Wenye amana benki FBME kulipwa milioni 1.5/-

WATEJA wenye amana katika Benki ya FBME iliyofilisiwa na Benki Kuu, wanaweza kuanza kulipwa amana zao wiki ijayo, lakini fedha watakazolipwa hazitazidi Sh milioni 1.5.

Mkurugenzi wa Bodi ya Amana, Emmanuel Boaz aliliambia gazeti hili jana kuwa wateja ambao wana kiwango cha fedha kinachozidi kiasi hicho, watalazimika kusubiri hadi mchakato wa kuifilisi benki hiyo utakapokamilika ndipo watalipwa salio litakalobaki.

Boazi alisema bodi yake italipa kiasi hicho cha fedha kwa kila mteja na wanafanya hivyo kwa mujibu sheria ya bima ya majanga inayokatwa na benki dhidi ya wateja walio na amana katika benki husika. “Naomba wateja wa FBME wavute subira, tunawahakikishia kuwa watalipwa baadhi ya fedha zao, hawawezi kupoteza fedha zote,” alisema Boaz.

Alifafanua kuwa kwa sasa wanaendelea na uhakiki ambao alisema uko katika hatua nzuri na wiki ijayo mwishoni wanaweza kuanza kuwalipa wateja wa benki hiyo. Alisema katika uhakiki huo wanachofanya ni kuhakiki idadi ya wateja waliopo, wateja wanaodaiwa na benki hiyo, mali zinazomilikiwa na FBME pamoja na wateja wanaoidai benki hiyo.

Alisema uhakiki huo ni muhimu kufanywa na bodi ya amana. Alisema baada ya hatua hiyo bodi ya amana itateua benki mojawapo nchini ambayo italipa fedha za wateja wenye amana. Alisema wanaendelea na mazungumzo na benki moja ambayo ina matawi katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Zanzibar na Mbeya ambako FBME walikuwa na matawi.

Alisema kwa kila akaunti sheria inaruhusu kumlipa mteja Sh milioni 1.5 tu na wale ambao wana akaunti zaidi ya moja wataziunganisha na kuwalipa stahiki yao. Hata hivyo, alisema anaamini baadhi ya wateja wana salio dogo jambo ambalo litasaidia kufanya kazi hiyo ya uhakiki kwa haraka.

Alisema baada ya kukamilisha ulipaji wa amana za wateja, ndipo mfilisi ataendelea na mchakato wa kuifilisi benki hiyo ikiwa ni pamoja na kuuza baadhi ya mali za wadaiwa wa benki hiyo.

Alisema mali hizo zitauzwa ili zipatikane fedha za kuweza kuwalipa watu wanaoidai benki hiyo wakiwemo wateja wenye amana kubwa. Boaz aliongeza kuwa ni katika kipindi hicho mteja wa FBME ambaye alikuwa na deni, wataangalia dhamana iliyowekwa na kama ni nyumba, bodi hiyo ya amani italazimika kuuza nyumba hiyo au kama mteja kabakiza kiasi kidogo watakubaliana namna ya kuweza kumalizia kiasi kilichobaki