loader
Wananchi wasisubiri maendeleo, wayatafute

Wananchi wasisubiri maendeleo, wayatafute

Kwa mujibu wa chapisho hilo lililofanyiwa uchambuzi na wataalamu wa Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), umri wa kuishi wa Mtanzania ni miaka 61, wanawake wanaongoza kwa kuishi umri mrefu zaidi wa miaka 63, wanaume wakiishi miaka 60.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, mwaka 1988 umri wa kuishi wa Mtanzania ulikuwa miaka 50 wakati wa Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, umri wa kuishi ulikuwa miaka 37.5.

Wakati anazindua chapisho hilo, Rais Jakaya Kikwete alisema takwimu hizo maana yake ni kuwa huduma za afya zimeimarika, watu sasa wanaishi kwa muda mrefu zaidi kuliko ilivyokuwa awali.

Kwa mtazamo wangu, ingawa Tanzania inatajwa kuwa ni taifa ambalo wananchi wake wana uhakika wa kuishi umri mrefu kuliko nchi zingine nne za Afrika Mashariki, kuishi miaka mingi hakutakuwa na maana kama mhusika ataishi maisha ya tabu.

Ni vizuri Watanzania tutumie takwimu kutafakari aina ya maisha tunayoishi, kwa kuwa kuna wananchi wengi wana umri unaozidi miaka 60, 70 na kuendelea, lakini hawaishi maisha bora ikiwa ni pamoja na kutokuwa na makazi mazuri, uhakika wa kupata chakula bora, tiba, na kipato cha kujikimu mahitaji yake.

Ingawa Rais Kikwete amesema, huduma za afya zimeimarika ndiyo maana umri wa kuishi umeongezeka, upatikanaji wa huduma hizo upo vipi, wananchi wa kipato cha chini hasa vijijini wakiwemo wazee wanamudu kugharimia tiba yao na familia zao?

Wakati wa kuzindua Mpango wa Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini nchini (MKUKUTA) awamu ya pili, mwaka 2012 Wizara ya Fedha ilisema, kasi ya kupunguza umasikini nchini katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, hairidhishi na waathirika wakubwa ni wakulima waliopo vijijini.

Mtazamo wa Wizara ni sahihi, umasikini upo zaidi vijijini wanapoishi Watanzania asilimia 75 ambao ni wakulima, kasi ya ukuaji wa sekta hiyo ni ndogo, hivyo ukweli ni kwamba, mantiki ya ukuaji uchumi, katika hali halisi inawagusa wananchi wachache.

Wananchi vijijini wanaweza kuwezeshwa waishi maisha bora, kwanza kwa kuelimishwa wabadili mtazamo kwamba Serikali ndiyo yenye wajibu wa kuwapelekea maendeleo, wafundishwe namna wanavyoweza kuzitumia fursa walizonazo, na pia ardhi ipewe thamani yake kuliko ilivyo sasa.

Wananchi waelimishwe, waache kuyasubiri maendeleo, wayatafute wao kupitia mazingira yaliyowekwa na Serikali kupitia fursa zilizopo ikiwemo mifugo.

Waache kufuga kwa mazoea, wafute kasumba ya kujiona wao ni tajiri kwa kuwa na idadi kubwa ya mifugo inayosababisha wawe watumwa kwa makundi makubwa ya ng’ombe, mbuzi, kondoo, punda nk. Wafugaji wabadili mtazamo, wauze sehemu ya mifugo yao waboreshe makazi yao, wasomeshe watoto, wanunue zana za kilimo kuboresha kilimo chao, ili nao waone thamani ya kuishi umri mkubwa.

Wananchi vijijini wana ardhi, Serikali inapaswa kutafuta namna ya kuwawezesha watumie maeneo yao kama dhamana ya kupata mikopo benki na kwenye taasisi za fedha ili vijana nao wapate mitaji ya kufanya ujasiriamali kupunguza kasi ya ongezeko la watu mijini.

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) inazidi kuimarika.

foto
Mwandishi: Basil Msongo

Post your comments