SMZ yakiri kuwepo vikwazo vya kibiashara Bara

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar(SMZ) imekiri kuwepo kwa vikwazo vya kibiashara kati yake na Tanzania Bara ambavyo vimekwamisha na kuzorotesha maendeleo ya biashara kwa viwanda vya ndani nchini.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, Balozi Amina Salum Ali wakati akijibu hoja za wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliochangia bajeti yake ambapo suala la kuzorota kwa biashara kati ya Zanzibar na Bara lilitawala mjadala.

Balozi Amina alikiri na kusema ni kweli bidhaa zinazozalishwa Zanzibar zimezuiliwa kuingia Tanzania Bara, wakati zile zinazozalishwa bara zipo kwa wingi katika soko la Zanzibar. Alisema tatizo hilo kwa kiasi kikubwa limesababishwa na ngazi za watendaji na sio sera ya biashara ya taifa inavyoelekeza.

Hata hivyo, aliwaambia wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwamba mazungumzo ya kulipatia ufumbuzi tatizo hilo yanatazamiwa kufanyika kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema kwa upande wa Tanzania Bara wametuma taarifa kusema kuwa wapo tayari kukutana na ujumbe kutoka Zanzibar kwa ajili ya kulipatia ufumbuzi tatizo hilo. Alizitaja athari za vikwazo vya kibiashara viliopo kati ya serikali mbili kwa kiasi kikubwa vimeathiri maendeleo ya sekta ya biashara ya viwanda vilivyopo Zanzibar.

Alisema baadhi ya viwanda vilivyopo Zanzibar vimeyumba kwa kiasi kikubwa katika uzalishaji wake ikiwemo kiwanda cha maji ya chupa pamoja na maziwa kinachomilikiwa na kampuni ya Azam Marine.

Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliochangia bajeti hiyo walisikitishwa kuwepo kwa vikwazo vya kibiashara ambapo bidhaa za Zanzibar zimeshindwa kuingia katika soko la Tanzania Bara.

Mwakilishi wa Chaani, Nadir Abdillatif alisema kitendo cha wafanyabiashara na viwanda vya Zanzibar kushindwa kuingia katika soko la bara ni tatizo ambalo linahitaji kupatiwa ufumbuzi wa haraka.