvu za kiume, kukuza maumbile, kupata kazi, kufaulu mtihani, mvuto wa biashara, kumilikishwa jini na kupewa pete ya bahati.

Hali hii ni ya hatari sana kiafya na pia kimaendeleo kwani haifai kufumbiwa macho hata kidogo na mamlaka husika kwa kuwa kutokana na kufanya ngono bila kinga, wanatumika wakijua, kuhatarisha maisha ya wenzao.

Nakubaliana kabisa na Kamanda Kiondo kwamba jamii inapaswa kuelimishwa zaidi kujua madhara yanayoweza kuwapata kwa kuamini ushirikina ni suluhisho la matatizo yao katika kufaulu, kulinda ndoa, kufanikiwa kibiashara na kimaisha.

Binafsi sioni uhusiano wowote wa mtu kufaulu wakati hajasoma anategemea dawa ya mganga, hii ni kudumaza akili za vijana ambao tunategemea ndio viongozi wa sasa na wataalamu wa afya na uchumi.

Wakati vyombo vya dola vikiendelea kuwashughulikia matapeli hawa, niombe wananchi wenzangu kuzinduka na kuwa macho na matapeli hawa, tusikubali kurubuniwa. Niombe Serikali kamwe isisite kuwachukulia hatua kali ili iwe fundisho kwa wengine.

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) inazidi kuimarika.

foto
Mwandishi: Regina Kumba

Post your comments