loader
Dstv Habarileo  Mobile
Wajumbe wataka sura ya ardhi Katiba mpya

Wajumbe wataka sura ya ardhi Katiba mpya

Mjumbe Doreen Maro kutoka kundi la 201 anayewakilisha wafugaji, alisema pamoja na Katiba kutambua kuwa ardhi ndio rasilimali kuu, inapaswa kuwa na sura maalumu itakayoelezea mgawanyo wake na namna ya kutatua migogoro baina ya wakulima na wafugaji.

“Inatosha damu ya wakulima na wafugaji iliyomwagika, Katiba hii iwe na sura maalumu inayozungumzia ardhi, si kwa ajili ya mkulima na mfugaji pekee, lakini hata mfanyakazi akistaafu, anaporudi kijijini kulima ama kufuga anahitaji ardhi,” alisema Maro.

Alisema Tanzania haitakuwa nchi ya kwanza kuweka sura ya ardhi katika Katiba na kueleza kuwa nchi ya Kenya katika Katiba yao ya 2010, Sudan Kusini kwenye Katiba yao ya 2011 na ya Uganda pia, zote zinazungumzia suala la ardhi kwa kina.

“Haitakuwa nchi ya kwanza kuweka sura ya ardhi katika Katiba, ardhi ndio kila kitu ambacho mwananchi anaweza kutumia na kufaidi matunda yake, ardhi haiongezeki bali sisi wanadamu ndio tunaongezeka, kamati yetu namba 12 iliridhia kuweka sura ya ardhi katika Katiba, naomba lisimamiwe ipasavyo,” alisisitiza Maro.

Naye Khalfan Shaaban Muhogo akijadili kuhusu sura ya kwanza na ya sita ya rasimu ya Katiba, alishauri pia kuwepo na sura maalumu ya masuala ya ardhi kama rasilimali ya pekee na kuweka wazi matumizi yake, ili kupunguza migogoro ya ardhi nchini hasa baina ya wakulima na wafugaji.

“Migogoro ya ardhi ni mingi sana nchini, wakulima wanapambana na wafugaji, wachimbaji wadogo kwa wawekezaji wakubwa, maeneo ya ufukweni sheria inasema meta 60 kutoka baharini ni maeneo huru lakini wengine wameyawekea uzio na wavuvi wanashindwa kutoka katika maeneo hayo,” alisema Muhogo.

Alisema Katiba inapaswa kutamka wazi kuwa, ardhi ni mali ya raia wa Tanzania, haiuzwi kwa asiye raia na ikiwa mtu anataka ardhi basi ikodishwe kwa muda mfupi.

Muhogo alisema ikiwa rasilimali ya ardhi itawekwa wazi katika Katiba, masuala ya kuwepo kwa migogoro ya ardhi inayosababisha hata watu kupoteza maisha, itakoma na rasilimali hiyo itatumiwa kwa mujibu wa sheria mama ambayo ni Katiba.

Naye mjumbe Adelgunda Mgaya, alishauri kuwepo kwa sura maalumu ya ardhi ndani ya Katiba ijitegemee ili kupunguza migogoro ya ardhi ya vijiji na kuongeza thamani ya rasilimali hiyo muhimu kwa raia wa Tanzania.

HALMASHAURI ya Manispaa ya Morogoro imepata nmkopo ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi