Majaliwa akaribisha Irani kuwekeza katika kilimo,uvuvi

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewakaribisha wawekezaji kutoka nchini Iran kujitokeza kuwekeza kwenye viwanda mbalimbali vikiwemo vya kuchakata mazao ya kilimo na uvuvi nchini Tanzania.

“Tumedhamiria kujenga Tanzania ya viwanda, tunawakaribisha wawekezaji kutoka Iran ili waje kuwekeza kwenye viwanda vya usindikaji mazao ya kilimo na uvuvi,” amesema.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo alipokutana na Balozi wa Iran nchini Tanzania, Mousa Farhang jijini Dar es Salaam.

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda ili kuongeza ajira na kuondoa umasikini miongoni mwa wananchi wake, hivyo wanahitaji uwekezaji mkubwa kwenye sekta mbalimbali.

Pia Waziri Mkuu aliwakaribisha raia wa Iran kuitembelea Tanzania kama watalii kwa sababu kuna fursa nyingi za utalii ukiwemo Mlima wa Kilimanjaro ambao unaongoza kwa urefu barani Afrika pamoja na mbuga nyingi zilizosheheni wanyama.

Kwa upande wake, Balozi Farhang ameipongeza Serikali ya awamu ya Tano kwa dhamira ya dhati ya kuimarisha uchumi na kupambana na dawa za kulevya na ufisadi.

Amesema Tanzania ni mfano wa kuigwa na mataifa mengine barani Afrika.

“Ufisadi na dawa za kulevya ni tatizo kubwa ambalo linazikabili nchi nyingi, hivyo kitendo cha Serikali ya Tanzania kupambana na tatizo hilo ni cha kupongezwa na kitaiwezesha kusonga mbele kiuchumi,” alisema.

Balozi Farhang alisema anaishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano mzuri na Iran ambao umedumu kwa miaka 40 sasa, hivyo ameiomba ifungue Ofisi ya Ubalozi nchini Iran ili kuimarisha uhusiano huo, ombi ambalo Waziri Mkuu amekubali.

“Tanzania na Iran wana uhusiano wa kihistoria ambao unadhihirishwa na uwepo wa Washirazi wengi husan visiwani Zanzibar ambao wana asili ya Iran na maeneo ya Kusini mwa Iran kuna Watanzania wengi hata muonekano wao ni wa Kitanzania,” alisema.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu jana alifika nyumbani kwa marehemu Sir George Kahama Mikocheni jijini Dar es Salaam na kutoa pole kwa mjane Janneth Kahama pamoja na watoto na ndugu wa marehemu.