loader
Dstv Habarileo  Mobile
Wanaosherehekea watoto kufeli mitihani wabanwe

Wanaosherehekea watoto kufeli mitihani wabanwe

Nikabaini kwamba wana sababu tena ya msingi. Swali langu linatokana na habari iliyoandikwa katika gazeti hili kutoka Sumbawanga na Mwandishi Wetu, Peti Siyame yenye kichwa: 'Wazazi Watengeneza Pombe Kusherehekea Watoto Kufeli.'

Nikajiuliza hivi hao wazazi wanaishi karne gani inayofagilia ujinga ambao ni miongoni mwa maadui watatu wa taifa letu pamoja na maradhi na umasikini ambao ulianza kupigwa vita na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere wakati tunapata uhuru Desemba 9, 1961?

Wazazi hao wa Sumbawanga wamenishangaza sana hata baada ya miaka 53 baada ya uhuru bado wao wanaendelea kumkumbatia adui ujinga kwa kusherehekea kufeli mitihani watoto wao.

Eti, wanasherehekea kwa kufeli watoto wao, wamefaulu kukwepa mkono wa Serikali wa kufuatwa ili kulipa ada za shule, michango na fedha za mabweni kwa wasichana! Nikaamua kuingia mtandaoni kupekua ufaulu wa watoto wa Shule ya Msingi Lusaka ukoje.

Nikabaini kwamba Shule ya Msingi Lusaka, iliyopo wilayani Sumbawanga Vijijini katika Halmashauri ya Sumbawanga kwenye matokeo ya darasa la saba ya mwaka 2013, ilikuwa na watahiniwa 88, kiwilaya ilishika nafasi ya 85 kati ya 96 na kimkoa ilishika nafasi ya 309 kati ya 347 na kitaifa nafasi ya 14,432 kati ya shule 15656.

Nikabaini kumbe ndio sababu, wanasherehekea watoto wao kufeli... Katika matokeo hayo sikuona wastani wa daraja la B wala la A isipokuwa daraja la C kwa wanafunzi wachache na wengi wao walikuwa wameangukia daraja la D na wachache wengine daraja la E ambalo ni la mwisho.

Ili kujiridhisha kulinganisha matokeo hayo na shule nyingine katika halmashauri hiyo, ya Kaengesa ambayo ilikuwa na watahiniwa 80 sawa la Lusaka; lakini yenyewe kiwilaya ilishika nafasi ya nne kati ya shule 96, kimkoa nafasi ya 48 kati ya shule 347 na kitaifa nafasi ya 4,571 kati ya shule 15,656.

Katika Shule ya Kaengesa niliona wastani wa madaraja yote yaliyopo katika Shule ya Lusaka lakini kwao niliona pia wastani wa daraja la B.

Ikanipa moyo kwamba, si shule zote wilayani Sumbawanga zipo hoi kimatokeo zipo nyingine ambazo wazazi wao wanajua umuhimu wa elimu kama Kaengesa japo nao hawana wastani wa daraja A.

Kutokana na matokeo hayo, nikashawishika kuamini kwamba uamuzi wa wanafunzi na baadhi ya wazazi wakiwamo Datus Seleman na Maria Maivune wa kumwomba Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Chrispine Luanda, apeleke ombi lao mbele ya Baraza la Madiwani ili litunge sheria ndogo za kuwachapa viboko wazazi ambao wanasherehekea watoto wao kufeli, lina mashiko.

Nikaungana kusikitika sambamba na wazazi hao, wakiwamo Maivune na wenzake ambao wamekerwa na kitendo cha baadhi ya wazazi wenzao kufuja fedha kwa kunywa pombe na kuoa wanawake wengi na hivyo kushindwa kuhudumia watoto wao wanaosoma katika shule za msingi na sekondari.

Kitendo cha wanafunzi na baadhi ya wazazi wa Kata ya Lusaka wenye uchungu wa elimu kumhimiza Kaimu Mkurugenzi, Luanda afikishe ombi lao kwenye kikao cha madiwani ili watunge sheria ndogo ya kuwaadhibu wazazi na walezi wanaokataa kuwatimizia watoto wao mahitaji ya shule, naliunga mkono asilimia 100.

Naungana na wazazi wanaotaka wazazi wenzao wanaoukumbatia ujinga waminywe kwa sababu nyingi; kwanza, wanasherehekea kufeli watoto wao; pili, fedha zao wanatumia kuoa wake wengi; tatu, shule yao haifanyi vizuri katika matokeo ya darasa la saba yakiwamo ya mwaka 2013.

Vitendo hivyo vyote na vingine ambavyo havijaelezwa, vinaonesha kwamba wazazi hao wamedhamiria kwa dhati kuendelea kuukumbatia ujinga hata baada ya miongo mitano kupita tangu Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere aanzise kampeni ya kupiga vita adui ujinga pamoja na maradhi na umasikini.

Nakubaliana na Kaimu Mkurugenzi, Luanda ambaye amewathibitishia wazazi hao kwamba halmashauri hiyo itahakikisha inawabana vilivyo wazazi wote wasiotimiza wajibu wao wa kutoa mahitaji kwa watoto wao ili wasome shule.

Ni ajabu na kweli, wazazi wanasherehekea kufeli kwa watoto wao, inaniuma, naomba wazazi hao wabanwe kibano cha nguvu, kwani hawajui ujinga ni ugonjwa.

WIKI iliyopita umefanyika uzinduzi wa siku ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi