Wafanyabiashara kuhamasishwa kuwekeza kwenye vituo vya reli

SERIKALI imesema itaiomba Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) kuwahamasisha wafanyabiashara kuchangamkia fursa za kuwekeza biashara na huduma mbalimbali kwenye vituo vya reli nchini.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum, Halima Bulengo (CCM). Mbunge Halima alitaka kujua kwa nini vituo vya reli vikubwa kama Morogoro, Dodoma, Tabora na Mwanza havijawekezwa huduma muhimu kama maduka na hoteli.

Ngonyani alisema serikali inashangaa kwa nini wafanyabiashara hawachangamkii kuwekeza katika vituo vya reli ambayo ni fursa muhimu kwa biashara. “Hata hivyo wizara itawashauri TRL kuwahamasisha wafanyabiashara kuwekeza biashara na huduma kwa ajili ya wasafiri katika vituo hivyo,” alisema.

Akijibu swali la Mbunge Halima aliyehoji serikali ina mkakati gani kuboresha huduma za maji, vyoo na sehemu za kukaa wakati wa mvua ili kuwaondolea adha akinamama na watoto.

Ngonyani alisema TRL ina stesheni 124 katika mtandao wake wa reli, na tayari imeshaanza ukarabati wa stesheni za reli ambapo pamoja na mambo mengine imezingatia uboreshaji wa mifumo ya maji, vyoo na sehemu za kukaa abiria wakati wa mvua kwa kutumia vyanzo vya ndani vya mapato.

Alisema stesheni zilizokishwa karabatiwa ni Kigoma, Kaliua, Pugu, Malindi na Mwanza ambacho ukarabati wake bado unaendelea. Ngonyani alisema kampuni inatambua changamoto ya ukosefu wa baadhi ya huduma katika stesheni za reli kutokana na kuwa na miuondombinu chakavu.