Ujenzi viwanda vipya, kufufua vya zamani kuimarishwa

UJENZI wa msingi wa viwanda ikiwamo kuendeleza viwanda vipya na kufufua vya zamani, pamoja na kupanua ruzuku na mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ni miongoni mwa maeneo ya vipaumbele vya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa Mwaka 2017/18.

Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, miradi mingi utekelezaji wake ulianza mwaka 2016/17 hivyo inaendelea. Aliitaja miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa reli ya Kati kwa kiwango cha standard gauge, kuhuisha Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) hususan kukamilisha malipo ya ununuzi wa ndege nne, miradi ya chuma cha Liganga na Makaa ya Mawe ya Mchuchuma.

Mingine ni uanzishwaji/uendelezaji wa kanda maalumu za kiuchumi, mtambo wa kuchakata gesi asilia Lindi, na shamba la kilimo na uzalishaji sukari Mkulazi. Akizungumzia ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda, alisema itahusisha miradi ya uendelezaji wa eneo la viwanda Tamco Kibaha, tathmini ya matumizi ya eneo la kiwanda cha General Tyre Arusha, mradi wa magadi soda Bonde la Engaruka- Arusha.

Pia kuimarisha Mfuko wa Taifa wa Maendeleo ya Wajasiriamali (NEDF), uendelezaji wa maeneo ya viwanda vidogo vidogo katika mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza, Kigoma na Mtwara.

“Maeneo mengine ni pamoja na kuendeleza viwanda vya ngozi, kupanua mnyororo wa thamani wa pamba hadi nguo na uzalishaji wa madawa na vifaa tiba nchini. “Kwa lengo hili, serikali itaendelea kuhamasisha uwekezaji binafsi hususan katika viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana kwa wingi nchini ikiwa ni pamoja na viwanda vya kusindika nyama, maziwa, maji, misitu, chokaa, mawe urembo, gypsum na mazao ya vyakula na matunda,” alifafanua Dk Mpango.

Alisema serikali itaendelea kuziimarisha taasisi zake ili kuwekeza katika viwanda kwa njia ya ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi. Kuhusu kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu, alisema miradi ya eneo hili ni ile inayolenga kuimarisha upatikanaji wa fursa za elimu na mafunzo ya ufundi.

Aliitaja kuwa ni kugharamia elimumsingi bila malipo, kupanua ruzuku na mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, ununuzi wa vifaa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu, ukarabatri na upanuzi wa Maktaba ya Mkoa wa Dodoma na ujenzi wa vyuo vitano katika mikoa ya Geita, Simiyu, Njombe, Rukwa na Kagera.

Kwa upande wa afya na maendeleo ya jamii, hatua zitaendelezwa za kuboresha hospitali za rufaa na mikoa, kuhakikisha upatikanaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba na vitendanishi katika hospitali, vituo vya afya na zahanati.

Pia kuongeza udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza, na kudhibiti maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi hususan kwa vijana. Katika miradi ya maji, kutakuwa na upanuzi wa huduma za maji vijijini, kuboresha huduma za maji katika Jiji la Dar es Salaam, mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda Kahama, Nzega, Igunga, Tabora hadi Sikonge.

Mingine ni ujenzi, ukarabati na upanuzi wa huduma za maji mijini na vijijini, na kutoa maji mto Ruvuma kwenda Manispaa ya Mtwara- Mikindani. Akizungumzia mazingira wezeshi kwa uendeshaji wa biashara, Dk Mpango alisema serikali itaendelea na azma yake ya kupanua miundombinu ya huduma za kiuchumi kufikia azma yake ya kuboresha mazingira ya kibiashara.

Alisema itahusisha miradi inayoendelea ya ukarabati wa miundombinu ya reli, miradi ya barabara na madaraja katika barabara za Kidahwe- Kasulu-Kibondo-Nyakanazi, Manyoni-Tabora-Uvinza, Tabora- Koga Mpanda.

Pia ujenzi wa barabara za juu za Tazara na Ubungo Interchange, ujenzi wa Daraja la Salender na miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (awamu ya II, III na IV) jijini Dar es Salaam. Pia imo miradi ya bandari ikijumuisha bandari za Dar es Salaam, Mtwara, Tanga, Bagamoyo, bandari kavu ya Ruvu na bandari za Maziwa Makuu (Victoria, Tanganyika na Nyasa).

Kwa upande wa usafiri wa anga, alisema serikali itaendelea na ujenzi wa jengo la abiria (Terminal III) kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kigoma, Tabora na Mwanza, ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege vya Geita, Sumbawanga, Shinyanga, Mtwara, Musoma, Iringa na Songea na ukarabati wa Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).