loader
Wazazi wanawajibika kuhakikisha haki za mtoto zinazingatiwa

Wazazi wanawajibika kuhakikisha haki za mtoto zinazingatiwa

Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika hufanyika kila mwaka Juni 16. Siku hiyo huadhimishwa na nchi zote wanachama wa Umoja wa Afrika(AU), kukumbuka mauaji ya watoto wa shule yaliyofanyika katika kitongoji cha Soweto nchini Afrika Kusini Juni 16, 1976.

Waziri wa Mendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba akizungumza na waandishi wa habari juzi alisema maadhimisho hayo hapa nchini yatafanyika katika ngazi ya Mkoa, kwa kila mkoa kufanya sherehe za maadhimisho hayo ili kutafakari vizuri matatizo yanayolikabili kundi hilo la watoto ikiwa ni pamoja na kupatiwa haki zao za msingi.

Simba alisema kauli mbiu ya mwaka huu; “Kupata Elimu Bora na Isiyo na Vikwazo ; Ni Haki ya Kila Mtoto,” ambayo inalenga kukumbusha wazazi, walezi, serikali na jamii kuhusu umuhimu wa kumuendeleza mtoto bila kubagua, kulingana na rangi, jinsia na hali aliyokuwa nayo.

Naungana na Waziri Simba kuwa bado kuna haja kubwa ya kukumbusha wazazi, walezi, serikali na jamii kwa ujumla kuwa wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha mtoto anapata haki zake za msingi ambazo katika hali halisi ya sasa watoto wamekuwa wakizikosa.

Hakuna anayeweza kubisha mazingira yalivyo sasa wakati Siku ya Mtoto wa Afrika ikiadhimishwa, kundi hilo bado linakabiliwa na changamoto kubwa wakati likiishi katika jamii inayowazunguka.

Wazazi, walezi na jamii imesahau wajibu wake wa kuhakikisha watoto wanalindwa, wanatunzwa na kuelimishwa hadi watakapofikia umri wa kujitegemea wenyewe, lakini hali imekuwa tofauti na inadhihirishwa kwa matukio ya kikatili, uonevu na matendo mengine kama hayo tunayoyashuhudia kila siku yakifanywa dhidi ya watoto.

Kuna mifano mingi inayodhihirisha namna watoto wanavyokosa haki zao za msingi, tazama hata katika miji yetu jinsia watoto wadogo wanavyorandaranda mitaani wakikosa malezi, elimu na wengine malazi yanayostahili ama kwa sababu ya kutelekezwa na wazazi na walezi, ama wazazi na walezi kushindwa kuwajibika na watoto kuamua kutoroka na kuingia mitaani ama wazazi na walezi wenyewe kuwatumia watoto kujiingizia vipato.

Katika mitaa yetu utakutana na watoto wengi wengine wakifanya biashara za uchuuzi wa vitu mbalimbali, wengine wakitumika na wazazi wao kama chambo cha kuombea fedha kwa wapitanjia na kibaya zaidi hali hiyo ya kuzurura mitaani imesababisha wengine kufanyiwa matendo maovu kama kubakwa na wengine kutumbukia katika utumiaji wa dawa za kulevya.

Jambo la kusikitisha unakutana na watoto wadogo ambao kwa umri wao wanapaswa kuwa nyumbani wakilelewa, kutunzwa au wakisoma, lakini waliopaswa kuwalinda au kuwatunza wamesahau wajibu wao.

Kama hilo halitoshi, wako wazazi na walezi wengine ndio wamegeuka watesaji na wauaji wa watoto wao, ni matukio mengi ya kusikitisha na kuogopesha kuwa hata yule aliyepaswa kuwa mlinzi wa kwanza wa mtoto wake ndio huyo anayegeuka kuwa mkatili kwa mtoto wake, inasikitisha na kuogofya sana, watoto hawa wakimbilie wapi.

Mtazamo wangu kuna kila sababu siku ya kesho jamii inapoadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika lazima ijikumbushe kuwa ina wajibu wa kuhakikisha watoto wanalindwa na kutunzwa, wazazi na walezi wakumbushwe kuwa kama wameweza kuleta watoto duniani basi wanawajibu wa kuhakikisha wanawatunza, wanawalinda na kuwapa haki zao za msingi mpaka inapofikia hatua ya kujitegemea.

Tuache hii tabia ya kulilia na kulaumu serikali kuwa haiwajali watoto, tuanze kwanza katika ngazi ya familia kuhakikisha haki za watoto zinapatikana na serikali iwajibike kwa nafasi yake kwa watoto wa taifa lake.

Naamini kama wazazi, walezi na jamii itaanza kusimama kwenye nafasi yake kama mlinzi na mtetea haki wa kwanza wa mtoto, basi Serikali nayo itakuwa katika nafasi nzuri ya kutimiza nayo wajibu wake.

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) inazidi kuimarika.

foto
Mwandishi: Angela Semaya

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi