loader
Dstv Habarileo  Mobile
Waziri Nyalandu acharuka

Waziri Nyalandu acharuka

Kampuni hiyo imefutiwa umiliki wake pamoja na vitalu vyake vyote vya Lake Natron GC East, Gobabis/ Kidunda –WMA, MKI- Selous na hatua hii pia inafuta vibali vyote vya uwindaji vilivyotolewa katika msimu huu wa uwindaji.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Nyalandu alisema amefikia maamuzi hayo baada ya kufanya uchunguzi wa tuhuma hizo zilizowasilishwa bungeni na Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa kwa njia ya DVD.

Alisema baada ya kusikiliza maelezo yaliyowasilishwa bungeni aligiza Idara ya Wanyamapori ifanye uchunguzi wa kina na kubaini ukweli dhidi ya tuhuma zinazoikabili kampuni hiyo.

“Kwanza niliagiza Idara itoe fursa kwa mtuhumiwa kusikilizwa ili kupata maelezo yake na Wizara iliita kampuni ya Green Miles Safaris Juni 5 mwaka huu na kupata maelezo ya Mkurugenzi wa kampuni hiyo,” alisema Nyalandu.

Aliongeza kuwa baada ya kusikiliza maelezo yaliyowasilishwa dhidi ya tuhuma hizo na timu ya idara ya wanyamapori kupitia video hiyo kwa kina ilibaini kuwa kampuni hiyo ilivunja sheria ya uhifadhi wa wanyama pori namba 5 ya 2009.

Alisema kampuni hiyo iliruhusu wageni wake kuwinda wanyama ambao hawaruhusiwi kwenye leseni ya uwindaji wakiwemo nyani na ndege na hii ni kinyume cha kifungu 19 (1), (2) na pia iliruhusu wageni wake kucheza na watoto wa pundamilia na ngiri kinyume na kifungu 19(1), Kufukuza wanyamapori kwa magari na kisha kuwapiga risasi wakiwa ndani ya magari.

Pia kampuni hiyo iliruhusu wageni wake kuwinda wanyama walio chini ya umri kinyume na kifungu 56(1) na kuruhusu watoto chini ya umri wa miaka 16 kuwinda kinyume na kifungu cha 43 (2)(a), wageni kuwinda huku wakipiga kelele jambo ambalo ni kero kwa wanyama na kinyume na kifungu cha 19 (1) na (2).

“Kwa kweli kampuni hii imevunja sheria ya wanyamapori ya mwaka 2009 sambamba na kanuni za uwindaji na hakuna kampuni yoyote bila kujali hadhi yake, utaifa, rangi, dini, anayeruhusiwa kuingia nchini na kuvunja sharia za Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,” aliongeza Nyalandu.

“Hatua hii iwe onyo kwa kampuni zote za uwindaji wa kitalii nchini kuhusu ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za uwindaji nchini,” alisema.

foto
Mwandishi: Sophia Mwambe

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi