loader
Dstv Habarileo  Mobile
Wenye vilainishi hafifu mkikamatwa msilalame

Wenye vilainishi hafifu mkikamatwa msilalame

Wazalishaji, waagizaji, wasambazaji na wauzaji wa bidhaa hafifu huwa mstari wa mbele kujieleza kwa vyombo ya habari kuwa wamekuwa wakionewa na taasisi za Serikali, kwa kufanyiwa misako ya kushtukiza ya bidhaa na kuharibiwa mali zao zinazoelezwa kuwa hazina ubora.

Tulijionea kilichotokea kwa baadhi ya wafanyabiashara wa mikate hasa katika maduka bubu ya mikate Dar es Salaam na wazalishaji nondo katika baadhi ya viwanda ndani ya jiji hilo, wakilalamika na kutupa lawama kwa TBS kuwa imekuwa ikiwaonea kwa kutowapa taarifa kuhusu bidhaa zao kuwa ni hafifu au zenye ubora unaokidhi viwango.

Wamekuwa wakisema kuwa badala yake shirika hilo limekuwa likiwashtukiza na kuwatia hasara kwa kuziharibu bidhaa zao. Hayo yote huzungumzwa pasipo ukweli kuwekwa wazi kuwa wafanyabiashara husika walikwisha pewa maonyo kuhusu bidhaa hafifu muda mrefu.

Tena, maonyo wanayopewa huwa ni ya maandishi kiasi cha kuweza kuwakumbusha ni nini hawapaswi kufanya au ni bidhaa za aina gani hawapaswi kuziagiza, kuzisambaza na kuziuza, lakini kwa sababu ya mazoea ya kulalama, wanapokamatwa na kuelezwa kuwa hawastahili kuendelea kuingiza sokoni bidhaa fulani wanazidi kulalamika.

Naweza kusema kuwa ulalamishi wa wafanyabiashara wanaobainika kuuza au kuingiza nchini bidhaa hafifu kama vilainishi vya mitambo na magari vilivyotajwa kuwa havifai ni njia ya kuteka akili za wateja wao (wanunuzi) na kuomba huruma ya jamii.

Nasema ni kuteka akili za wateja, kwa sababu wanapopata nafasi ya kuzungumza hasa kupitia televisheni na magazeti, huzungumza kwa kulibebesha shirika lawama na kuionysha jamii kuwa wanakuwa sahihi wakati wote, jambo ambalo si kweli kutokana na kuendelea kuzalisha, kuingiza, kusambaza na kuuza bidhaa zilizopigwa marufuku.

Malalamiko hayo wakati mwingine hufanikiwa kunasa akili za wateja (wanunuzi) ambao baadaye hudhurika na bidhaa hizo za viwango vya lazima kwa njia mbalimbali.

Kwa zile zinazoliwa kama chakula huweza kuwadhuru walaji kama ifanyavyo sumu nyingine yoyote na kwa bidhaa kama vilainishi vya magari, imekwishaelezwa kuwa hufanya mitambo na injini za magari kushindwa kufanya kazi, hivyo kuwa sababu ya ajali.

Aina 15 za vilainishi zimetajwa na TBS kuwa ni hafifu na kwamba hazifai kwa matumizi ya mitambo na magari, kutokana na ukweli kwamba zinaharibu vyuma kwa kurahisisha usagikaji wake na kutu, na wala sio kuvilainisha.

Hebu jiulizeni, hadi leo ni wanunuzi wangapi wa vilainishi hivyo wamekwisha vitumia na kuharibu magari na mitambo yao? Na je, hadi TBS ilipotoa tahadhari kupitia vyombo vya habari mbalimbali kuwa bidhaa hafifu bado zipo sokoni , ni wafanyabiashara wangapi walikwisha faidika kupitia udanganyifu huo wa kuingiza visivyofaa sokoni?

Sasa sioni sababu ya wafanyabiashara watakaokamatwa katika msako huo wa vilainishi hafifu unaokuja wakati wowote, wakiendelea kuviuza ilhali vilipigwa marufuku. Walikwishapewa muda wa kutosha waviteketeze wenyewe vilainishi vyote vilivyotajwa kuwa havina ubora na pia walipewa maelekezo na shirika hilo kuwa wazuie wanaowaletea kutoka wanakovitoa wasiwaletee tena kwa sababu havifai.

Kwa ufupi, hakuna atakayekuwa na haki ya kulalamika kama ni muingizaji, mzalishaji, msambazaji au muuzaji wa kilainishi chochote kati ya hivyo 15 vilivyotajwa kwa sababu, taarifa kuwa haviruhusiwi anayo.

Inakuwa ni vigumu kufahamu endapo wafanyabiashara wanapolalamika kuwa TBS imewaonea kwa kutekeleza wajibu wake wa kisheria kwa kuzikamata bidhaa hafifu na kuziteketeza, wanakuwa hawajielewi au ni makusudi tu, kwa sababu ya kutowajali watumiaji wanaodhurika baada ya kuzitumia na kuweka mbele tamaa ya fedha.

Nawasihi wafanyabiashara wa vilainishi vya magari na mitambo wawe wazalendo kwa kuhakikisha vilainishi wanavyoviingiza sokoni vinakidhi kiwango kilichopitishwa na shirika hilo la Viwango nchini, vinginevyo, faida yao itakuwa ni majonzi kwa wateja wao, uharibifu wa mazingira na kuua soko la bidhaa zao baadaye.

WIKI iliyopita umefanyika uzinduzi wa siku ...

foto
Mwandishi: Namsembaeli Mduma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi