loader
Wanachama Simba msikurupuke kuchagua viongozi

Wanachama Simba msikurupuke kuchagua viongozi

Uchaguzi huo uligubikwa na changamoto mbalimbali ikiwa pamoja na kuzuiliwa kuendelea kwa uchaguzi huo amri iliyotolewa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi.

Malinzi katika agizo lake hilo la awali, aliitaka Klabu ya Simba kuunda Kamati ya Maadili hadi kufikia Juni 30, itakayokuwa na jukumu la kusimamia maadili kutokana na kusikia malalamiko kutoka kwa watu mbalimbali wakilalamikia ukiukwaji wa maadili katika uchaguzi huo.

Lakini juzi alitoa tamko la kuruhusu uchaguzi huo uendelee kama kawaida na kusisitiza amehakikishiwa na Mwenyekiti wa Klabu hiyo Ismail Aden Rage kuwa kila kitu katika uchaguzi kitaenda sawa.

Naomba kutumia nafasi hii kuwatakia kila la heri Simba katika uchaguzi wao huo wa aina yake. Ni uchaguzi ambao umekuwa na shamrashamra nyingi za hapa na pale na ambao uliwaweka wanachama wa klabu hiyo roho juu huku kila mmoja akitaka kuona mgombea wake aking’ara.

Katika nafasi ya Urais ambayo ndio inaonekana kuwa ina mwamko zaidi, wanaogombea ni Evans Aveva na Andrew Tupa. Napenda kuwasihi wanachama wa Simba kutambua kuwa mustakabali wa maendeleo ya soka kwa klabu hiyo upo mikononi mwao.

Inapaswa kujua kuwa uchaguzi wa uongozi wa klabu kubwa na kongwe kama hiyo unahitaji zaidi ya umakini wa kawaida. Umakini huo ni pamoja na kujua nani wa kumchagua kuwa Rais na viongozi wengine.

Rushwa katika kuchagua uongozi ni kitu kibaya na hasa zaidi ikizingatiwa kuwa tayari klabu ilikuwa na mwelekeo mzuri. Inabidi wachague mtu ambaye wanakuwa na imani naye katika kuisimamia, kuilinda na kuiheshimu Katiba ya Simba.

Simba inakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zinahitaji mikakati endelevu itakayoikuza klabu hiyo zaidi. Suala la kuendelea uwanja wa Simba ni muhimu pia kwa sasa kwa kuwa karibia kila klabu ina uwanja wake.

Inatakiwa wapiga kura wasikilize sera za kila mwanachama na kujiridhisha kutokana na namna anavyoweza kuzitekeleza sera husika. Pia hata kwa wagombea wenyewe wanatakiwa pia kutathmini imani kubwa ambayo wanachama wa klabu hiyo wameionesha kwao na kisha kuhakikisha kuwa wanatimiza ahadi zao.

Miaka iliyopita, kulikuwa na idadi kubwa ya wagombea wa nafasi mbalimbali katika vyama vya michezo kutoa ahadi nzuri ambazo wanajua kuwa hawana uwezo wa kuzitekeleza, lakini walikuwa wakiwahonga wapiga kura na kupata kile walichokitaka.

Chaguzi za sasa hazihitaji mtu ambaye anaweza kuwahadaa wapiga kura kwa maneno tu ila mtu ambaye anaweza kutekeleza mambo mengi katika kuendeleza soka.

Simba ni moja kati ya klabu kubwa za soka hapa nchini na inatakiwa kuwa na hadhi kubwa kulingana na ukongwe wa klabu hiyo. Zipo klabu kama Azam FC na nyinginezo ambazo zimeanza muda si mrefu, lakini zimeonesha mikakati yao ya kuendeleza soka kwa timu yao na hata kwa nchi kiujumla.

Simba kutokana na idadi kubwa ya wanachama iliyonayo inaweza kupata fedha nyingi na kuendeleza klabu hiyo ikafika mbali. Kinachotakiwa ni kuwa na viongozi wenye nia ya kuendeleza soka na kuwa na mikakati mizuri na endelevu katika kukusanya ada ya mwanachama kila mwaka.

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) inazidi kuimarika.

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Post your comments