loader
Wawekezaji wa China washawishiwa kutumia EPZA

Wawekezaji wa China washawishiwa kutumia EPZA

Mkurugenzi Mkuu wa EPZA, Dk Adelhelm Meru alitoa wito huo wakati alipokuwa akitoa mada kuhusu maeneo maalum ya uwekezaji Tanzania na mamlaka yake wakati wa kongamano la pili la biashara kati ya Tanzania na China lililofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Akitoa mfano, Dk Meru alisema kuwa serikali tayari imetenga jumla ya hekta 22,000 katika eneo la uwekezaji Bagamoyo na kuwa anawahimiza wawekezaji toka nchi hiyo kuja kuwekeza katika eneo hilo.

“Tunataka eneo hili kuwa la viwanda na kituo cha biashara,” alisema. Alisema kuwa serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi iko mbioni kuendeleza miundombinu katika eneo hilo na kuwa sasa ni wakati muafaka kwa wawekezaji kuja na kutekeleza azma yao.

Alisema kuwa bandari kubwa nchini itajengwa katika eneo hilo na kuwa itabadilisha kwa kiwango kikubwa muonekano wa Bagamoyo. Katika mpango huo pia kuna kiwanja cha ndege cha kisasa na reli itakayounganishwa na ile ya kati na TAZARA.

EPZA imetenga maeneo huru na maalumu ya uwekezaji katika mikoa 20 yakiwa na ukubwa wa ekari 500 hadi 9,000 kila moja.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Viwanda wa Chama cha Wafanyabiashara, Wenye viwanda na kilimo (TCCIA) Adam Zuku alisema kuwa watanzania wananatakiwa kuzidisha ujuzi na taaluma ili kuweza kushirikiana kati ya nchi hizo mbili.

Hivi karibuni, EPZA ilisaini makubaliano na Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) kwa ajili ya kupata mikopo ya kujenga miundombinu itakayovutia wawekezaji kuanzisha viwanda katika maeneo yake maalumu.

Makubaliano hayo yalilenga kuendeleza maeneo ya mamlaka hiyo yaliyosambaa pote nchini. Kupitia makubaliano hayo maeneo maalumu ya uwekezaji kama Bagamoyo, Mtwara, Kigoma, Tanga na mengine yote yaliyo katika mikoa 20 yatapata miundombinu itakayovutia wawekezaji wa ndani na nje.

Kongamano hilo lilishirikisha kampuni zaidi ya 100 kutoka China na kampuni zaidi ya 120 za kitanzania. Hadi sasa China imesajili miradi 522 kwenye Kituo cha Uwekezaji(TIC) yenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 2.4 ambayo inatarajiwa kuzalisha ajira 77,335.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi